Thursday, January 3, 2013

KUMBUKUMBU YA BABA AMOS MUTARAGARA CHIRANGI


Leo  03/01 ni takribani miaka sita tangu atutoke baba yetu mpendwa Mzee Amos Mutaragara Chirangi.  Huwa tunatafakari kwa kurejea maisha mema ya mfano aliyotuachia baba yetu ambayo kwayo tunapaswa si tu kujivunia bali kuyaenzi wakati wa kumbukizi ya maisha yake.

Mwaka huu tunajifunza kuwa kuna MAZURI NA MABAYA ambayo yanatufika katika maisha yetu hapa duniani. Mengine tutajua sababu zake na mengine hatutajua sababu zake kwa akili zetu za kibinadamu. Hapa chini ninanakiri  mambo (makuu) mazuri na mabaya ambayo yalimpata yeye mwenyewe katika maisha yake, akawa anayakumbuka sana na yeye mwenyewe akaweza kuyaandika na kuyatunza katika moja ya makala zake ambazo sasa zinatunzwa na familia.

Twaweza kujifunza jambo toka katika hayo mazuri na mabaya maana nasi kama binadamu tulio hai yanaweza kutupata hata kama ni tofauti lakini kuna mabaya na mazuri ambayo tutapaswa kuyakabiri katika maisha yetu.

Baba yetu Mutaragara wa Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wewe ambaye uliwahi kuitwa standard ; tunakuenzi na kuendelea kujifunza katika standards zako kadha wa kadha.

Mola atujalie kukabiliana na hayo yote mazuri na mabaya yanayotufika.

Hapa chini, tafadhali pata alichokiandika mwenyewe Marehemu Baba yetu.      
MAMBO MAKUU MAWILI KATIKA MAISHA NINAYOKUMBUKA:

MAZURI
1.   Daima ninakumbuka jinsi nilivyokuwa nikichaguliwa mara kwa mara katika nyadhifa za ngazi mbalimbali, nyanja ya kidini, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni tangu nikiwa mwanafunzi na nikiwa kazini. Mara nyingi nilikuwa nikishinda wenzangu kwa kura ingawa baadhi yao niliona kuwa walikuwa na sifa zaidi yangu; nikijilinganisha katika Kisomo, Umbo, Ukoo, Umri, Uwenyeji na hali ya Kipato (Kifedha).

2.   Kazi nilizokuwa nikipewa au nikikusudia kufanya kwa ombi lolote kila mara nilipata mafanikio makubwa kuanzia asilimia ya 85-95.

MABAYA
1.   Daima ninakumbuka sana kuona watu karibu wote niliowasaidia kwa hali na mali, hawanithamini na kukataa mahusiano na ushirikiano tangu nistaafu kazi na kuachia ngazi mbalimbali nilizokuwa nazo wakati nina Kipato na Madaraka. Naona  ni shida hata kutembelewa na kusalimiwa.

2.   Mawazo yangu kutokubaliana na ya wengine katika jamii huweza huleta kutokubalika na hivyo kutoshirikishwa kwa baadhi ya maamuzi kwa kutengwa hususani katika shughuli mbalimbali za kijamii na hata kisiasa.

A.   Mutaragara Chirangi

No comments: