Monday, May 17, 2010

‘Huduma za Uuguzi zinazokidhi Viwango; Wauguzi Kuongoza katika Huduma juu ya Magonjwa Sugu)’







TAFAKURI YA KAULI MBIU KWA WAUGUZI NA 
WATUMISHI WENGINE WA AFYA MKOANI MARA

KATIKA SIKU YA WAUGUZI DUNIANI
(INTERNATIONAL NURSES DAY) 12 MEI, 2010

‘Huduma za Uuguzi zinazokidhi Viwango;
Wauguzi Kuongoza katika Huduma juu ya Magonjwa Sugu)’




IMEANDALIWA NA KUWASILISHWA NA :

Dr. Chirangi, Bwire, (MPH)





I. Utangulizi

Wageni waalikwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kiserikali na yasiyo ya kiserikali, Viongozi wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Wapendwa Mashujaa wa Taaluma nyeti – Wauguzi wa Tanzania,

Paukwa…., Pakawa!

Madaktari walipokuwa wamekamilisha kazi zao, wamechoka bin taabani na kupumzika, ule wakati ambapo ukimya na giza totoro vimetawala miongoni mwa wagonjwa majeruhi vitandani, yeye aliweza kuonekana akiwa peke yake na ki-taa chake mkononi akipita kuwazungukia wagonjwa na kuwahudumia ipaswavyo..







Florence Nightingale (12 May 1820 – 13 August 1910)



Habari ndiyo hiyo, iliyoleteleza mtaalamu na shujaa - Florence Nightingale, kutambulika aka mama mwenye taa (a lady with the lamp) katika kutoa huduma ndani ya hospitali ya kijeshi (Scutari hospital) huko Uturuki wakati wa vita (Crimean War) kama ilivyonukuliwa katika gazeti (Times newspaper) la Alhamis 08 Februari 1855.

Kutokana na ushujaa wake katika kufuata wito na vipawa vyake vilipomsukuma, kutokana na moyo wake wa huruma kwa wagonjwa, kutokana na uongozi wake wa mipango, kutokana na utendaji wake wa kimaadili na usafi wa kiwango cha juu, kutokana na umahiri wake katika kutunza takwimu, kuzitafsiri na kuziwasilisha kwa ajili ya kuboresha mfumo wa afya, kutokana na kuitetea na kuiboresha taaluma ya Uuguzi, Baraza la Kimataifa la Wauguzi (The International Council of Nurses kwa kifupi ICN) liliamua tuwe tunashereheka kwa kutambua mchango mkubwa wa Wauguzi wote katika Afya na Maendeleo ya jamii zetu kwa kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya shujaa wetu Florence kila tarehe 12 Mei.

Tunaipongeza ICN kwa kazi yake makini ambapo huandaa si tu kauli mbiu ( bali pia nyenzo za utekelezaji wa kauli mbiu kwa kila mwaka. Aidha nawashukuru pia Chama cha Wauguzi Tanzania kwa kazi kubwa ya uratibu kuhusiana na maendeleo ya Taaluma ya Uuguzi na pia kutukutanisha hapa leo kama iliyo kiada, wataalamu wanapowasha ile taa na kujikumbusha kiapo cha maadili ya taaluma ya Uuguzi na zaidi ya yote kutafakari mipango mkakati juu ya mada husika ya mwaka katika maboresho ya Afya ya Mtanzania.


II. Magonjwa Sugu Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya mwaka 2010
Mwaka huu Wauguzi wanapiga mbiu juu ya utoaji wa huduma za Uuguzi katika jamii zinazokidhi viwango na kuhakikisha kwamba Wauguzi wanashiriki kikamilifu katika huduma dhidi ya magonjwa sugu / sindika (delivering quality, serving communities:
Nurses leading chronic care)

Ndugu, Wauguzi wataalamu wenzangu katika huduma za afya, tukumbushane kuwa kwa mujibu wa takwimu za WHO (2005), magonjwa sugu kama vile Saratani, Pumu, Kiarusi, Shinikizo la Damu, Unyongofu (msongo wa mawazo), Kisukari n.k ndio yanasababisha asilimia 60% ya vifo vyote ulimwenguni.

Aidha kama tunafuata nyayo zake malaika wa huduma (the Ministering Angel)- Florence, katika kuwa makini na takwimu na kuzitumia katika kuboresha afya zetu, basi sote tutashirikiana kwa kuelimisha jamii kuwa ni hoja potofu isiyo ya kisayansi, kudhani kuwa magonjwa hayo sugu yanawakabiri zaidi watu wa nchi zenye kipato cha juu (matajiri). WHO (2005) inaonyesha takwimu za wazi kwamba 80% ya wagonjwa ni wale walio katika nchi za kipato cha chini na kati (Low & Middle income countries), hivyo Tanzania ni mojawapo!

Wengi wetu tumejifunza kwa namna moja au nyingine juu ya hayo magojwa kwa undani na tutaendelea kupata elimu juu ya matokeo ya tafiti mbalimbali kuhusu kinga, matibabu na au huduma kwa wagonjwa husika. Hapa niruhusuni nidodose tu kidog kwa nini udhibiti wa magonjwa sugu ni mada nyeti na jukumu la watu wa Mataifa yote pasi kujali utofauti wetu katika nasaba, jinsia, umri, kipato, imani wala itikadi za kisiasa .


Ni bayana Magonjwa sugu, yanatugharimu uhai wetu. bila kuchukuwa hatua, inakadiriwa kuwa jumla ya watu wapatao milioni 17 watakufa dunianii, mwaka huu kutokana na maradhi sugu.

