Monday, January 14, 2008

BETHSAIDA CENTRE FOR HEALTH AND DEVELOPMENT





UZIO WA 'THE HOUSE OF BETHSAIDA ' MAHALA AMBAPO PANATARAJIWA KUWA KITUO CHA AFYA KWA AJILI YA WANANCHI KATIKA MANISPAA YA MUSOMA SIKU ZA USONI.
HII NI HATUA MOJAWAPO YA KUMUENZI BABA MUTARAGARA CHIRANGI KWA KAZI YAKE YA HUDUMA KWA WANANCHI.
MAANDALIZI YATAKIWAYO YANAENDELEA KWA MUJIBU WA TARATIBU ZINAZOPASWA.
Imetolewa kwa hisani ya mpiga hizi picha P.Mamuya.

Thursday, January 3, 2008

KUMBUKUMBU ZA MWAKA MMOJA JUU YA MAISHA YA MZEE CHIRANGI




KIUMBE HADIMU AMBAYE JAPO AMEKUFA SAUTI YAKE NA MATENDO YAKE YANAENDELEA KUTOA CHANGAMOTO CHANYA KATIKA MAISHA YETU WANAMARA NA TAIFA ZIMA KWA UJUMLA.

Hakutoka katika familia maarufu wala hakuwa na mali nyingi na elimu yake ilikuwa tu ya wastani. Hata hivyo ukithubutu kunyambulisha mitizamo, misimamo na matendo yake waweza kubaini kuwa upatikanaji wa viumbe wenye matendo sanjari na kauli mbiu ya ‘HAKI HUINUA TAIFA’ ni adimu katika ulimwengu wa leo.

Siku kama ya leo, mwaka mmoja uliopita makucha ya kifo pasipo huruma wala taarifa yalituondolea pumzi ya uhai Mzee wetu


Amos Mutaragara Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wa Rihu- Omumbogo wa Kumusoma gwa Nyambita..

Marehemu mzee Chirangi aliyezaliwa mwaka 1932 huko Bushora Mwirengo Mugango, Mkoani Mara aliacha alama za kishujaa kama Kiongozi, Mzalendo na Muumini wa kuigwa katika kizazi hiki na vijavyo.

Familia ya Chirangi inawashukuru sana wananchi wote wa Mkoa wa Mara na kwingineko, Serikali yetu, Jumuiya zote za Kidini, CCM na Vyama vyote vya siasa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi na Asasi mbalimbali za kijamii kwa Faraja, Misaada mbalimbali, Umoja na Mshikamano wao waliotuonyesha wakati wa msiba hadi huduma za mazishi za marehemu baba yetu Mutaragara Chirangi. Ni bayana kuwa hakuna chombo chochote cha habari wala mtunzi wala hifadhi ya makumbusho inayoweza kwa ukamilifu kutuhabarisha juu ya wasifu wa marehemu mzee Chirangi. Hata hivyo kweli isiyofichika huchomoza popote ikitukumbusha machache tu ya utu na utumishi wake kwa wanadamu. Kila mwaka familia yake itakuwa inaainisha dhamira moja kuu ambayo inaakisi moja ya sifa zake kama changamoto kwetu. Mwaka huu tunaanza na sifa yake ya UWEKAJI MIPANGO (Planning):-

Kila kitu chake alitaka kiwe kimeandaliwa barabara kwa wakati muafaka na kwa kiwango kinachoridhisha hivyo akaitwa ‘mzee wa Standard’. Ni mzee aliyepinga kwa vitendo uongozi na maisha ya uzima moto, ndiposa tulishuhudia hata akiwa amejiandalia Wosia kwa familia na kaburi lake mwenyewe sio kwa udhoofu wa afya yake bali kwa msingi wa kujiandaa na kutotaka kusababisha usumbufu wowote kwa jamii wakati anajua kuwa kauli ya Mungu pale Edeni kuwa ‘hakika mtakufa’ ni ya kweli na kwamba ilimuhusu pia hata na yeye.
Ni mzee aliyekuwa rafiki wa karibu wa nyenzo KALENDA si kwa sababu ya kujua jinsi siku zinavyokwenda bali zaidi kujipanga katika siku zinavyokuja.
Tunapoanza mwaka mpya 2008 sauti ya mzee Chirangi inatuasa sote kuwa tuwe watu wa mipango na utekelezaji. Tuweke mipango yetu ya muda mfupi na mrefu popote tulipo iwe ni katika familia, au katika Chama au Taasisi au Kampuni au Usharika, au Jumuiya yeyote kwa ajili ya maendeleo yetu. Maana ni kweli kuwa usipojua unapoelekea kamwe huwezi kupotea maana popote utakapokuwa utafikiri kuwa umefika.

“ Busara zako, utu wako na hekima zako ni hazina kubwa sana sio kwa familia yako tu bali kwetu sisi sote” Mgeni namba. 228 wa Mzee Chirangi. Mh. H. N. Ole – Mkuu wa Wilaya Musoma, Aug. 2001.

KWA HESHIMA NA SHUKRANI, FAMILIA YA CHIRANGI INAWASILISHA.




Prof. Dr. Sospeter Muhongo
Mdogowe Mzee Mutaragara

SHUHUDA, MAONI NA USHAURI WA WAGENI WA A.M.CHIRANGI



Kutoka Kushoto (Mwenye kitambaa Cheupe) Mjane wa Mzee Mutaragara, mama Bertha Nyabwire na mjukuu wake Judith na kulia ni Bibi (Marehemu) Nyarukonge Mjane wa Babu Faru wa Muhongo watu waliomlea mzee Mutaragara.
------------------------------

Yafuatayo ni mawazo ya sehemu ndogo tu ya wageni wenye demografia mbalimbali waliokuwa wakimtembelea mzee Chirangi maana alipenda sana kukaribisha wageni. Kama ilivyo kiada, Mzee Chirangi aliwapa namba na kisha kitabu kwa ajili ya kuandika maoni au mawazo yao ambayo aliyatunza.

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba.116.
ASkofu S. B. M. Muttani
Kamunyonge Area, S.L.P. 336, Musoma
11/07/1996.

MAELEZO:
Ndugu A.M. Chirangi,
Mwenyekiti wa CCM,
Musoma – Mjini.

KAZI YA USHUJAA KWANGWA PLOTS.

Ndugu Mwenyekiti, Suala hili juu, siyo lelemama.

Kutokana na kauli yako yenye moyo safi, kunizungumza mara nyingi; ili nitembelee eneo la Kwangwa.

Kwa hiyo, asubuhi ya tarehe 11/7/1996, nilipanda Baiskeli yangu mpaka kwenye eneo lenyewe, ambalo limeanzia katika bonde la Kigera hadi uwanda wa Kwangwa.

Wahenga walinena muungwana ni kitendo, kuhusu usemi huu. Wewe mwenyewe umetekeleza kwa kitendo halisi; ambacho kinaonekana kwa Mungu na kwa watu sawia.

Kwanza, hulipata dhana nadharia, kuwe na sehemu ya makazi ya watu.

Pili, ukaangaika kutoa ushauri kwa wakaaji wa Kwangwa wakubali kuacha viwanja vyao, viwe makazi ya Umma.

Tatu, ukasimamia wewe mwenyewe kwa hali na mali kwa muda wote, wa kufyeka machaka na kuziba korongo na upashaji wa miamba na mawe n.k.

Nne, kusimamia uchoraji na upimaji wa viwanja na barabara, kwa utaalamu sahihi.

Tano, kuelekeza kwa kuzingatia hulka za jamii yaani kutenga maeneo ya utamaduni wa jamii.

Hivyo ukaweka viwanja vya burudani k.v. Makanisa, Misikiti, Shule, Chekechea na Soko n.k.

Sita, ilibidi upige mbiu kwa wananchi, ili wajipatie viwanja vya kujenga nyumba zilizo na hakika, sasa na baadaye bila migogoro.

Saba, kwa uthabiti wa fadhila yako ya moyo wa ushujaa, umekuwa mstari wa mbele kufyeka vichaka na kung’oa mawe. Hatimaye kujenga makao ya hakika, “Hongera sana”.

Umeweka alama kwa Ramani katika historia ya vizazi vifuatavyo.

Baada ya kisa, mkasa, usemi huu umenihulkisha kuwa na mkasa, kuomba usaidie kupata viwanja viwili ambavyo vitakuwa karibu na mto Kigera Magharibi.

Tamati, ujira wa nguvu zako hutalipwa hapa duniani na baadaye huko peponi.

Kwa hiyo, tukimwinulia Bwana macho ya mioyo yetu. Yeye amejaa fadhili nyingi.

Maana ndiye amlipaye kila mtu sawasawa na haki yale (Zab. 62:12).

“Yeye azidi sisi tupungue”
**************************************






Mzee Mutaragara na familia yake pamoja na wakweze

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 166.
Vivian Juma- Mwenyekiti wa Mkoa (CHADEMA) na
Mmratibu Kitengo cha Wanawake Taifa (CHADEMA)
BOX 1482, Musoma.
07/01/1999

MAELEZO:
Natoa shukrani kwa wema wako Mheshimiwa Mutaragara Chirangi na ni histori kubwa kwani sijawahi kukaribishwa hasa na heshima ambayo nimepewa ikibainika kwamba mimi ni kiongozi wa upinzani. Hivyo ni heshima ambayo sitaweza kuisahau siku hii ya leo.

Mungu abariki nyumba hii.

****************************************

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba . 228.
Mh. H. Hepillal N. Ole – Molloimet – Mkuu wa Wilaya Musoma
P.O. BOX 20, Musoma
Aug. 2001

MAELEZO:

Mimi na ujumbe wangu kutoka Wilayani nimefurahishwa sana na makaribisho yako nyumbani kwako - hatimaye katika makazi yako ya baadaye, mapya Kwangwa ambako tumeweza kuona jitihada zako za hali ya juu, mipango ya sasa na baadaye, utundu na utashi wako katika kubuni mambo ya sasa na baadaye, mipangilio ya uwekaji kumbukumbu zako za maisha, mali, vifaa, taarifa mbalimbali za uongozi wako, jambo ambalo hata baadhi ya watu hawafanyi. Busara zako, utu wako na hekima zako ni hazina kubwa sana sio kwa familia yako tu bali kwetu sisi
sote. Umetufundisha umetuonyesha na kutuelekeza tulivyo na ulivyo wewe ni mtu wa kuigwa na wale wasio na choyo! Wewe ni kero kwa wale wasiopenda haki, uwazi na ukweli na haki. Wewe ni mtu wa watu wakati wa uongozi wako na hata sasa ndani ya jamii wewe ni mfano wa kuigwa na wale wasio na choyo.
Mimi ni mmoja akutakiaye mema na familia yako na kukutakia maisha marefu pesa na wakati ujao. Endelea na moyo huo usikate tamaa kwani kufanya hivyo ni dhambi – dawa ni kujua. Kwako, wewe, wanao, wajukuu, vilembwe na vilembwekezo – muwe na rutuba ndani ya jamii.
************************************************










Mzee Mutaragara aki'pozi' kwa ajili ya picha na familia yake.
UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 265.
Dr. Mwitondi Kassim Saidi (Ph.D)
School of Mathematics
Universty of Leeds
United Kingdom
07/02/2004

MAELEZO:

FACE TO FACE WITH MUTARAGARA CHIRANGI.

