KWA HESHIMA YA MZEE MUTARAGARA CHIRANGI ( Nyarutangwe - Omwana wa Nyamurugwa wa Kafwenyi). ALISUKUMWA NA DHANA YA KUTENDA HAKI NA KUISHI KWA 'STD' INAYORIDHISHA. ALIONGEA JUU YA HAKI, AKATENDA HAKI KI-STD, AKAITWA MZEE WA STD-MTETEZI WA HAKI. NJOO TUSHAURIANE JUU YA KUBORESHA MAISHA YETU ILI TUISHI KATIKA HAKI NA KWA STD INAYORIDHISHA
Tuesday, May 25, 2010
Monday, May 17, 2010
‘Huduma za Uuguzi zinazokidhi Viwango; Wauguzi Kuongoza katika Huduma juu ya Magonjwa Sugu)’
TAFAKURI YA KAULI MBIU KWA WAUGUZI NA
WATUMISHI WENGINE WA AFYA MKOANI MARA
KATIKA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI
(INTERNATIONAL NURSES DAY) 12 MEI, 2010
‘Huduma za Uuguzi zinazokidhi Viwango;
Wauguzi Kuongoza katika Huduma juu ya Magonjwa Sugu)’
IMEANDALIWA NA KUWASILISHWA NA :
Dr. Chirangi, Bwire, (MPH)
I. Utangulizi
Wageni waalikwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kiserikali na yasiyo ya kiserikali, Viongozi wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Wapendwa Mashujaa wa Taaluma nyeti – Wauguzi wa Tanzania,
Paukwa…., Pakawa!
Madaktari walipokuwa wamekamilisha kazi zao, wamechoka bin taabani na kupumzika, ule wakati ambapo ukimya na giza totoro vimetawala miongoni mwa wagonjwa majeruhi vitandani, yeye aliweza kuonekana akiwa peke yake na ki-taa chake mkononi akipita kuwazungukia wagonjwa na kuwahudumia ipaswavyo..
Florence Nightingale (12 May 1820 – 13 August 1910)
Habari ndiyo hiyo, iliyoleteleza mtaalamu na shujaa - Florence Nightingale, kutambulika aka mama mwenye taa (a lady with the lamp) katika kutoa huduma ndani ya hospitali ya kijeshi (Scutari hospital) huko Uturuki wakati wa vita (Crimean War) kama ilivyonukuliwa katika gazeti (Times newspaper) la Alhamis 08 Februari 1855.
Kutokana na ushujaa wake katika kufuata wito na vipawa vyake vilipomsukuma, kutokana na moyo wake wa huruma kwa wagonjwa, kutokana na uongozi wake wa mipango, kutokana na utendaji wake wa kimaadili na usafi wa kiwango cha juu, kutokana na umahiri wake katika kutunza takwimu, kuzitafsiri na kuziwasilisha kwa ajili ya kuboresha mfumo wa afya, kutokana na kuitetea na kuiboresha taaluma ya Uuguzi, Baraza la Kimataifa la Wauguzi (The International Council of Nurses kwa kifupi ICN) liliamua tuwe tunashereheka kwa kutambua mchango mkubwa wa Wauguzi wote katika Afya na Maendeleo ya jamii zetu kwa kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya shujaa wetu Florence kila tarehe 12 Mei.
Tunaipongeza ICN kwa kazi yake makini ambapo huandaa si tu kauli mbiu ( bali pia nyenzo za utekelezaji wa kauli mbiu kwa kila mwaka. Aidha nawashukuru pia Chama cha Wauguzi Tanzania kwa kazi kubwa ya uratibu kuhusiana na maendeleo ya Taaluma ya Uuguzi na pia kutukutanisha hapa leo kama iliyo kiada, wataalamu wanapowasha ile taa na kujikumbusha kiapo cha maadili ya taaluma ya Uuguzi na zaidi ya yote kutafakari mipango mkakati juu ya mada husika ya mwaka katika maboresho ya Afya ya Mtanzania.
