Namuaminia[1] mnyama wa kisiasa mmoja, mzee wa busara aliyewaacha Wanasiasa, Wanahistoria na Wahabarishaji midomo wazi.
Nawatunuku pia Wapigania-Haki wengine kama vile Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyiga, Martin Luther King, Julius Kambarage Nyerere, MamaTereza wa Calcutta, Mohandas Karamchand Gandhi, Bibi Aung San Suu Kyi wa Myanmar na wengine wote walio mifano kwetu.
Alizaliwa katika kijiji cha Qunu karibu na Umtata, Transkei. Rolihlahla akakua akiwasikiliza Wazee na akafundwa chini ya utamaduni asilia katika ufukwe wa mto Bashee zamani za Utawala wa Kiimla na Ubaguzi wa Rangi.
Katika harakati za Umkhonto we Sizwe na mchango wake dhidi ya utawala wa Makaburu, akachukiwa, akasingiziwa makosa ya kiuhaini, akashitakiwa na kufungwa kifungo cha maisha katika gereza la wafungwa sugu na lenye ulinzi wa hali ya juu kuliko yote.
Msimamo wake haukuyumbishwa na mpango wa kupewa takrima yenye ndoano, eti awekwe huru kinamna huku watu wake wanaendelea kutaabika.
Siku ya uhuru ikawadia, baada ya muda wa yapata miongo mitatu, akaachiwa huru akatoka katika harufu mbaya, mateso na upweke. Wananchi wakarejea katika demokrasia na haki; uchaguzi ukaitishwa.
Ndipo aliyekuwa mfungwa wa kisiasa alipoibuka mshindi kwa kura nyingi. Akaingia Ikulu akaketi katika kiti chaUraisi.
Akaongoza nchi, lakini kinyume na matarajio ya wengine, pia akawasamehe na kuwashirikisha Wabaya wake.
Pamoja na mamlaka aliyopata na kutunukiwa Mali, Ukazi wa Kimataifa, Shahada, Medali na Tuzo nyingi mbalimbali ikiwemo ya Amani ya Nobeli na hata jina lake kutambulisha barabara, tuzo na majumba katika Mabara yote Duniani bado aliendelea kuwa mtu wa watu, muungwana asiye na kiburi wala dharau.
Ninapenda kusimama katika Usawa, Haki, Demokrasia na Umoja uletao Ufanisi. Kwa vile Jitihadi haiondoi kudura, namwomba Mungu anisaidie niige mfano huu wa muasisi Nelson Mandela katika hali yangu nichaguapo viongozi, nigombeapo uongozi au nikabidhiwapo dhamana ya kuongoza.
Pasi kilinge nachukia hasilani maisha ya Ufalisayo yaliyokubuhu uzandiki na uburuzaji wa wanyonge.
Nakereketwa kutafuta, kujenga na au kurejesha amani popote nitakapokuwa.
Nina heshimu uongozi shirikishi wenye ushawishi mwanana unaojali utu wa mwana- adamu uliopitishwa katika tanuru la michakato ya kisayansi, maadili ya kitaaluma na utamaduni uliokubalika kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya mwanadamu.
Ada ya mja hunena muungwana ni kitendo Mungu nisaidie nitende sasa na hata milele.
Nyamuwanga nunsakile kajanende na kajanende!
[1] Tofauti na neno Namuamini, hapa ni kuwa na uhakika wa utendaji wa mtu na sio kumtukuza kama MUNGU
2 comments:
nimekukubali maana ukiri huu unagusa kweli na haki tuitafutayo.
Moses
MZEE,
Nami nakuaminia kwa kushusa vitu vya nguvu.
Kadogo
Post a Comment