I knew Mzee Chirangi as a dedicated school teachers, social worker and active sports activist. The past was particularly interesting as it went down well with my personal interest namely watching and playing football, little did I know then that almost 30 years later I would be brought to face with Mzee Chirangi in a surprise encounter that would unfold a lot of facts about him, his human, moral and social properties as I had never anticipated. This is how I got to talk to Mzee Chirangi. I had just returned to Musoma from the United Kingdom, for the funeral of my father – Mzee Said Mwitondi who passed away on the 4th of February 2004, barely a week after I had parted with him to return to the UK.
Living within the area, Mzee Chirangi had decided to pop in and pass his condolences. This by itself is a wonderful moral property as Mzee Chirangi never knew our family but felt a moral obligation to pay us a visit at that difficult moment but like a shimming star in the sky everyone in our family knew him – not least myself, as I had earlier tried to get some sporting information through him. I had contacted Professor Sospeter Muhongo, my former teacher, friend and adored football player, who in turn introduced me (by email) to Musuto Chirangi the son of Mzee Chirangi. For some reasons, the sought information could not be obtained for over 3 years. Believe me what I could not get in 3 years, I got with a couple of hours meeting Mzee Chirangi. The required information was on football activities in Musoma in particular, photographs of the guardians and players of the 70 who characterised Musoma footballing boom in my teenage. I needed then for a Musoma website, the link to which is available from my official website below. So when Mzee Chirangi visited us my immediate request to him was about this long-overdue plan and he immediately invited me (with two other friends) to visit him at his Kamunyonge residence. In the light of that invitation – I started laying down the strategies of comparing my theoretical knowledge of Mzee Chirangi with the ‘empirical readily’.
We arrived at Mzee Chirangi’s residence about 7.15 pm on 7th February, 2004.
Less than 30 minutes later I was up dating my knowledge of Mzee Chirangi with a new property of a “LIVING ARCHIVE”. He took us through massive archive files ranging from education, sports, social services and spirituality manual databases so informative that one of my friends suggested that Mzee Chirangi liaise with the relevant ministries to put the data to even better use. Another newly acquired piece of information was that Mzee Chirangi was a “Politician with a different attitude”. In Tanzanian political terms a typical politician is associated with some level of corruption (you are welcome to your own views if you disagree). Listening to the way Mzee Chirangi spoke, browsing through his writings, speeches and vision, left no doubt that he was what most “typical politicians aren’t”. Look at the following contesting cases. One works on individual’s voluntary service in a local neighborhood (and charges nothing) while another individual does the same and quotes an ample of million shillings. The former is Mzee Chirangi, working at Kwangwa, Kigera and Kiara and the letter is an “Unknown” individual channeling quotations through the Town Council.
Family is also an important entity in Mr. Chirangi’s life (you may argue that it is in every one’s life). Daily routine is clearly laid down as are basic principles that guide human life. My recommendation is for Mzee Chirangi to put his work in a more formalized style books/ CD ROM and be officially archived for the benefit of generations. I will be happy to assist into that direction.
*****************************
Mzee Mutaragara kama ilivyokuwa kawaida yake alikuwa akiendaButiama kwa rafiki yake baba wa Taifa J.K.Nyerere mara kwa mara. Hapo ameambatana na Mdogo wake Prof. Muhongo, Mkewe na wanawe.

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 277.
Rashon M. Matete, Mwenyekiti wa Wazazi – Musoma Mjini.

MAELEZO:
Maelezo yangu kimuhtasri yahusuyo Mzee A. M. Chirangi ni kama ifuatavyo:-
Alipokuwa mwalimu wakati wa shule za serikali na madhehebu alidhihirisha uwezo wake wa kufundisha hasa alipokuwa anafundisha darasa la nne wakati huo. Shule zote za Primary I – IV alizopata kufundisha katika dhehebu la TMC zilikuwa mfano mzuri katika Jimbo la Ziwa Wilaya ya Musoma.

Mzee A. M. Chirangi alikuwa mwalimu darasani, wanafunzi wake wa darasa la nne walifaulu kwa wingi kuingia katika shule za kati (Middle School)
Kwa kujiweka katika uhodari huo hatimaye aliteuliwa na dhehebu hilo la TMC kuwa Katibu wa Elimu wa TMC. (Education Secretary) na Primary Schools I - IV.

Hii ni picha kamili inayodhihirisha kwamba juhudi zake za kutoa huduma kwa wanadamu hazikuanza jana. Ni tangu ujana hadi uzee.

Juhudi mbalimbali za kuwasaidia wananchi wa Musoma na Mkoa wa Mara kwa ujumla zilizidi kujitokeza kwa kiwango kikubwa alipochaguliwa na wana C.C.M. kuwa Mwenyekiti wa C.C.M. Wilaya ya Musoma Mjini na pale alipokuwa Mwenyekiti wa Jumiya ya Wafanyakazi.

Kwa hiyo mimi binafsi ninaelewa kuwa Mzee A. M. Chirangi ana haya ya kuiga na yanayompa sifa nzuri:-
- Mchapa kazi tangu ujana wake mpaka sasa.
- Ana uzoefu katika uongozi na uendeshaji.
- Anafaa sana katika ushauri nasaha unaohitajika kwa watu walio wengi.
- Ni mfano pekee wa dhati kwa nchi yake na watanzania wenzake.
- Amejitahidi kujiweka katika mazingira ya kusaidia jamii na taasisi mbalimbali kuelewa mbinu za kupambana na mazingira yao.
- Ni mtu ambaye yuko miongoni mwa watu ambao waliombea Taifa hili Amani.
- Ni mtu ambaye anataja kosa waziwazi bila woga.
- Ni mpenda haki na msema kweli pindi suala kati ya mtu na mtu ua miongoni mwa watu linapojitokeza.
- Ni mtu anayetunza akadi na muda kwa jambo hili yeye ni pekee katika mji huu wa Musoma.
- Ni mbunifu wa kuigwa anapopewa madaraka.
Kwa hahika siwezi kutaja mambo yote yanayomhusu Mzee huyu bali ninachomalizia kusema ni kwamba ni vema kuiga mazuri ambayo Mzee A. M. Chirangi amefanya katika maisha yake ili iwe faida kwa vizazi vijavyo.

Mungu wetu wa mbinguni ampe baraka na maisha marefu kwa madhumuni ya kukamilisha mradi wake wa ujenzi wa mji mpya huko Kiara.
**********************************************










Mzee Mutaragara akiwa nyumbani kwao Kawawa st. Musoma wakati wa chakula cha pamoja na mazungumzo pamoja na Mkewe, Shangazi yake, Mdogo wake (na mkewe) na Dada zake.

UTAMBULISHO WA MGENI:

Namba. 305.

EMMANUEL MULESI
RADIO VICTORIA FM.
29/01/2006.

MAELEZO:
Nilifika nyumbani kwa Mzee Mutaragara Chirangi, kwenye majira ya saa 10 jioni, Tarehe 29/01/2006 eneo la Kwangwa.

Katika safari hii nikiwa njiani nilijionea mambo mengi ambayo pia nilijifunza vitu vingi sana kutoka kwa Mzee huyu.

Mambo makubwa niliyoyaona ni pamoja na jitihada kubwa ya Mzee huyu kujituma na kujitolea katika kuleta maendeleo hasa katika kuleta maendeleo katika maeneo ya Kigera na Kwangwa, hasa katika sekta za barabara na maji.

Nilijionea zaidi ya barabara 20 ambazo amejitolea kuzijenga kwa nguvu zake mwenyewe, pamoja na kuweka bomba kubwa la maji kwa maeneo hayo.

Mambo hayo yalinishtua kidogo kabla ya hata kufika nyumbani kwake Kwangwa.

Tulipofika nyumbani hapo nilizidi kustaajabu kujionea nyumba ya Mzee Mutaragara ambayo alianza kuijenga mwaka 1994, kwa kweli ujenzi wa nyumba hiyo ilinionyesha ni kwa jinsi gani Mzee huyu alivyo mkarimu, kutokana na ujenzi wa nyumba yake kuzingatia sehemu mbalimbali ambazo ameziandaa kwa ajili ya wageni wanaokuja kumtembelea kupumzika.

Pia ujenzi wa nyumba hiyo unaonyesha ni kwa jinsi gani amejiandaa kwa maisha yake bila kuwa na shida ya maji katika nyumba hiyo na pia utunzaji wa mazingira.

Nilipoingia ndani ya nyumba hii ya Mzee Mutaragara ndipo nilipothibitisha kuwa Mzee huyu ni mtu ambaye anatunza kumbukumbu zake kwa kila kitu anachokifanya katika maisha yake ya kila siku, na anaonekana ni mtu anayejali muda kwa kujiwekea ratiba yake ya kila siku, na anaonekana ni mtu anayejali muda kwa kujiwekea ratiba yake ya kila siku tangu kuamka mpaka wakati wa kulala.

Mbali ya hayo niliyoyaona na kujifunza kuwa Mzee Mutaragara ni mtu mwenye KIPAWA cha uongozi na ni mtu mwenye MAONO na uongozi kutokana na kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa miaka mingi iliyopita.

Nimejifunza kuwa siri kubwa ya uongozi wa Mzee Mutaragara Chirangi ni
HEKIMA na BUSARA, katika kuwaongoza watu mbalimbali.

Nilipomuuliza siri ya yeye kuongoza kwa muda mrefu ni ipi? Alinijibu kuwa mara nyingi yeye amekuwa akifanya kazi bila ya kujali mkubwa, mdogo, jinsia, rangi, maskini au tajiri na pia yeye mara nyingi huwa na maono ya kuangalia mbele na kuona kuna nini? Ambacho kinaweza kujitokeza na kukitatua kabla hakijatokea na kuleta matatizo.

Pia katika ziara hii nimeona kuwa Mzee Mutaragara ni mtu mwenye uwezo wa kuelewa na ni kiongozi shujaa katika kufanikisha mambo yake ya ongozi, mtunza nyaraka mzuri na ni mwandishi.

Aidha Mzee huyo ni mkarimu, mwenye kipaji cha uongozi mtunza muda mzuri mtu wa kujituma katika kuhakikisha kama anashughulikia jambo fulani anahakikisha linafanikiwa na ni kiongozi asiyependa rushwa hata kidogo.

Lakini katika hayo niliyoyaona kwake pia nimegundua kuwa Mzee huyo bado ana maono ya kuongoza hasa katika nyadhifa za Taifa.

Na mwisho nilichobaini ni kwamba uongozi wa Mzee Mutaragara Chirangi
haukuwa katika nyanja moja tu bali ameweza kiongozi katika nyanja tofauti tofauti za elimu, kisiasa, kidini, kiutamaduni, kiuchumi na kimaendeleo.
**************************************


UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 274
JAJI, DAN P. MAPIGANO
Dar es salaam
09/09/2004

MAELEZO:

Siku ya tarehe 09.09.2004 nimefika hapa kwa kaka A. M. Chirangi kuona mradi wake Majengo ya makazi, mashamba, bustani n.k. kwa kweli ni mradi wa ubunifu mkubwa na wa kupendeza. Bila shaka utekelezaji wake kikamilifu utahitaji gharama kubwa, subira na kikubwa zaidi baraza za mbinguni. Naamini kabisa kwamba kaka ni mwenye subira, dhamira na bidii. Anachohitaji hasa ni uwezo wa kukabili gharama zinazohusika. Na kwa hilo amtegemee zaidi Mwenyezi Mungu na misaada ya hali na mali toka kwa wote wanomtakia ufanisi kidhati.

Mungu amsaidie na kumbariki.
*******************************************

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 268. Mwl. Happines Baitan & Mwl. Devotha Damas
S.L.P. 128, Musoma
Mara

MAELEZO:

SHUKRANI:
Shukurani zetu zikuendee kwa kutukaribisha nyumbani kwako na kufanya ziara kwenye nyumba yako iliyoko Kigera.

Kwa kweli tulifurahia sana ziara hiyo ya tarehe 08/05/2004, hatutaisahau maishani mwetu.

MAMBO TULIYOJIFUNZA:
Kwa kweli ni mambo mengi sana na muhimu tuliyojifunza kutoka kwa Mzee M. Chirangi, nayo ni:-

i) Ukarimu
ii) Upendo
iii) Ushirikiano na watu wa aina zote.
iv) Utunzaji wa kumbukumbu.
v) Uongozi kwa ujumla.
vi) Busara na hekima
vii) Utunzaji wa muda.

MAONI YETU:
Maoni yetu tunaomba mambo muhimu tuliyojifuza kwako mathalani ukarimu, upendo, ushirikiano, maamuzi ya busara n.k uendelee kuirithisha jamii.

Na mwisho tunakuombea Mwenyezi Mungu akujalie ili uweze kutimiza malengo yako na hasa ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba yako ya Kigera.
Na Mungu akubariki na kukufanikisha katika yote.
***************************************************************

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 266.
MR. DAVID M. SINDA
MWENYEKITI RED-CROSS MARA 2000 - 2005
TRCS

MAELEZO:
Nimekutembelea leo tarehe 26.4.2004 baada ya kunitembeza katika miji yako, maeneo ya kazi za mikono, uandishi wa vitabu, nyaraka na utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali.

“ NIMEGUNDUA”
Vitu vikuu vya kuigwa kutoka kwako ambavyo ni sifa za kiongozi anayefaa katika jamii.
(a) MUDA:
- Wewe unajali muda kuwa ni mali na uheshimiwe/kutukuzwa na watu wote kwani haurudi nyuma bali unaenda mbele.

(b) MCHAPAKAZI:
- Nimeamini kuwa kila mtu anatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili uzeeni ufaidi matunda (Nyumba bora, watoto, shule).
- Umetoa nguvu zako, pesa zako, akili zako muda n.k. kwa ajili ya kuendeleza jamii ya Tanzania husasani Musoma na Kata ya Kigera (utengenezaji wa mabarabara) Mungu akubariki.
- Ni vizuri jamii iige na kutekeleza.

(c) MTU ASIYEPENDA DHULUMA:
- Mimi sikuwepo katika uongozi wako, lakini jamii inakushuhudia hukujihusisha na rushwa wala dhuluma katika jamii. Nakupongeza na Mungu aendelee kukuimarisha katika tabia hiyo.

(d) MKARIMU MPENDA ELIMU NA MTOA MISAADA KATIKA JAMII:
- Nimeangalia na kuchunguza kwa undani vitabu na kumbukumbu zako zimeonyesha umesaidia wazee, vijana, watoto katika misaada mbalimbali ya vitu, pesa, vyakula, mawazo, ushauri.
- Nakushauri usifunge milango katika talanta hiyo.
- Pia hongera kwa kusomesha watoto.

(e) KIONGOZI BORA:
- Mtafiti/mvumbuzi.
- Mwenye hekima.
- Mwadilifu na mshauri.
- Msafi. - Mpenda Mungu.

MWISHO:
Nina imani na tumaini kwa akili za binadamu kuwa wewe ni mjoli wa Mungu. Nilichojifunza kwako, Mungu akipenda nitakuwa tayari kukifanyia kazi katika jamii. Nakushukuru kunikaribisha nyumbani kwako pia kushiriki chakula cha jioni pamoja cha kimwili na kuomba pamoja kwa Mungu wetu aliye hai.
Nakutakia kazi njema na Mungu aendelee kutubariki na kutuandaa familia hizi mbili kwa WOKOVU UJAO.
********************************************

UTAMBULISHO WA MGENI:

Namba. 252.
MWL. JOHN M. SARARA.
MUSOMA TECH. SCHOOL
08/06/2003

MAELEZO:

MAONI YANGU JUU YA MZEE AMOS MUTARAGARA CHIRANGI.

Ziara yangu ya masaa 5 Nyumbani kwa Mzee A. M. Chirangi Kamnyonge na Kwangwa tarehe 08/06/2003 kuanzia saa 9 Alasiri hadi saa 2 Usiku. Ninayo mengi ya kujifunza kwetu na jamii kwa ujumla. Ilikuwa Jumapili njema.

Ni waheshimiwa wachache wanaoweza kukutana na watu wasio wa tabaka lao wakakaa kindugu, wakawapa ushauri, wakawaomba ushauri wakala na kunywa pamoja, wakaona shughuli za mfano wa kusali pamoja na hata kupoteza muda kama alivyofanya na anavyofanya Mheshimiwa Mzee Chirangi.

Ni waheshimiwa wachache wanao weza kuwaonyesha walio wengi njia sahihi ya kufuata
MUDA/RATIBA na kuonyesha kwa vitendo bila kinyongo njia ya mafanikio ikiwemo Elimu, Kazi, viwanja,Ndoa, utunzaji kumbukumbu na kuendesha michango bila kudai malipo au kamisheni.

Ni waheshimiwa wachache wanaoweza kuishi na watu bila ya kujikweza na kujivuna kwa nyadhifa zao au kikauli na badala yake kuishi na watu kuwa sehemu ya jamii.

Ni waheshimiwa wachache wanaoweza kumtukuza Mungu wakati wote wa madaraka yao na kukubalika na madhehebu yaliyo mengi.

Ni waheshimiwa wachache wanaoweza kuvumilia kuwa katika Chama cha Siasa hukuitetea Serikali ambayo inayo onyesha kuwasahau baada ya kuwa wamevitumikia vyombo hivyo kwa uaminifu, haki na uadilifu katika maisha yao yote.

Ni waheshimiwa wachache wenye kumbukumbu za kila siku za maisha yao, licha ya kuwa wanaouwezo wa wasaidizi, wanayo Elimu na vyombo vya kutunza kumbukumbu.

Ni watu wachache wenye hazina nyeti za Serikali ambazo nadhani hata Serikali inazihitaji lakini inashindwa kuzitumia.

Yako mengi lakini yote haya na sifa hizi anazo Mzee, Mwalimu A. M. Chirangi, Mwanasiasa mkongwe, Mwanahistoria, Mwandishi, Mzazi, Mzee mwenye utu, Busara na hekima anayeonekana kusahauliwa lakini HISTORIA HUENDA IKAJA KUTUSHITAKI.

Ziara yangu na maisha yake yanaelekea kufanana na ya Baba wa Taifa licha ya tofauti ya nyadhifa walizokuwa nazo. Nina imani busara na Mawaidha yake, kazi na maono yake yatakumbukwa na kudumu Daima na siku moja Mtaa, Barabara ya Chirangi itakuja kuwa maarufu si Musoma tu bali Nchi nzima.

AU.

Familia yake, watoto au wajukuu watakuja kurejesha jina na Hadhi za Chirangi kama wataenzi kazi na Busara ya Mzee A. M. Chirangi na mtaa wa Chirangi pia nyumba ya Mzee wetu iliyoko Kwangwa.

Ni namwombea Mzee Chirangi maombi yake matano yafike kwa Mwenyezi Mungu na yapate majibu mema.

Namwombea kwa Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, vyama vya michezo, Mashirika ya Dini, Ndugu, Jamaa na Marafiki tuenzi kazi zake kufanya kila liwezekanalo kuenzi kazi zake na busara yake na kujibu maombi yake kwa vitendo.

Aidha namwombea Mzee M. Chirangi asijutie aliyoyafanya na matusi au bezo anazozipata. Hata Yesu alitemewa mate leo tunamtukuza. Farijika na kuwa na familia yenye furaha, iliyoelimika na matunda ya kazi zako na misaada uliyotoa Mungu akubariki na atakupa afya njema.

Tuombee na sisi tunaothamini mchango wako wa hali na mali na busara zako zimekuwa kioo na dira kwetu, WASAMEHE WALIOKUKOSEA.
Na siku Mungu akikuchukua usijutie, farijika kwa vile umejiandalia kaburi na staili ya mazishi ulale pema peponi, uiombee Musoma, Tanzania na Dunia kwa mema.

Ziara yangu kwako ni ya KIHISTORIA, KIOO NA DIRA, nitakuja tena kuchuma Busara zako.
*************************************************************************

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 242.
Lucas O. Wadenya
S.L.P 1405
Kisumu - Kenya -
03 Octoba 2002

MAELEZO:

Mimi Lucas O. Wadenya nimemtembelea Ndg. Mutaragara Amos Chirangi na kutembezwa katika mazingira yake yote. Mambo ambayo nimevutiwa na Mzee huyu ni mtunzaji wa takwimu zote za kila siku za aina zote kitu ambacho sijawahi pata kuona kwa mtu yeyote tangu niwepo. Pia ameteyalisha kaburi hivyo amekumbuka kuwa kuna kifo kitu ambacho si rahisi kwa watu wengi. Molla akuzidishie baraka.
***********************************************************************************
UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 194.

Ndg. C. I. Mtengera,
MHASIBU HAZINA NDOGO
MKOA WA MARA
S.L.P. 974,
Musoma
October, 1999

MAELEZO:
Mpendwa Mzee A. M. Chirangi,

Nashukuru kwa kunipa fursa ya kuyatembelea maeneo ya KIGERA na KWANGWA ambayo kwa juhudi zako binafsi ukiwa kiongozi wa Chama uliwezesha maneno hayo kupimwa na barabara nyingi kupasuliwa.

Ni kitendo cha kuruhusu watu wa kawaida na wa juu kufika na kutembelea nyumba yako ni ushahidi sahihi kuwa nyumba hiyo haukujenga kwa kipato chenye hila.

Hivyo nakuombea kwa Mungu akujalie maisha mema uweze kukamilisha jengo hilo.
Kadhalika namwomba Mungu azifungue nyoyo za watu waweze kukubali kutoa michango yao ya hali na mali uweze kulikamilisha jengo hilo na hatimaye uhamie na kuishi humo. Hivyo ndivyo njia pekee ya kukuenzi na kuzikumbuka fadhila zako kwa wananchi.

IKUMBUKWE KWAMBA KILA MTENDA WEMA DAIMA ATAKUMBUKWA KWA WEMA.
********************************************************


UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba.157.
B.M. MAZIKU
MHANDISI WA MJI, MUSOMA.

MAELEZO:

Nimetembelea eneo la Mzee A. Mutaragara anakojenga nyumba mpya. Nampongeza sana kwa juhudi zake hizo. Pamoja na yeye kujitolea kutengeneza Barabara.

UTAMBULISHO WA MGENI:
Namba. 209.
Ng’araga
AFISA UHUSIANO
VI- Agroforestry Mara
20/01/2001

MAELEZO:
VI – Agroforest Project inampongeza Mzee A. M. Chirangi kwa ujumla kwa yote ambayo yanaendelea katika eneo lake. Hii ina maana kwamba yeye ni kielelezo bora ndani ya Mji wa Musoma.

Katika matendo yake na utekelezaji wake Mutaragara mradi tutakuwa naye katika kuboresha mazingira ya kilimo mseto katika maendeleo yake. Pia shamba hilo litakuwa ni mfano kwa watu wa Kata ya Kigera.

Namtakia kazi njema na Mwenyezi Mungu amsaidie.











Nyote bado mnaendelea kukaribishwa. Baada ya utafiti na mashauriano kuhusu hiyo nyumba iliyoko eneo la Kwanga, mipango imewekwa kuwa siku za usoni ukifuata hicho kibao cha Chirangi Street utakuta na Bethsaida Centre for Health and Development ambapo huduma mbalimbali za Afya zitatolewa kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Baba katika harakati zake za kunyanyua viwango vya maisha ya Watu.
____________________________________
----------------------------------------------------------------

VIUMBE SABA , IMANI JUU YAO NA MATUMIZI YAKE KWA WATU WA JAMII YA WARURI NA MAKABILA YANAYOLANDANA NAO KATIKA UKANDA WA ZIWA VICTORIA.








Hii ni moja ya Makala nyingi zilizoandikwa na Mutaragara Chirangi.

Jamii ya Waruri na makabila yanayoshabihiana kwa karibu kiutamaduni kama vile Wakwaya na Wajita wamekuwa na imani mbalimbali juu ya baadhi wa wanyama wa aina mbalimbali. Aidha wamewatumia wanyama hao katika maisha yao ya kila siku si kwa ajili ya chakula bali zaidi kama nyenzo katika tiba au kuboresha shughuli za maisha yao. Hapa chini nakutajia viumbe saba na matumizi yao.

I. INDURUTI
Induruti ni jamii ya wadudu wadogo kama Inzi mdogo.
Kuna aina mbili za Induruti kama ifuatavyo:-
A. Iduruti inayozalia ndani ya mashimo ya miti na mapango ya mawe.
B. Induruti inayozalia katika mashimo ardhini.

Uwezo / Matumizi
Induruti ni miongoni mwa viumbe wenye sifa kubwa. Waganga wa Tiba Asilia hutambua umuhimu wao na kuwathamini. Matumizi mengine ni kama vile ifuatavyo:-

A. Induruti inatoa asali nzuri na tamu kuliko asali ya nyuki ambayo hutumika kama chakula na wengine kuitumia kama sehemu ya dawa asilia, kama dawa kuongeza mvuto wa kimapenzi, kama dawa kwa ajili ya biashara,kama dawa ya kuzindua miji ya watu, dawa kwa ajili ya ushindi wa michezo n.k
B. Induruti huaminika kuleta taarifa mbalimbali kwa kuandamana na watu njiani kama askari ili kufuchua ‘siri’ za watu.


II. IMBURUKAKA – (Kaka-kuona)
Imburukaka ni jamii ya keng na kobe na pia hujongelea polepole. Ingawa ni mkubwa kuliko kobe, Imburukaka ni kudra sana kuonekana kwa watu. Mahali alipo mara nyingi unaweza kukuta pia wanaishi na nyoka wa eneo hilo. Imburukaka ina uwezo wa kuvuta viumbe vingine.