II. Magonjwa Sugu Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya mwaka 2010
Mwaka huu Wauguzi wanapiga mbiu juu ya utoaji wa huduma za Uuguzi katika jamii zinazokidhi viwango na kuhakikisha kwamba Wauguzi wanashiriki kikamilifu katika huduma dhidi ya magonjwa sugu / sindika (delivering quality, serving communities:
Nurses leading chronic care)
Ndugu, Wauguzi wataalamu wenzangu katika huduma za afya, tukumbushane kuwa kwa mujibu wa takwimu za WHO (2005), magonjwa sugu kama vile Saratani, Pumu, Kiarusi, Shinikizo la Damu, Unyongofu (msongo wa mawazo), Kisukari n.k ndio yanasababisha asilimia 60% ya vifo vyote ulimwenguni.
Aidha kama tunafuata nyayo zake malaika wa huduma (the Ministering Angel)- Florence, katika kuwa makini na takwimu na kuzitumia katika kuboresha afya zetu, basi sote tutashirikiana kwa kuelimisha jamii kuwa ni hoja potofu isiyo ya kisayansi, kudhani kuwa magonjwa hayo sugu yanawakabiri zaidi watu wa nchi zenye kipato cha juu (matajiri). WHO (2005) inaonyesha takwimu za wazi kwamba 80% ya wagonjwa ni wale walio katika nchi za kipato cha chini na kati (Low & Middle income countries), hivyo Tanzania ni mojawapo!
Wengi wetu tumejifunza kwa namna moja au nyingine juu ya hayo magojwa kwa undani na tutaendelea kupata elimu juu ya matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu kinga, matibabu na au huduma kwa wagonjwa husika. Hapa niruhusuni nidodose tu kidog kwa nini udhibiti wa magonjwa sugu ni mada nyeti na jukumu la watu wa Mataifa yote pasi kujali utofauti wetu katika nasaba, jinsia, umri, kipato, imani wala itikadi za kisiasa .
Ni bayana Magonjwa sugu, yanatugharimu uhai wetu. bila kuchukuwa hatua, inakadiriwa kuwa jumla ya watu wapatao milioni 17 watakufa dunianii, mwaka huu kutokana na maradhi sugu.
Kwa vile magonjwa sugu ni ya muda mrefu na yenye uhitaji wa huduma za muda mrefu, maradhi haya yana madhara hasi makubwa `kwa nchi kiuchumi na kijamii. Maana yanafisha nguvu kazi katika uzalishaji na kuongeza matumizi makubwa serikali na familia husika katika kuyathibiti. Magonjwa haya yanasababisha watu kushindwa kufikia malengo yao maishani. Kuna gharama zisizo za moja kwa moja (indirect costs) kama upotezaji wa rasilimali muda makazini, mashuleni na hata majumbani n.k
Kuongezeka kwa magonjwa sugu duniani kunatokana na sababu kadha wa kadha zikiwemo ya mabadiliko ya kijamii, utandawazi, kuenea kwa maisha ya mijini (urbanization) pasipo utoshelezaji wa miundo mbinu na huduma kwa wote, kuongezeka kwa idadi ya wazee na hata ubinywaji wa haki na fursa sawa kwa wote katika mapato na huduma.
III. Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya mwaka 2010
Kwa mujibu wa Maadili ya jumla ya Uuguzi kama yanavyoainishwa na ICN – Code of Ethics, Wauguzi wana wajibu wa msingi wa kushiriki katika kuimarisha afya na kuzuia maradhi. Aidha tunakubali kushirikiana na jamii kwa ujumla kuanzisha na kuunga mkono shughuli zinazostawisha afya na mahitaji ya kijamii ya umma.
Ndugu zangu haitoshi kutambua na kulalama juu ya changamoto mbalimbali zinazotukabili leo katika taaluma ya Uuguzi nchini. Ni vyema kwa kutumia elimu, ujuzi na umoja wetu ndani ya Chama cha Wauguzi Tanzania, Vikao vya Wauguzi na Uongozi katika Vituo vya Afya husika, Bodi za Afya za Wilaya na Mikoa na hata kupitia Kitengo cha Huduma za Uuguzi katika Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, tuwasilishe matatizo yetu na mapendekezo yanayotukabili kwa hoja zenye takwimu rejea zilizotafsirika kisayansi kama Muasisi wetu, Meneja, Mtakwimu, Mkufunzi, Mshauri na Muuguzi mwana maboresho Florence alivyofanya katika kuipa Taaluma hadhi yake, kuwajengea uwezo Wauguzi na kuleta mapinduzi chanya ya mfumo katika huduma za Afya.
Shime, tushirikiane na wadau wote wa afya katika maeneo yetu kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu katika sekta ya afya (the third Health Sector Strategic Plan) 2009 – 2015 ambao uko sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millennium Development Goals) kufikia 2015 .
Tushirikiane kuelimisha umma juu ya vidokezo hatarishi vya magonjwa sugu na pia sisi wenyewe kama watumishi wa idara ya afya tuwe mfano (model) wa kuigwa katika familia zetu, makazini kwetu na katika jamii zetu kwa ujumla katika namna tunavyoishi kuboresha afya zetu; mfano:
Kuepuka uvutaji wa sigara / tumbaku
Kuepuka unywaji wa pombe uliokithiri
Kupata lishe bora kwa wakati muafaka
Kufanya mazoezi
Kuepuka ngono sisizo salama
Kudhibiti muendelezo wa msongo wa mawazo nk
Katika kutoa huduma husika kwa wakati muafaka kwa wagonjwa, wa magonjwa sugu, tunashauriwa kutumia CCM ( the Chronic Care Model) ambapo tunaunda mfumo:-
wenye mgojwa aliyehamasika na mwenye taarifa kamili, anayejiamini na kuweza kufanya maamuzi juu ya afya yake nauwepo wa timu ya Wataalamu ambao pia wana taarifa kamili juuu ya ugonjwa, maamuzi na mahitaji kwa ajili ya kutoa huduma kwa kiwango cha juu kwa kushirikiana na taasisi za afya.
Na pia kufuata ushauri wa WHO- ICC Framework, 2002 ( WHO-Innovative Care for Chronic Conditions , mkakati ambao pia unasisitiza kufanya maamuzi kwa rejea za takwimu, kulenga jamii husika, kuzuia ugonjwa, huduma bora iliyoratibiwa vyema,uwezo wa kuiga na kutumia kinachofaa kufuatana na mazingira husika na kuwa na ushirikiano miongoni mwa Wataalamuna na kuungwa mkono na jamii katika huduma zitolewazo.
III. Hitimisho
Ndugu Wauguzi na wageni wote waalikwa tofauti na siku kubukizi nyingi tulizonazo nchini, katika siku ya Wauguzi duniani hatukutani kwa sababu tu ya kusherehekea bali tunakutana kutafakari juu ya uratibu na utekelezaji wa mpango mkakati katika kutimiza kauli mbiu yetu ya mwaka husika.
Kwa moyo wa upendo, ninasajiri shukrani zangu za dhati kwa mchango mkubwa wa kipekee unaotolewa na Wauguzi popote walipo ulimwenguni hata ambapo Madaktari na Wataalamu wengine wanakuwa wamechoka bin taaban na giza totoro likitanda ama katika kumpunguzia mwanadamu maumivu au kurejesha na kuboresha siha yake au kumkarabati au kumtunza au kumwelimisha na kumshauri juu ya hamasa na utetezi wa maisha ya afya njema, kinga na au tiba ya maradhi.
Tutakiane kila la kheri tunapowasha taa zetu katika kuhamasisha mabadiliko chanya ya mifumo yetu na jamii kwa ujumla kuelekea huduma bora kwa wote na maisha yenye siha bora dhidi ya maradhi sugu yanayotukabili.
Sunday, January 3, 2010
Kumbukumbu ya Baba Chirangi Rubhoja Bhanu
'WALIGA ULI-RUBHOJA BHANU'
Tarehe 03, Januari, 2010 inakamilisha takribani miaka mitatu tangu ututoke ghafla.
Familia yako na Wanahistoria tunaendelea kukukumbuka kwa mengi uliyotufundisha kwenye njanja mbalimbali katika Uongozi, Uadilifu na Wema wako.
Katika kumbukumbu hii, dhamira zetu leo zinaguswa zaidi na tabia yako isiyokifani ya
UKARIMU ULIOKUWA NAO KWA WATU WOTE PASI KUJALI MAKABILA, ITIKADI ZA KISIASA, IMANI, JINSI, UMRI WALA HALI ZAO ZA KIUCHUMI.
Aidha haikuwa ajali Wanadamu wakati wa ujana wako wakakupa majina ya utani kama vile Rubhoja Bhanu na pia Nyamulila Mwirango utambulisho ulioashiria tabia hii ya kukarimu watu uliyoionyesha kwa vitendo pasipo uzandiki wala masharti kwa manufaa binafsi.
Tunamuomba Mola azidi kutukumbusha nasi leo kuwakarimu wageni na wahitaji kwa jinsi tunavyoweza kuwasaidia maana kwa kufanya hivyo si tu kuwa tutakuwa tunaenzi kauli mbiu
uliyoipenda ya Haki Huinua Taifa bali pia tutakuwa tunawajibika kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji mbalimbali kama tunavyotakiwa katika kujali utu na haki za kila Binadamu.
KWA HESHIMA NA SHUKRANI, FAMILIA YA CHIRANGI INAWASILISHA.
Friday, January 1, 2010
HERI YA MWAKA MPYA 2010
Ndugu zangu Watanzania,
Huku wengine tukiwa tumetengana kwa milima, mabonde, bahari, mipaka ya nchi na umbali mrefu na tukiwa katika mazingira tofauti kiutamaduni na kijiografia
nawatunuku nyote katika jina liletalo umoja na matumaini ya maisha.
“Mwenye matumaini hukesha usiku hadi auone mwaka mpya bali
asiye na matumaini hukesha ili kuhakikisha kuwa mwaka unapita”.
("An Optimist stays up to see the New Year in, a Pessimist waits to make sure the old one leaves ")Ama tuwapo Watumishi au Wanafunzi, kauli hii niliyoinukuu ya busara ya
Bill Vaughan inatugusa sote ikituhasa kuwa, tunapoingia katika mwaka mpya wa 2010 tuwe watu wa matumaini.
Pasi uzandiki sote tunapewa changamoto ya kuwa na matumaini katika:
1. Kuweka mipango na kuimarisha uongozi wetu katika kazi na katika familia zetu
2. Kutoa huduma bora zaidi kwa Wateja wetu
3. Kujifunza kwa bidii stadi anuwai zenye ufanisi katika kutatua matatizo yetu
4. Kujenga na au kuboresha Umoja na Amani katika Taasisi na kwa Taifa lote.
Ninawatakieni afya njema, kila la kheri na fanaka tunapofungua sura ya kwanza na kuanza kuiandika katika hiki kitabu kipya cha 2010.
Wakatabhau,
Musuto wa- Chirangi
Utrecht, Uholanzi,
Thursday, November 26, 2009
VETERANS
SOCCER VETERANS
Mara nyingi, Ma- 'Veterans' hutumika kwa wastaafu au watu waliotumika muda mrefu katika Majeshi. Hata hivyo ni bayana kuwa jina hilo pia tunaweza kuliazima na kulitumia kuwaenzi watu waliotumikia fani za michezo.
Katika historia ya Mpira wa Miguu Tanzania, mkoa wa Mara bado haujatukuka sana ingawa katika michezo mingine kuna Timu kama vile Buhemba JKT Handball Team na Magereza Mara - Netball Team wamewahi kuutoa Mkoa Mara kimasomaso.Aidha kuna Wachezaji na Wasanii mmoja mmoja ambao ama walitokea Mkoani Mara au wana nasaba ya watu wa Mkoani Mara pia walionekana nyota katika kushiriki michezo na sanaa mbalimbali nchini na nje ya nchi. Hawa ni kama vile Mujaya Suleiman Nyambui (Athletic), Mahesa (Basketball); Fehadah Faru (Netball); Ali Mchumila, Lucas Jamberi, Nico Bambaga, Bite John, Castor Mumbara (Soccer); Judith Wambura, Nyangómboli , Maringo Omwichukuru wa Kabondo-imbwa ya Salehe (Musicians); Sele Kum-cha (Karate)- na wengine wengi ambao kamwe sitaweza kuwaorodhesha wote.
Hata hivyo tunawakumbuka na kuwaenzi wachezaji wote wakongwe waliowahi kucheza katika vilabu maarufu vya soka huko Mara kama vile timu ya Kazi, Usagishaji, Maji, RTC,Tanesco, Mutex, Posta & Simu, Mugango, Musoma Shooting, Tarime, Seronela, Amani na Timu machachari ya muungano - Mara Stars.
Hapo juu ni picha ya pamoja ya baadhi ya Maveteran hao waliowahi kuchezea vilabu hivyo wakiwa katika uwanja wa Posta - Musoma (2008).
