Friday, July 29, 2011

BURIANI WA ASK. BUTENGÉ

B
Azikwa Musoma, tarehe 27/072011.

BURIANI ASK. MSTAAFU SALMON SARIGE BUTENGÉ
Uwepo wa utulivu mahala hapa ni heshima, tafakuri na kujihoji wakati tunapata rejea ya safari ya maisha ya Mtenda-kazi wa Bwana, Ask. Salmon Sarige Butengé  japo kwa dakika moja.
Ewe kifo, unaweza kuitenga miili yetu lakini kamwe huwezi kuzitenga roho zetu, huwezi kuifuta miguso wala kumbukumbu za maisha ya Wapendwa wetu.
U wapi mauti  na machungu yako?  Hatukuongelei tena kwa kuwa umaarufu wako ulishafunikwa  na  Ufufuo  na Tumaini alilotuachia Bwana wetu Yesu Kristo.
Kama hamasa toka kwa Bibi Mahalia Jackson ilivyomgusa Mch. Martin Luther King, Jnr, na hatimaye kuteremsha mistari ya karne “Nina njozi” (I have a dream), ndivyo tulivyoweza kushuhudia  hamasa  ya kishujaa, isiyomungúnya maneno ya mama  yetu,  Bibi Ask.  Lois Sarige Butengé  akinena,
"Yaika! wa Butengé, yaika!",  katika kadamnasi hususan wakati wa Makambi pindi  Mchungaji  / Askofu Butengé  alipokuwa akitema cheche za injili mathalani  juu ya  somo la Mtenda-kazi wa Bwana au Maji yaliyo hai n.k, huko Mugumu, Bumangi, Majita, Mugango, Musoma, Nyabange, Shirati, Mwanza, Dar es salaam na kwingineko.
Ee Mola, kama huko Mbinguni pangehitajika Mkutano wa Kiroho, tusingesita kutamka kuwa Mjoli wako Salmon Sarige uliyemtwaa ni mmojawapo wa Rasilimali-Binadamu mwenye taranta husika.
Bwana umetwaa, Jina lako linaendelea kubarikiwa na bila shaka mwangwi wa sauti ya mama Lois, sasa imepokelewa na malaika wakiimba,
"Gendelela okwaika wa Buteng’e, gendelela okwaika! "
Wana Familia, Jamaa, Marafiki na Wana – KMT kwa ujumla poleni sana kwa msiba huu.

Ni sisi

Judy, Marja & Musuto  wa- Chirangi.
Utrecht, the Netherlands
26 Julai, 2011