Saturday, April 20, 2013

AFYA JUMUISHI


Utaifa kwanza: Siku bendera ya nchi yetu ilipepea kwenye mlingoti katika 
Kitivo chetu cha Sayansi- Leiden University. Niko na Msimamizi wangu Prof. Slikerveer

Nyumbani  nikiwa na Mke wangu mwenye furaha Dr. Marja Chirangi, MD, MPH.  

Kutoka kushoto(kwako): Prof. Lionis (Ugriki), wa- Chirangi (Tanzania), Prof. Slikkerveer (Uholanzi) Prof. Joesron (Indonesia) wajumbe wa kamati ya Udaktari wa Falsafa (PhD)

Pembeni kabisa kushoto  na kulia ni Miss Judith (PhD Cand) toka Austria na Mr. Kurniawan (PhD Cand) kutoka Indonesia watu walionisindikiza kama Wapambe wa Kitaaluma (Paranymphs) kwa mujibu wa desturi za tukio hili  kwenye meza ya Utetezi wa Tasnifu 

Kushoto kwangu ni baba Mh. Prof. Muhongo ambaye pia alihudhuria na uwepo wake ulitambuliwa kipekee na Wanadhuoni  zaidi kutokana na yeye kuwa Profesa.


Hiki ndicho kitabu changu chenye Tasnifu yangu niliyoitetea yenye sura 8; kurasa 301; maneno 127,335 ambayo nimeitabaruku (dedicated) kwa Baba yetu kwa kauli ya wazi nikinena, 

This dissertation is dedicated to our beloved father, the late Mutaragara Chirangi wa Muhongo (1932 - 2007), an exemplary social, political and religious individual whose challenging legacies on innate strategic planning, efficient use of time, attention to the disadvantaged, zero tolerance on corruption, indefatigable documentation and preservation of indigenous knowledge shall continue to be evidenced in the annals of his prosopography.




 Wakati wa kusaini katika ukuta ndani ya Academy Building kuungana na wote waliowahi kuhitimu au kutunikiwa Shahada na Leiden University (Chuo cha awali Uholanzi) toka 1575 kilipoanzishwa na William, Prince of Orange. Ukutani zipo saini za akina Albert Einstein, Malkia Juliana, Malkia Beatrix, mwana wa Ufalme Willem Alexander, Nelson Mandela n.k

 

Hiki ni mojawapo ya vyumba (Senate Room) ambapo katika utamaduni na hekima ya toka enzi za mababu na mabibi katika Chuo kikuu cha Leiden watahiniwa wa uzamivu huletwa na kuulizwa maswali na jopo la wanadhuoni maprofesa kabla ya kukabidhiwa shahada za uzamivu
______________________________________

Namtukuza Mwenyezi Mungu mwenye rehema na nawashukuru Msimamizi wangu Prof. Dr. L.J.Slikkerveer, Wahadhiri wangu, Wazazi wangu, Familia yangu, Ndugu zangu, Marafiki zangu, Mwajiri wangu na Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maombi, kunipa moyo au kwa misaada yao anuwai wakati wa masomo yangu ya Udaktari wa Falsafa (Shahada ya Uzamivu).

Saa 8.00 Mchana, ya tarehe 17 Aprili 2013 nilitetea Tasnifu yangu iliyohusu:
'AFYA JUMUISHI: KUELEKEA USHIRIKIANO WA KITAALUMA KATI YA WATUMISHI WA AFYA WA TIBA YA JADI NA YA KISASA KATIKA MKOA WA MARA, TANZANIA'

Katika Ukumbi wa Kiseneta wa Chuo Kikuu cha Leiden (Leiden University), Uholanzi ambapo Mkuu wa  Chuo (Rector Magnificus) alinitunuku gombo lenye Shahada ya Uzamivu na haki zake stahiki chini ya kitivo cha Sayansi (Faculty of Science) kwa mujibu wa sheria, taratibu zihusikanazo na pia tamaduni za Taasisi za Kisomi toka hekima za enzi za mababu na mabibi .

 Tasnifu yangu ni juu ya utafiti wiani (correctional research)  ulifanyika katika Mkoa wa Mara Tanzania ambao unaolenga kuleta mabadiliko ya ki-sera katika asasi na mlimbi wa watumishi wa afya.

Zoezi hili ni kiashiria tosha cha WITO WA KUENDELEA KUWAHUDUMIA WANANCHI KWA UFANISI ZAIDI  kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu Tanzania.





Mungu ibariki Tanzania,

wa Mutaragara wa Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wa Rihu.


Sunday, January 13, 2013

KUHUSIKA KUUWA WANANCHI NA TAIFA !


Wanahabari wote Shomy (Binda News), Marato, Mgendi, Mayunga, Cales, Bonny, Timba na wengine wote na TBC, ITV, Star TV, Victoria FM, BBC(Swahili) na vyombo vyote vya habari ingawa ni wajibu wenu, binafsi nawapongeza sana kuendelea kutuhabarisha mambo kadha wa kadha. 
Leo (jana) kuna habari zimeumiza ubongo na moyo wangu sana. Kweli sote kama wananchi tuwe macho katika mambo kama haya yanayoua Raia na Taifa kwa ujumla. Habari hizo zilikuwa ni:

1. Mauaji ya kinyama ya wananchi Mkoani kwetu (imehusisha kiongozi wetu)

2. Biashara ya meno ya tembo (ikuhusisha Askari wetu) ambayo sasa ni biashara haramu iliyoratibiwa (organized crime) na taarifa ya CNN pia imethibitisha kuwa sasa biashara hii ni zaidi ya ile madawa ya kulevya na hata zaidi ya utoroshaji haramu wa dhahabu.

3. Mfanyabiashara mwizi (si mwekezaji) wa kiwanda Dar naye akishirikiana na Mtumishi wetu (kishoka) wa TANESCO wakakwepa kulipa deni la mamilioni linalowakabili la matumizi ya umeme kwa miaka na badala yake tena wakajiungia umeme bila kupitia kwenye mita na wakaendelea kuutumia bila kuulipia wakati mwananchi wa kawaida mwenye nchi anaitafuta nishati hiyo

4. Mfanya biashara wa (Dar) kukutwa anatoa stakabadhi yenye thamani ya fedha chini ya tshs. 10,000 wakati kauza zaidi ya laki moja hivyo kukwepa kulipa kodi ambayo ni pato la Taifa kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi na maendeleo ya nchi yetu. Kama mnunuzi unaweza kuona jambo dogo lakini hili janga kubwa sana katika Taifa ambalo lazima sote tubadilike kama lile la matumizi mazuri ya muda.

Musuto wa- Chirangi post on facebook
Like ·  · Promote

Thursday, January 3, 2013

KUMBUKUMBU YA BABA AMOS MUTARAGARA CHIRANGI






Leo  03/01 ni takribani miaka sita tangu atutoke baba yetu mpendwa Mzee Amos Mutaragara Chirangi.  Huwa tunatafakari kwa kurejea maisha mema ya mfano aliyotuachia baba yetu ambayo kwayo tunapaswa si tu kujivunia bali kuyaenzi wakati wa kumbukizi ya maisha yake.

Mwaka huu tunajifunza kuwa kuna MAZURI NA MABAYA ambayo yanatufika katika maisha yetu hapa duniani. Mengine tutajua sababu zake na mengine hatutajua sababu zake kwa akili zetu za kibinadamu. Hapa chini ninanakiri  mambo (makuu) mazuri na mabaya ambayo yalimpata yeye mwenyewe katika maisha yake, akawa anayakumbuka sana na yeye mwenyewe akaweza kuyaandika na kuyatunza katika moja ya makala zake ambazo sasa zinatunzwa na familia.

Twaweza kujifunza jambo toka katika hayo mazuri na mabaya maana nasi kama binadamu tulio hai yanaweza kutupata hata kama ni tofauti lakini kuna mabaya na mazuri ambayo tutapaswa kuyakabiri katika maisha yetu.

Baba yetu Mutaragara wa Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wewe ambaye uliwahi kuitwa standard ; tunakuenzi na kuendelea kujifunza katika standards zako kadha wa kadha.

Mola atujalie kukabiliana na hayo yote mazuri na mabaya yanayotufika.

Hapa chini, tafadhali pata alichokiandika mwenyewe Marehemu Baba yetu.      




MAMBO MAKUU MAWILI KATIKA MAISHA NINAYOKUMBUKA:

MAZURI
1.   Daima ninakumbuka jinsi nilivyokuwa nikichaguliwa mara kwa mara katika nyadhifa za ngazi mbalimbali, nyanja ya kidini, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni tangu nikiwa mwanafunzi na nikiwa kazini. Mara nyingi nilikuwa nikishinda wenzangu kwa kura ingawa baadhi yao niliona kuwa walikuwa na sifa zaidi yangu; nikijilinganisha katika Kisomo, Umbo, Ukoo, Umri, Uwenyeji na hali ya Kipato (Kifedha).

2.   Kazi nilizokuwa nikipewa au nikikusudia kufanya kwa ombi lolote kila mara nilipata mafanikio makubwa kuanzia asilimia ya 85-95.

MABAYA
1.   Daima ninakumbuka sana kuona watu karibu wote niliowasaidia kwa hali na mali, hawanithamini na kukataa mahusiano na ushirikiano tangu nistaafu kazi na kuachia ngazi mbalimbali nilizokuwa nazo wakati nina Kipato na Madaraka. Naona  ni shida hata kutembelewa na kusalimiwa.

2.   Mawazo yangu kutokubaliana na ya wengine katika jamii huweza huleta kutokubalika na hivyo kutoshirikishwa kwa baadhi ya maamuzi kwa kutengwa hususani katika shughuli mbalimbali za kijamii na hata kisiasa.

A.   Mutaragara Chirangi