Monday, November 16, 2009
KITI CHA MAUTI
.jpg)
Mbele ya vipaza sauti, nje ya kituo cha kukarabati tabia cha Grerenville, Kusini mwa Richmond, sauti inasikika ikinena, “Kafa kwa amani zaidi kuliko wengi wa aliowauwa”. Hiyo ndio kauli ya Mshitaka mwakilishi wa mashahidi wa kutekelezwa kwa adhabu ya kifo (KWENYE KITI NCHA MAAUTI kwa sindano ya mauti) kwa Mdunguaji, John Allen Muhammad, aliyetuhumiwa kuua watu 10 na kusababisha hofu kuu iliyotanda jiji la Washington yapata wiki tatu, Oktoba 2002.
Historia inasema kuwa adhabu ya kifo imekuwapo kwa karne nyingi na imetolewa karibu kila kona ya dunia kwa wakosefu mbalimbali hususani waliohusika katika Uuwaji wa kukusudia, Uhaini, Usaliti (Majeshini), Ufisadi, Ukahaba na hata Ufanyaji wa biashara za madawa ya kulevya n.k kutegemeana na sheria au imani za nchi husika.
Kwa mujibu wa Amnesty International, Mwaka 2008, yapata watu 2,390 wamekufa kwa adhabu ya kifo katika nchi 25 na watu 8,864 wamehukumiwa adhabu ya kifo katika nchi 52. Tunahabarishwa kuwa Nchi zinazoongoza katika kutekeleza adhabu hii kwa mwaka 2008 ni China, Iran, Saudi Arabia, Pakistan and Marekani.
Angalau karne hii kumekuwepo na mabadiliko kiasi juu ya namna adhabu hiyo inavyotolewa katika sehemu nyingi kuliko ilivyokuwa. Hapo kale, Wanadamu waliotiwa hatiani wakahukumiwa adhabu ya kifo wame ondolewa pumzi ya uhai kwa namna mbalimbali, msisitizo ukiwa ni kufa kwa maumivu makali na au ya muda mrefu mbele ya kadamnasi ili iwe fundisho kwa wengine. Njia zilizotumika zilikuwa kama vile:-
kupigwa risari hadharani; kukoseshwa hewa kwa kufukizwa moshi au kuzamishwa majini; kuchunwa ngozi; kukatwa vipande vipande; kuchomwa moto; kuchemshwa ndani ya maji; kuchanwa vipande kwa kuvutwa na wanyama wanne;kupondwapondwa na kitu kizito sana au mnyama mzito kama Tembo; kukatwa kichwa kwa upanga; kukatwa kwa msumeno;kupigwa mawe; kusulubiwa mtini; kuachwa polini ukiwa umefungwa; kuchapwa mijeledi juu ya gurudumu la miiba; kunyongwa, kupitisha umeme mgeuko mwilini n.k.
Nadhani mabadiliko haya ya njia na hata nchi nyingine kupiga marufuku utolewaji wa adhabu hii ni zao la kukuwa kwa uelewa, mabadiliko ya kufikra, utandawazi na juhudi za Wanaharakati wa haki za Binadamu duniani kote ukiwemo Umoja wa Mataifa, Amnesty International n.k
Mjadala wa kukubali au kutokubali hukumu ya kifo ni wenye mvutano mkubwa sana duniani kwa kuwa unaibua hisia nyingi tofauti na pia kugusa imani na misimamo ya watu juu ya uhai wa Mwanadamu.
Haitoshi kusema tu kuwa malipo ya kuuwa ni kuuwawa au kwamba hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mwenziwe katika mazingira yeyote.
Hivyo kabla ya kufia uamuzi wa kuunga mkono upande fulani nashauri tutafakari bila mining’inio kwa umakini wingi na uzito wa sababu za msingi za kuunga au kutounga mkono adhabu hii ya kifo.
Aidha natoa changamoto nikiuliza kuwa;
Je tunafahamu ni wafungwa wangapi wako kwenye orodha ya kusubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo nchini kwetu; je tunafahamu adhabu hiyo hutekelezwa wapi na kwa namna gani? Je ni vyema vyombo vya habari viwe vinafuatilia na kuruhusiwa kuhabarisha wananchi pindi mtu anapoadhibiwa au karibia kuadhibiwa hukumu ya kifo?
Subscribe to:
Posts (Atom)