Mbele ya vipaza sauti, nje ya kituo cha kukarabati tabia cha Grerenville, Kusini mwa Richmond, sauti inasikika ikinena, “Kafa kwa amani zaidi kuliko wengi wa aliowauwa”. Hiyo ndio kauli ya Mshitaka mwakilishi wa mashahidi wa kutekelezwa kwa adhabu ya kifo (KWENYE KITI NCHA MAAUTI kwa sindano ya mauti) kwa Mdunguaji, John Allen Muhammad, aliyetuhumiwa kuua watu 10 na kusababisha hofu kuu iliyotanda jiji la Washington yapata wiki tatu, Oktoba 2002.
Historia inasema kuwa adhabu ya kifo imekuwapo kwa karne nyingi na imetolewa karibu kila kona ya dunia kwa wakosefu mbalimbali hususani waliohusika katika Uuwaji wa kukusudia, Uhaini, Usaliti (Majeshini), Ufisadi, Ukahaba na hata Ufanyaji wa biashara za madawa ya kulevya n.k kutegemeana na sheria au imani za nchi husika.
Kwa mujibu wa Amnesty International, Mwaka 2008, yapata watu 2,390 wamekufa kwa adhabu ya kifo katika nchi 25 na watu 8,864 wamehukumiwa adhabu ya kifo katika nchi 52. Tunahabarishwa kuwa Nchi zinazoongoza katika kutekeleza adhabu hii kwa mwaka 2008 ni China, Iran, Saudi Arabia, Pakistan and Marekani.
Angalau karne hii kumekuwepo na mabadiliko kiasi juu ya namna adhabu hiyo inavyotolewa katika sehemu nyingi kuliko ilivyokuwa. Hapo kale, Wanadamu waliotiwa hatiani wakahukumiwa adhabu ya kifo wame ondolewa pumzi ya uhai kwa namna mbalimbali, msisitizo ukiwa ni kufa kwa maumivu makali na au ya muda mrefu mbele ya kadamnasi ili iwe fundisho kwa wengine. Njia zilizotumika zilikuwa kama vile:-
kupigwa risari hadharani; kukoseshwa hewa kwa kufukizwa moshi au kuzamishwa majini; kuchunwa ngozi; kukatwa vipande vipande; kuchomwa moto; kuchemshwa ndani ya maji; kuchanwa vipande kwa kuvutwa na wanyama wanne;kupondwapondwa na kitu kizito sana au mnyama mzito kama Tembo; kukatwa kichwa kwa upanga; kukatwa kwa msumeno;kupigwa mawe; kusulubiwa mtini; kuachwa polini ukiwa umefungwa; kuchapwa mijeledi juu ya gurudumu la miiba; kunyongwa, kupitisha umeme mgeuko mwilini n.k.
Nadhani mabadiliko haya ya njia na hata nchi nyingine kupiga marufuku utolewaji wa adhabu hii ni zao la kukuwa kwa uelewa, mabadiliko ya kufikra, utandawazi na juhudi za Wanaharakati wa haki za Binadamu duniani kote ukiwemo Umoja wa Mataifa, Amnesty International n.k
Mjadala wa kukubali au kutokubali hukumu ya kifo ni wenye mvutano mkubwa sana duniani kwa kuwa unaibua hisia nyingi tofauti na pia kugusa imani na misimamo ya watu juu ya uhai wa Mwanadamu.
Haitoshi kusema tu kuwa malipo ya kuuwa ni kuuwawa au kwamba hakuna mwenye haki ya kuondoa uhai wa mwenziwe katika mazingira yeyote.
Hivyo kabla ya kufia uamuzi wa kuunga mkono upande fulani nashauri tutafakari bila mining’inio kwa umakini
wingi na uzito wa sababu za msingi za kuunga au kutounga mkono adhabu hii ya kifo.
Aidha natoa changamoto nikiuliza kuwa;
Je tunafahamu ni wafungwa wangapi wako kwenye orodha ya kusubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo nchini kwetu; je tunafahamu adhabu hiyo hutekelezwa wapi na kwa namna gani? Je ni vyema vyombo vya habari viwe vinafuatilia na kuruhusiwa kuhabarisha wananchi pindi mtu anapoadhibiwa au karibia kuadhibiwa hukumu ya kifo?