Uwezo / Matumizi
Waganga wa Tiba Asilia wanaitumia kwa dawa ya:-
A. Mvuto kwa watu - Ekisagara
B. Kuongeza mauzo katika Biashara – Samba
C. Hutumika kwa Mazindiko ya miji na kwa kinga ya watu.
D. Huweka hofu – mamlaka ya utawala uwezo kama Simba.
E. Samba ya mapenzi na zindiko.


III. INJILILI (NYAMWERA OMWANA WA INJILILI)
Injilili ni ndege mwenye umbo zuri la kupendeza na kuvutia. Katika macho yake, Injilili ana ngozi au utando wa aina mbili, unaomuwezesha kuona ndani ya maji na wa pili humuwezesha kutumia katika nchi kavu, kama mamba. Injilili ana manyoya mazuri sana na hayalowani maji kwa urahisi kama ya bata. Ana manyoya yenye rangi zaidi ya tatu – udhurungi, Kijani, nyekundu, bluu na nyeupeInjilili ni aina ya ndege mwenye hulka na uwezo mkubwa kwa kujitosa kilindini (Murwena kuruondo) na kutandika kiota cha makazi yake huko kwa kuzificha siri zake ndani sana

Majina mengine ya Injilili.
Anaitwa Injilili Nyamwalika kuruondo – kurwena mwitubi bhya magoji (Kilindini). Pia anajulikana kama Injilili mzalia chini ya Bahari kama alivyo Mzamia lulu madini yenye thamani kubwa

Uwezo / Matumizi
Waganga wa Tiba Asilia uthamini viungo vya ndege huyu kwa ajili ya matumizi ya dawa hususani kama vile:-
A. Dawa ya mvuto – (Samba)
B. Kuzuia bahati mbaya (nuksi)
C. Kuepusha madhara au maafa fulani



IV. OMUNYAMUNYA.
Omunyamunya ni jamii ya mnyama mdogo sana kama panya mkubwa (panya- buku). Ngozi yake ina mfano wa miiba kama ya Nungunungu.

Uwezo / Matumizi yake
A. Hutumika kuongeza mvuto wa mapenzi na wa biashara
B. Hutumika kwa kuweka zindiko la mali



V. IPINGU.
Ipingu pia ni jamii ya ndege mdogo.

Uwezo wake
A. Ana uwezo mkubwa wa hurka ya maono na hisia.
B. Ana uwezo wa kutambua ni wapi kuna mzoga hata kama ni mbali kwa kutumia milango yake ya fahamu kama Fisi.
C. Kusaidia kugundua mazuri na mabaya.

Matumizi yake
A. kusaidia Kutambua mazingira ya mahali fulani
B.Kusaidia kutambua maadui walipo.
C. kuongeza uwezo wa kutambua na kutafsiri ndoto ( imbwira)

VI. KUNJU MUROGOMBI:
Kunju ni jamii ya ndege. Kunju anaumbo la mvuto. Ni msafi na muimbaji hodari kwa kuigiza semi au sauti za watu.

Uwezo / matumizi yake.
A. Hutumika kama pambo
B. Jina lale (Murogombi) hutumiwa na wanasiasa kumtambulisha Mhutubu shupavu



VII. ITARITA – MUFUBYA NG’ENDO (SAFARI)
Itarita ni jamii ya ndege akaaye porini kwenye miti na mapango ya mawe. Ni ndege aliyefunikwa na manyoya mengi.

Matumizi yake
kitokea ndege huyu akalia wakati mtu anaandaa safari (Orugendo), basi mtu huyo huweza kuahirisha hiyo safari. Safari huahirishwa pia pale ambapo ndege huyu anapokatiza barabara/njia mbele ya mtu aanzaye safari. Imani ni kuwa safari hiyo itakuwa na mikosi au matatizo fulani makubwa. Ndiyo sababu anaitwa Mukubya – Mufubya Ng’endo yaani Mvunja safari.

Hivyo Itarita hutoa tahadhari kwa wasafiri na hivyo pia kuaminika kuwa mpiga mbiu ya taadhari wakati wa hatari.

Wednesday, January 2, 2008

HOTUBA YA A.M. CHIRANGI - MWENYEKITI WA CCM WILAYA YA MUSOMA MJINI KWENYE MKUTANO MKUU WA CCM WILAYA YA MUSOMA MJINI - AGOSTI 1997.

Baada ya kutoa huduma kwa miaka 15 mfululizo, ebu msome kiongozi huyu anavyohutubu.


I. UTANGULIZI

A) SALAAM NA SHABAHA YA HOTUBA

Ndugu wasimamizi wa uchaguzi, ndugu wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM (W), ndugu wageni waalikwa, mabibi na mabwana. Awali ya yote ninapenda wasalimuni nyote na kuwakaribisheni kushiriki vema na kikamilifu katika kikao hiki cha Chama Wilayani Musoma Mjini.

Hotuba hii inakusudia kuwapeni picha halisi ya maendeleo ya Wilaya yetu kwa mtazamo wa Chama cha Mapinduzi na nasaha zangu binafsi kwa Chama na Serikali baada ya kuwatumikieni katika dhamana mliyonienzi kwa muda wa takribani, miaka kumi na mitano (1982 - 1997).

B) PONGEZI NA MAELEKEZO YA KAZI KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA CCM (W)
Ninachukua wasaa huu kwa moyo wa dhati pasipo husuda, wala uzandiki kuwapongezeni wale wote mliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano huu wa viongozi wa Chama katika ngazi za matawi na kata kwa kipindi cha 1997 – 2002 na pia kwa wale wote ambao majina yenu yamepitisha kugombea nafasi mbalimbali za Chama Wilayani, Mkoani hadi Taifa, dhamira na makusudio yenu katika kukitumia Chama ziendelee kwa kadri ya majukumu na nafasi zetu pasipo uvunjaji wowote wa miiko na maadili ya uongozi. Sote tunapaswa kuyaeneza matunda ya uhuru kwa wananchi wote kwa manufaa yao na maendeleo ya Taifa zima kwa ujumla.

