Tuesday, March 22, 2016

REST IN PEACE - COMRADE SOSPETER KONGOLA KARAMBA




BURIANI KAMARADE SOSPETER  KONGOLA WA KARAMBA

Kwa mara nyingine tena, kauli isiyobadilika wala kuulizwa ya Mola wetu pale Bustanini Edeni, akinena “….hakika mtakufa” imetimia:  Tarehe 18/03/1016, mauti imezuru katika familia ya Karamba!   
Kwa butwaa na huzuni mkubwa, tulipokea taarifa hiyo iliyobeba simanzi tokana na kifo cha Kijana Sospter  Kongola akiwa katika matibabu huko Dar es salaam.
Ewe Mauti ya Mwili kamwe, hutaweza kutuondolea kumbukumbu ya ushirika usio mipaka na huduma njema zenye umilisi na adala ya mtu wa watu, mdogo wetu Kongola.
Tunakiri kuwa kifo huleta simanzi, lakini imani husababisha fikra tunduizi za maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Pale ambapo, tunasema ni mwisho wa maisha ya kiwavi, hakika ni mwanzo wa maisha ya kipepeo! Japo amekufa, mdogo wetu ameanza maisha mapya!
Ewe kifo, waweza kusababisha mtanziko; tena una uwezo wa kuitenga miili yetu lakini kamwe huwezi kuzitenga roho zetu; huwezi kuzifuta hisia zetu,  kumbukumbu za maisha wala picha isiyofutika ya tabasamu la Kongola lililoashiria ushirika wake katika jamii.
Tunamkumbuka kwa mengi ya kutufunza sisi ambao bado tunaendelea kujaliwa nafasi ya kuishi hapa duniani.  Sosy  atakumbukwa kwa ucheshi na kujenga mahusiano na watu wengi  huku akiwapa misaada mbalimabli iliyokuwa ndani ya uwezo wake.  


Tunakiri kuwa:  “KIFO HUACHA MAUMIVU YA MOYO, HAKUNA AWEZAYE KUYATIBU,
 BALI UPENDO HUACHA KUMBUKUMBU, HAKUNA AWEZAYE KUIIBA”. KOMREDI SOSY KONGOLA,  KATIKA KUSANYIKO HILI LENYE SIMANZI, UPENDO WETU KWAKO UMETUACHIA  KUMBUKUMBU ISIYOIBIWA AMBAPO TUNAENDELEA KUKUPIGIA SALUTI TUKIENZI CHAPA  ULIZOTUACHIA KATIKA SAFARI YA MAISHA YAKO HAPA DUNIANI.

PENGINE WENGINE WATAELEZA MENGINE YANAYOJIKITA KATIKA MAPUNGUFU YAKO KAMA BINADAMU AMBAYO HATA WAO WANAYO;  SISI  TUTAENDELEA KUELEZA  NA KUJIFUNZA NA KUYATUNUKU MAISHA YAKO YA:-

Ø  UCHESHI NA  UTANASHATI ULIOTUKUKA MAHALA POPOTE, KILA WAKATI ,
Ø  URAFIKI  NA USHIRIKA MWANANA  KWA WATU WENGI PASIPO MIPAKA ISIYO NA TIJA,
Ø  UTUMISHI WAKO HODARI  KAMA MFANYAKAZI  KATIKA IDARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII  ULIYEAJIBIKA KWA MAADILI YA UTUMISHI WAKO,
Ø  USHIRIKI WAKO KWA VITENDO KATIKA SHUGHULI ANUAWI ZA SIASA, MAENDELEO YA KIJAMII NA  KIUCHUMI.
Si maandishi wala machozi yetu, yanayoweza kuonyesha kwa ukamilifu  huzuni tuliyo nayo moyoni mwetu kwa kuachwa na mpendwa wetu. Nawasihi tumuenzi Kongola kwa kuiga yale mema aliyoyatenda katika jamii.
Wana Familia, Jamaa, Marafiki,Wana – KMT, Wana CCM na wafiwa wote kwa ujumla poleni sana kwa msiba huu.
Faraja kuu na mioyo ya subira iwe nasi sote toka kwa Rabuka wetu hata katika mwamba huu tusioweza kuupanda kama Zaburi 61:2 ituelekezavyo:  
“Toka mwisho wa nchi nitakulilia nikizimia moyo, uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda.”
Tunawapa pole wafiwa wote kwa msiba huu mkubwa.

Buriani Sosy, Buriani Komredi Kongola.


Dkt.  Musuto wa Mutaragara wa Chirangi
Mmoja wa Rafiki Wengi wa Kongola.

No comments: