Monday, September 20, 2010

Matumizi Holela ya Msimu 'Chakachua'




Utangulizi
 Chakachuliwa,  ni msamiati nyumbulifu (derivative word) toka neno mzizi chakachua  uliotumika katika mijadala Bungeni na sasa pia waandishi wa habari kueleza hali ya mafuta (dizeli & petroli) yaliyochanganywa na vimiminika vingine kama vile mafuta ya taa, maji n.k ili kuongeza ujazo kwa ajili ya kujipatia faida zaidi baada ya mauzo (kwa bei ile ile) ya bidhaa hiyo iliyoteremshwa thamani ulinganisha na uhalisia wake.
 Sina hakika kama neno hili linatambuliwa rasmi na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo kisheria ndilo lenye mamlaka ya kuratibu shughuli za uundaji wa istilahi za Kiswahili. Wala si yakini kama utafiti wa kina umefanywa na Taasisi yeyote yenye ithibati kama vile TUKI juu ufafanuzi wa dhana iliyobebwa katika istlahi hii kutoka lugha chanzi na hatimaye uundaji wa kisawe hicho cha chakachua.  Mpaka hapo itakapoelimishwa vinginevyo, neno hili nalichikulia kama kisawe kisicho rasmi katika lugha ya Kiswahili.


Eneo Stahiki Kiteminografia
Kwa kuzingatia mbinu ya kiteminografia (terminography), hili neno chakachua linastahili zaidi  kuonekana katika Kamusi ya Istilahi ya Sayansi-Fani ya Kemia hususani kwenye somo la taitresheni (titration) ambapo kuna uchambuzi wa matokeo ya uchanganyaji wa vimiminika tofauti sanjali na udhibiti wa ujazo wake.
 Maana & Kusudi
Kuchakachua  ni udanganyifu kwa kusudi la ama ki- biashara katika kutafuta faida kubwa kwa njia isiyo halali au kwenye upimaji (tests) ambapo matokeo fulani yanalazimishwa ama yaonekane au yasionekane kinyume na hali halisi. Mara nyingi kuna njia kuu tatu za udanganyifu katika vimiminika kama vile:-
 1.      Adulteration –  ughushi kwa kuongeza vimininika au kuchanganya na vitendanishi  (reagents) duni
2.      Dilution   - uchujuaji kwa kuongeza zaidi maji
3.      Substitution – kibadala, kwa kuongeza kimiminika mbadala.   

Matumizi ya neno
Pamoja na changamoto katika lugha yetu ya Kiswahili ya kuwa na upungufu wa istilahi anuwai katika uwanja wa Sayansi na Teknolojia, hivi  karibuni, neno kuchakachuliwa  limetumika kama msimu katika medani za siasa na kijamii kwa ujumla katika tamathali za semi na kwa mapana kama sinonimi (synonym) ambapo  istilahi moja ya Kiswahili inahusishwa na dhana zaidi ya moja katika lugha chanzi. Ndiposa neno hili limeweza kutumika kubeba dhana kadha wa kadha hadi kuleta mikanganyiko, kama vile kughushi, kubadilisha, kutotenda haki, kuharibika, kudanganya, kubatilishwa (mfano, leo nimesikia mtangazaji akisema kuwa “Ratiba ya ligi kuu imechakachuliwa”) n.k,  na hata –enye utata,  (mfano mtu anasema, “Alipata mchumba aliyechakachulika”akimaanisha mchumba mwenye utambulisho tata) n.k
 
Pendekezo
Ningekuwa na uwezo wa kushawishi BAKITA, ningependekeza kuwa kisawe rasmi kinacholandana na dhana nzima ya kupunguza uthamani wa kimiminika kwa kuchanganya na kitu kingine kiwe  kuchukuchua  badala ya kuchakachua. Kwamba neno mzizi liwe chukuchua ambalo linaweza kutoholewa kutoka chukuchuku mf. mchuzi chukuchuku  ambao ni mchuzi mwepesi usio na thamani inayoridhisha, mchuzi uliowekwa maji mengi (omusosi omujubhe) kupita kiwango kitakiwacho  hivyo mafuta yaliyochukuchuliwa ni mafuta yasiyo katika kiwango kitakiwacho ni mafuta yaliyoonhezwa kimiminika kingine na kushusha ubora wake.
  
Nathubutu kusema,


Musuto wa- Mutaragara wa- Chirangi




Verbal Diarrhoea Dehydrates Human Dignity. Chirangi, (2000)



(Shukrani kwa Blogu ya barclayp yenye picha)

1 comment:

LJSer said...

Hii imetulia.
naona kweli kazi ya mwl. wa Kiswahili Mwasamwaja bado unaikumbuka na kuiendi!