Saturday, August 21, 2010

WOSIA KWA WAHITIMU WA 2010 KISARE NURSING SCHOOL

Vitabu katika Maktaba ya Kisare Nursing School
Wapendwa Wahitimu,
Kisare Nursing School,
Mugumu, Serengerti,

Sanjari na kuwatunuku Wahitimu vyeti husika, mara nyingi inapofika siku ya mahafali mengi yanasemwa na kuimbwa katika ama kuwapongeza au kuwahasa kama siyo kuwaangaliza katika majukumu yatakayowakabili katika jamii.

Turuhusuni nasi leo tuwatunuku nukuu chache zinazohusika na KUPATA ELIMU kama tafakuri mtakazozibeba katika fikra zenu kama zilivyoanikwa na magwiji katika nyanja na tasnia mbalimbali kama ifuatavyo:-

 “Vitabu vyaweza kuwa hatari, vile vyenye uzuri wa hali ya juu, ni vema vikawekewa tahadhari isemayo, Onyo, hiki kinaweza kubadilisha maisha yako”. Helen Exley .


 “Vitabu na maandiko yote ni tishio kwa wale wanaonuia kuiminya kweli.”
Wole Soyinka.


 “Upo utofauti kati ya mwenye ari atafutaye kusoma kitabu na asiye na ari atafutaye kitabu cha kusoma”. Gilbert Chesterton


 “Kusoma ni nauli yenye unafuu kuelekea kokote”. Mary Schmich.


 “Elimu yetu inatakiwa kutupa chanjo ya kujituma kwa ajili ya jamii nzima na kuwasaidia wanafunzi kukubali yale yanayokubalika kwa ajili ya maisha yetu ya mbeleni”. Baba wa Taifa, Mwl. J. K. Nyerere


 “Elimu ni siraha ya nguvu kubwa unayoweza kutumia kuibadili dunia”. Nelson Mandela.


 “Mizizi ya elimu ni michungu, lakini matunda yake ni matamu”. Aristotle.


 “Wakati mnaondoka hapa (Chuoni), msisahau kwa nini mlikuja hapa”. Adlai Stevenson
Masomo yenu hapa yanaweza kuwa yamefika ukingoni,
lakini kumbukeni kuwa kuelimika kunaendelea daima!
Wahitimu, Wakufunzi, Watumishi na Wadau wengine wote
hongereni sana na tunawatakieni kila la kheri.


Wenu,

Judy, Marja & Musuto Chirangi
Uholanzi, July, 2010.

Friday, August 20, 2010

MFANO WA MWANA DIASPORA SHUJAA

“…Why should my face not look sad when the city where my fathers are buried lies in ruins, and its gates have been destroyed by fire?" Nehemiah 2:3

MISINGI 10 ALIZOTUMIA MWANA DIASPORA SHUJAA


1. Kuwa na mawasiliano endelevu na nyumbani kujua si tu habari za kifamilia lakini pia maisha ya jamii na maendeleo yao kwa ujumla.
2. Kuwa na mzigo na matatizo yaliyoko nyumbani.
3. Kumshirikisha Mola katika mipango na mafanikio yetu.
4. Kutumia fursa na rasilimali tulizo nazo kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu
5. Kufanya tathinini za kisayansi za matatizo / mahitaji yetu halisi na kuweka mipango kazi na mikakati.
6. Kuhamasisha wengine na kugawana majukumu ikiwezekana kwa kujali vipaji / uzoefu / uwezo wetu.
7. Kushiriana pamoja kutekeleza mipango kazi.
8. Kutokuyumbishwa wala kukatishwa tamaa na wanaotubeza na au wanaotaka kutuondoa katika maono na mwelekeo wetu wa ki-maendeleo.
9. Kuonyesha ushujaa, kujilinda na ikibidi kupambana na wale wanaotaka vita na sisi.
10. Kusimamia haki, maadili na kuwajali wahitaji zaidi.

Kanuni hizi nimezinyambulisha nilipomkumbuka Kiongozi - shujaa mmoja katika Agano la kale, aliyeitwa Nehemia.

TAFADHALI KAMA HUJAWAHI SOMA AU KUTAFAKARI KWA UNDANI KITABU CHA NEHEMIA WAKATI NDIO SASA!
N.B Hata katika misaafu mingine kama Koran na hali kadhalika Hadith kuna mashujaa na wanamapinduzi wengi tu kama Nehemia.

Kwa kifupi tu ili kukupa hamu ya kusoma,

 Nehemia alikuwa mshika kombe (the Cup- bearer) wa Mfalme wa Uajemi. Pamoja na kuwa katika maisha mazuri huko ughaibuni na katika hiyo kazi ya watu wachache sana katika ‘special branch’, katika kuwasiliana kwake na nyumbani, alipata habari kuwa kuta za Yerusalemu & malango yake vimebomolewa na kuchomwa moto.
 Alibeba mzigo wa taabu zilizokuwa zinawakabili watu wa nyumbani Jerusalem, akahuzunika na kuomboleza sana.
 Akamwomba Mola juu ya jambo hilo
 Akatumia nafasi yake kumwendea Mfalme ambaye alimpa ruhusa na kumpa usalamana pia vitendea kazi vya kuanzia kazi ya ujenzi. (Sisi tunatumiaje vipawa na nafasi tulizo nazo kuendeleza jamii zetu?)
 Alipofika kabla ya kuanza kazi alifanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na kazi iliyotakiwa kufanywa na kupanga kazi.
 Akahamasisha wenzake na kuwaambia kuwa tujenge pamoja, kazi iligawanywa vyema kufuata uzoefu/ uwezo. Mfano Makuhani walipewa kushughulia mlango waliouzoea na kuufahamu – mlango wa kondoo!
 Watu walishirikiana wakachapa kazi mchana na usiku
 Kuliibuka akina Sanbalati, Tobian na wenzao wakawabeza na kutaka kuwaondoa kazini, lakini Nehemia alisisitiza kuwa hawezi kuacha kazi.
 Maadui walipopanga njama, ulinzi mkali uliwekwa na wakapambana nao. (Ni aibu sisi leo tunakatishwa tamaa wala hatupambani na maadui wetu katika maendeleo!)
 Nehemia aliwasimamia haki kama kuwasaidia maskini n.k na pia akawawajibisha wakiukaji ili kulinda maadili yaliyokubalika.

Hitimisho:


Yawezekana tukawa na maisha bora zaidi popote tulipo nje ya mji au nchi, inatubidi kubeba mzigo na kuhuzunika na hali yoyote mbaya (kama ipo) katika jamii zetu. Mbele ya Viongozi wetu au Mashirika yenye uwezo au yeyote mwenye uwezo wa kutusaidia kutatua tatizo lililopo, tunapaswa kusema kuwa,
“Tutakosaje kuwa na huzuni wakati mji/ nchi ya baba zetu na mama zetu ina hali isiyoridhisha?”
Halafu tufanye kweli kwa tuchukuwa hatua 10 za kuleta maendeleo kama kiongozi wa mfano Nehemia alivyofanya.

Verbal Diarrhoea Dehydrates Human Dignity. Chirangi (2000).

Tuesday, August 3, 2010

UGONJWA WA TAFSIRI NJE YA MAZINGIRA (Contextomy)


 Zao la Sanaa hiyo hapo juu ni vazi-potosha liloundwa nami mwenyewe kuonyesha jinsi ugonjwa nyemelezi wa Tafsiri nje ya mazingira yake (Contextomy) unavyoweza kuwa na athari katika kupotosha umma. 

Pata chanjo yake mapema kwa kutafakari jambo katika mazingira yake na katika ukamilifu wake!