Friday, August 31, 2012

BURIANI MAMA BERTHA KIFUTU


Kwa huzuni, tunapotafakari kututoka kwa ghafla kwa mpendwa Mama yetu Bertha Kifutu, tunaendelea kukumbushwa kuwa kifo si kutoweka kwa mwanga wake, bali kuzimwa kwa taa yake wakati wa mapambazuko baada ya kukamilisha safari ya maisha yake hapa duniani.


Ingawa Mwandishi, Hans Christian Andersen, alitukumbusha kuwa, maisha ya Mwanadamu ni hadithi  isimuliwayo kwa ukamilifu na Mola, turuhusuni nasi tusimulie japo kwa kudodosa rejea ya maisha ya huyu Mama yetu japo kwa aya moja, kama Mithali ya Mfalme Solomoni Mwana wa Daudi inavyosimulia;
Kwamba, Mwanamke mwema, kwa mikono yake, hufanya kazi zake kwa nguvu na Wanawe humwita Mbarikiwa, pia huamka kungali giza (asubuhi na mapema), kuangalia mambo ya nyumbani kwake, wala hali chakula cha uvivu; hivi ndivyo ilivyokuwa pia kwa huyu Mama yetu, Sengi Nyamambala wa Makanya hadi mauti ilipomkuta asubuhi na mapema (katondo- tondo muruguru) akiwa mfano wa Mama aangaliae mambo ya nyumbani kwake na kutunza familia!

Hakika, ingawa kifo kinatuondolea wapendwa wetu, kamwe hakiwezi  kutuondolea fikra na matendo yao ya kishujaa. Aidha, kwa vile huacha katika kumbukumbu zetu, alama za upendo zisizofutika kwa jinsi walivyoshirikiana nasi, basi tumuombe ndg. Sira, Kiongozi wa iliyokuwa kwaya yake (Imani - Choir), Kanisa na Jamii kwa ujumla, tuendeleze hamasa na jitihada za mpendwa wetu katika kuishi maisha ya kumtukuza Mungu wetu kwa furaha.

Swali kuu la kujiuliza; je, sisi tumempa Mungu kipi cha ziada kuturuhusu kuingia katika kumbukumbu za Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi leo tarehe 26/08/2012, ilhali makucha ya mauti hayakutoa nafasi hata ya siku mbili tu wala kwa familia ya mpendwa wetu kuweza hata kusikiliza tamko lake au kuagana naye?


Katika huzuni twaomboleza, katika huruma twawafariji wafiwa, katika tafakuri twajihoji juu ya maisha na uhai wetu- swali lisilojibiwa hata na Wana-Baijirontolojia (Biogerontoligists) wazamivu wanaotafiti namna ya kurefusha miaka ya kuishi uzeeni!

  
Pamoja nanyi katika maombolezo,Judy, Marja & Musuto wa Mutaragara wa Chirangi

No comments: