Tuesday, July 20, 2010

Wahubiri katika sauti zenye Mpangilio

Kwanza Bofya kwenye play button ya Redio hapa chini usikilize.
Miziki ya kumsifu na kumtangaza Mungu imekuwepo tangu enzi za agano la kale na inaendelea kukua kwa kasi katika mapigo,ghani na staili kadha wa kadha za uchezaji wa Waimbaji.

Umuhimu wa nafasi ya muziki katika Makanisa, Misikiti na Masinagogi ni mkubwa sana katika kusaidiana na Wahubiri wengine kufikisha ujumbe kwa hadhira inayokusudiwa.

Aidha Kwaya ziimbazo au zipigazo miziki ya Kiroho pia kama  walivyo mawakala wengine wa mabadiliko ya mwanadamu, zimefanya kazi kubwa ya kuwabadili, kuwafariji, kuwahubiri, kuwashawishi,  kuwafundisha, kuwaonya na hata kuwapagaisha wanadamu wengi, mimi nikiwa mmoja wao!

Ukiachilia wasanii au kwaya ambazo zimeshapiga hatua kubwa, Wahubiri hawa wa sauti zenye mpangilio wanakabiliwa na changamoto nyingi, hapa chini leo nataja mbili tu:- 

1. Kuhakikisha kuwa ujumbe wao unahaririwa na kupangwa vyema kabla haujawafikia hadhira. (si kujali tu mipangilio ya midundo na staili za kuruka)

2. Kurekodi kazi zao na kuwa na hati miliki. Wengi wametunga nyimbo na baada ya muda zimeachwa na kupotea tu bila kutunzwa, hapa namkumbuka Mwalimu wangu Julius Zabuloni Machumu (RIP), ambaye hadi mauti yake hakuwahi kurekodi kazi yake ya usanii iliyokuwa na ubunifu wa hali ya juu enzi hizo za miaka ya 80. Kati ya vibao vyake vilivyotikisa katika makambi ya kiroho ni  Katondo tondo Maryamu Nemuka, Isaka, Kinachoshangaza, Jerusalem, Paliondokea Yohana Mbatizaji n.k 

Wito:
Wadau wote tujifunge vibwebwe kuwasaidia Wahubiri hawa kwa kadiri ya uwezo wetu na vipawa vyetu  maana utume wao na jumbe zao ni za muhimu sana katika maisha yetu leo na kwa vizazi vijavyo.


Hapa chini ni picha ya Mwalimu mzoefu wa Kwaya ya Upendo ya Kanisa la Mennonite Tanzania Mugumu,  ndg. Gemma Igira (mwenye shati nyeupe) akiwa na Mwalimu mwenzake gwiji katika muziki wa injili ndani ya Studio yenye wapishi wa muziki waliobobea ijulikanayo kama Studio Habari Maalum  Mwanza wakati waliporekodi Album ya Upendo Choir kwa jina la Tenda Miujiza. Heshima kuu kwa Waalimu wote waliotoa msaada mkubwa, Wanakwaya wote walioshiriki kutoka Jimboni kwao chini ya uongozi wa jimbo wa Mchungaji  Wilson Shanyangi Machota.  .

Ukipenda kujipatia nakala yako ya Album hiyo ambapo kibao hicho hapo juu (SIFUNI) kimo ndani wasiliana moja kwa moja na Uongozi wa Kwaya ya Upendo au Uongozi wa Jimbo (KMT- Mugumu c/o S.L.P 17 Mugumu, Serengeti, Tanzania au tuma barua pepe kwa gemma.igira@hotmail.com.
2 comments:

Magiri said...

Kweli kuna aja ya kutangaza kazi ya bwana na kutuza kumbukumbu za kazi zetu

Anonymous said...

Du kazi njema sana hii.
wa- chirangi tunashukuru kwa kutujuza kuhusu hili, ubarikiwe sana.