BURIANI KAMARADE SOSPETER KONGOLA WA KARAMBA
Kwa
mara nyingine tena, kauli isiyobadilika wala kuulizwa ya Mola wetu pale
Bustanini Edeni, akinena “….hakika mtakufa” imetimia: Tarehe 18/03/1016, mauti imezuru katika
familia ya Karamba!
Kwa
butwaa na huzuni mkubwa, tulipokea taarifa hiyo iliyobeba simanzi tokana na
kifo cha Kijana Sospter Kongola akiwa
katika matibabu huko Dar es salaam.
Ewe Mauti ya Mwili
kamwe, hutaweza kutuondolea kumbukumbu ya ushirika usio mipaka na huduma
njema zenye umilisi na adala ya mtu wa watu, mdogo wetu Kongola.
Tunakiri kuwa kifo huleta simanzi, lakini imani
husababisha fikra tunduizi za maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Pale
ambapo, tunasema ni mwisho wa maisha ya kiwavi, hakika ni mwanzo wa maisha ya
kipepeo! Japo amekufa, mdogo wetu ameanza maisha mapya!
Ewe kifo, waweza
kusababisha mtanziko; tena una uwezo wa kuitenga miili yetu lakini kamwe huwezi
kuzitenga roho zetu; huwezi kuzifuta hisia zetu, kumbukumbu za maisha wala picha isiyofutika ya
tabasamu la Kongola lililoashiria ushirika wake katika jamii.
Tunamkumbuka kwa mengi ya kutufunza sisi ambao bado
tunaendelea kujaliwa nafasi ya kuishi hapa duniani. Sosy
atakumbukwa kwa ucheshi na kujenga mahusiano na watu wengi huku akiwapa misaada mbalimabli iliyokuwa
ndani ya uwezo wake.
Tunakiri kuwa: “KIFO HUACHA MAUMIVU YA MOYO, HAKUNA AWEZAYE
KUYATIBU,
BALI UPENDO HUACHA KUMBUKUMBU, HAKUNA AWEZAYE
KUIIBA”. KOMREDI SOSY KONGOLA, KATIKA KUSANYIKO HILI LENYE SIMANZI, UPENDO
WETU KWAKO UMETUACHIA KUMBUKUMBU
ISIYOIBIWA AMBAPO TUNAENDELEA KUKUPIGIA SALUTI TUKIENZI CHAPA ULIZOTUACHIA KATIKA SAFARI YA MAISHA YAKO
HAPA DUNIANI.
PENGINE WENGINE
WATAELEZA MENGINE YANAYOJIKITA KATIKA MAPUNGUFU YAKO KAMA BINADAMU AMBAYO HATA
WAO WANAYO; SISI TUTAENDELEA KUELEZA NA KUJIFUNZA NA KUYATUNUKU MAISHA YAKO YA:-
Ø UCHESHI
NA UTANASHATI
ULIOTUKUKA MAHALA POPOTE, KILA
WAKATI ,
Ø URAFIKI NA USHIRIKA MWANANA KWA WATU WENGI PASIPO
MIPAKA ISIYO NA TIJA,
Ø UTUMISHI WAKO HODARI KAMA
MFANYAKAZI KATIKA IDARA YA AFYA NA
USTAWI WA JAMII ULIYEAJIBIKA KWA MAADILI
YA UTUMISHI WAKO,
Ø USHIRIKI WAKO KWA VITENDO KATIKA SHUGHULI ANUAWI ZA SIASA, MAENDELEO YA
KIJAMII NA KIUCHUMI.
Si maandishi wala machozi yetu, yanayoweza kuonyesha kwa
ukamilifu huzuni tuliyo nayo moyoni
mwetu kwa kuachwa na mpendwa wetu. Nawasihi tumuenzi Kongola kwa kuiga yale
mema aliyoyatenda katika jamii.
Wana
Familia, Jamaa, Marafiki,Wana – KMT, Wana CCM na wafiwa wote kwa ujumla poleni sana
kwa msiba huu.
Faraja kuu na mioyo ya subira iwe nasi
sote toka kwa Rabuka wetu hata katika mwamba huu tusioweza kuupanda kama Zaburi
61:2 ituelekezavyo:
“Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia
moyo, uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda.”
Tunawapa
pole wafiwa wote kwa msiba huu mkubwa.
Buriani Sosy, Buriani Komredi Kongola.
Dkt. Musuto wa Mutaragara wa Chirangi
Mmoja wa Rafiki Wengi wa Kongola.