Kwa vile magonjwa sugu ni ya muda mrefu na yenye uhitaji wa huduma za muda mrefu, maradhi haya yana madhara hasi makubwa `kwa nchi kiuchumi na kijamii. Maana yanafisha nguvu kazi katika uzalishaji na kuongeza matumizi makubwa serikali na familia husika katika kuyathibiti. Magonjwa haya yanasababisha watu kushindwa kufikia malengo yao maishani. Kuna gharama zisizo za moja kwa moja (indirect costs) kama upotezaji wa rasilimali muda makazini, mashuleni na hata majumbani n.k

Kuongezeka kwa magonjwa sugu duniani kunatokana na sababu kadha wa kadha zikiwemo ya mabadiliko ya kijamii, utandawazi, kuenea kwa maisha ya mijini (urbanization) pasipo utoshelezaji wa miundo mbinu na huduma kwa wote, kuongezeka kwa idadi ya wazee na hata ubinywaji wa haki na fursa sawa kwa wote katika mapato na huduma.



III. Utekelezaji wa Kauli Mbiu ya mwaka 2010

Kwa mujibu wa Maadili ya jumla ya Uuguzi kama yanavyoainishwa na ICN – Code of Ethics, Wauguzi wana wajibu wa msingi wa kushiriki katika kuimarisha afya na kuzuia maradhi. Aidha tunakubali kushirikiana na jamii kwa ujumla kuanzisha na kuunga mkono shughuli zinazostawisha afya na mahitaji ya kijamii ya umma.

Ndugu zangu haitoshi kutambua na kulalama juu ya changamoto mbalimbali zinazotukabili leo katika taaluma ya Uuguzi nchini. Ni vyema kwa kutumia elimu, ujuzi na umoja wetu ndani ya Chama cha Wauguzi Tanzania, Vikao vya Wauguzi na Uongozi katika Vituo vya Afya husika, Bodi za Afya za Wilaya na Mikoa na hata kupitia Kitengo cha Huduma za Uuguzi katika Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, tuwasilishe matatizo yetu na mapendekezo yanayotukabili kwa hoja zenye takwimu rejea zilizotafsirika kisayansi kama Muasisi wetu, Meneja, Mtakwimu, Mkufunzi, Mshauri na Muuguzi mwana maboresho Florence alivyofanya katika kuipa Taaluma hadhi yake, kuwajengea uwezo Wauguzi na kuleta mapinduzi chanya ya mfumo katika huduma za Afya.

Shime, tushirikiane na wadau wote wa afya katika maeneo yetu kutekeleza Mpango Mkakati wa tatu katika sekta ya afya (the third Health Sector Strategic Plan) 2009 – 2015 ambao uko sanjari na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millennium Development Goals) kufikia 2015 .
Tushirikiane kuelimisha umma juu ya vidokezo hatarishi vya magonjwa sugu na pia sisi wenyewe kama watumishi wa idara ya afya tuwe mfano (model) wa kuigwa katika familia zetu, makazini kwetu na katika jamii zetu kwa ujumla katika namna tunavyoishi kuboresha afya zetu; mfano:
 Kuepuka uvutaji wa sigara / tumbaku
 Kuepuka unywaji wa pombe uliokithiri
 Kupata lishe bora kwa wakati muafaka
 Kufanya mazoezi
 Kuepuka ngono sisizo salama
 Kudhibiti muendelezo wa msongo wa mawazo nk

Katika kutoa huduma husika kwa wakati muafaka kwa wagonjwa, wa magonjwa sugu, tunashauriwa kutumia CCM ( the Chronic Care Model)  ambapo tunaunda mfumo:-
wenye mgojwa aliyehamasika na mwenye taarifa kamili, anayejiamini na kuweza kufanya maamuzi juu ya afya yake nauwepo wa timu ya Wataalamu ambao pia wana taarifa kamili juuu ya ugonjwa, maamuzi na mahitaji kwa ajili ya kutoa huduma kwa kiwango cha juu kwa kushirikiana na taasisi za afya.

Na pia kufuata ushauri wa WHO- ICC Framework, 2002 ( WHO-Innovative Care for Chronic Conditions , mkakati ambao pia unasisitiza kufanya maamuzi kwa rejea za takwimu, kulenga jamii husika, kuzuia ugonjwa, huduma bora iliyoratibiwa vyema,uwezo wa kuiga na kutumia kinachofaa kufuatana na mazingira husika na kuwa na ushirikiano miongoni mwa Wataalamuna na kuungwa mkono na jamii katika huduma zitolewazo.


III. Hitimisho

Ndugu Wauguzi na wageni wote waalikwa tofauti na siku kubukizi nyingi tulizonazo nchini, katika siku ya Wauguzi duniani hatukutani kwa sababu tu ya kusherehekea bali tunakutana kutafakari juu ya uratibu na utekelezaji wa mpango mkakati katika kutimiza kauli mbiu yetu ya mwaka husika.

Kwa moyo wa upendo, ninasajiri shukrani zangu za dhati kwa mchango mkubwa wa kipekee unaotolewa na Wauguzi popote walipo ulimwenguni hata ambapo Madaktari na Wataalamu wengine wanakuwa wamechoka bin taaban na giza totoro likitanda ama katika kumpunguzia mwanadamu maumivu au kurejesha na kuboresha siha yake au kumkarabati au kumtunza au kumwelimisha na kumshauri juu ya hamasa na utetezi wa maisha ya afya njema, kinga na au tiba ya maradhi.

Tutakiane kila la kheri tunapowasha taa zetu katika kuhamasisha mabadiliko chanya ya mifumo yetu na jamii kwa ujumla kuelekea huduma bora kwa wote na maisha yenye siha bora dhidi ya maradhi sugu yanayotukabili.



1 comment:

Anonymous said...

hii imetulia Dr!