Wajumbe wa kikao hiki pamoja na kazi nyingne zote mtakazokuwa nazo, mtapaswa kutoa maelekezo ya utekelezaji wa sera ya CCM kwa kipindi kijacho kutokana na taarifa ya kazi iliyotolewa na Halmashuri Kuu ya CCM Wilaya.

Aidha mtahakikisha kuwa maazimio na maagizo ya vikao vya ngazi za juu yanatekelezwa kwa maendeleo ya wilaya yetu na Taifa letu kwa ujumla.
Mtayazungumzia mambo yote yahusuyo: “Ulinzi, Usalama na Maendeleo ya Wilaya Musoma Mjini, mtaunda Kamati za Mkutano Mkuu wa CCM (W) kwa kadri itakavyofaa na zaidi ya yote mtashiriki katika Uchaguzi huru na wa haki kuwachagua:-
Mwenyekiti wa CCM (W), Wajumbe kumi kuingia Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, Wajumbe watano kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM-Taifa.
Ni mategemeo yangu kuwa mtatumia vizuri haki hiyo mliyonayo kuwasimika watu wenye stahili na moyo wa kuitumikia CCM, pasipo upendeleo.



C) SERA YA CCM
Ni bayana kuwa maendeleo ya Serikali ya chama cha Mapinduzi yanaendelea kupimwa na Watanzania wote kwa mizani iliyojiwekea yenyewe. Hii ndiyo sera ya CCM kama ilivyofafanuliwa katika ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Taifa ya CCM ya Oktoba 1995.

Ndugu viongozi, sote tunapaswa kuelekeza nia, nguvu, raslimali, ujuzi na uzoefu wetu wote katika mwelekeo wa ilani hiyo kwa kipindi chote cha 1995 - 2002.

Yafuatayo ndiyo maeneo muhimu ya kuzingatia ili CCM iendelee kupata ridhaa ya wananchi wengi zaidi wa Tanzania na hivyo kuiwezesha kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi kijacho cha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000, na hatimaye katika kuwafikisha Watanzania kwenye Mapinduzi ya kweli na kuendeleza mapambano dhidi ya aina zote za unyonyaji, udhalilishaji, udhoofishaji na uzoroteshaji wa maisha na uchumi wa Taifa letu.

i) Kutumia sayansi na teknolojia katika uchumi.
ii) Kuimarisha kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa.
iii) Kuimarisha na kuendeleza viwanda vyetu, mashirika ya Umma machache yenye faida na kukuza biashara.
iv) Kuhimiza matumizi bora ya maliasili, kukuza utalii na kuhifadhi mazingira.
v) Kuendeleza uchimbaji madini na kupanua sekta ya nishati.
vi) Kuimarisha sekta ya mawasiliano na uchukuzi.
vii) Kuboresha na kupanua huduma za jamii hususani elimu, afya, maji na nyumba.
viii) Kuimarisha na kuzienzi fani za michezo na sanaa.
ix) Kuongoza kwa kufuata kanuni za Menejiment, biashara na kujitegemea katika kuliinua pato la Taifa.
x) Kuzingatia nafasi, haki na wajibu wa wafanyakazi, vijana, wanawake na walemevu katika jamii yetu.
xi) Kuimarisha ulinzi na usalama.
xii) Kuboresha uhusiano wetu na nchi za nje.
xiii) Kudumisha ushirikiano na umoja. Kudumisha Muungano kati ya Tanzania Bara na visiwani.
xiv) Kuimarisha Chama.

II. MIZANIA YA KAZI ZA CCM (W) KWA KIPINDI CHA 1992 – 1997
Ndugu Wajumbe, siyo kazi rahisi kuandaa mizania ya mahesabu ya taasisi au kampuni fulani. Kwa kuwa kabla ya kufanya hivyo wataalam hukamilisha kwanza kazi ya Kuorodhesha mali, wadai na wadeni katika kipindi husika.

Ili kuweza kuonyesha uwiano wa hasi na chanya. Sawia na mfano huo; tunawajibika kuorodhesha mafanikio na matatizo yote yaliyojitokeza kwa kipindi husika. Sikusudii kutoa taarifa ya kazi ya CCM, bali ninadodosa machache yake niliyoyaona muhimu katika kipindi changu cha uongozi. Jinsi yalivyoathiri maendeleo yetu na ikiwezekana mapendekezo yangu:-

i. Uanachama
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka huu 1997 tunao wanachama wa CCM 6262 ikilinganishwa na wanachama 7061 waliokuwepo mwaka 1992 kabla ya kuyafunga matawi ya sehemu za kazi na majeshi.

Hata hivyo, uchunguzi wa kina unaonyesha kuwa uhai wa wanachama waliopo hauridhishi sana hususan baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

ii. Vikao vya Chama 1997
Suala la vikao kwa mujibu wa Katiba limetekelezwa kwa kiwango kikubwa. Hasa katika ngazi ya Wilaya na chini ya wastani katika ngazi nyingine kama ifuatavyo kwa mwaka 1997:-

NGAZI YA VIKAO
ASILIMIA YA LENGO
Vikao vya Kamati ya siasa
Vimefanyika mara saba =>100%
Vikao vya Halmashauri
mara tatu =>100%
Vikao vya Mkutano Mkuu
Mara mbili =>100%

iii. Mashina na matawi ya CCM
1987, kulikuwa na jumla ya mashina 550 ya CCM mwaka huu 1997, idadi ya mashina imeogezeka na kufikia 808. Mwaka 1987, kulikuwa na jumla ya matawi arobaini na tatu (43). 30 yalikuwa ya sehemu za kazi na 13 ya mitaani. Mwaka jana (1996) tulikuwa na jumla ya matawi 56, katika kata 3.

iv. Jumuiya za Chama 1997
Wilaya inazo Jumuiya tatu (3), yaani; vijana, wazazi na Wanawake zinazoongozwa na Chama. Kwa ujumla Jumuiya hizi zina maendeleo ya wastani tu.
Kazi kubwa ambazo zimeweza kufanywa na Jumuiya hizo ni kama vile:-
1. Kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM na kuunda matawi mapya.
2. Kutoa hamasa kwa Umma juu ya umuhimu wa Elimu na ujenzi wa mashule.
3. Kuunga mkono kwa dhati CCM katika chaguzi mbalimbali za Serikali.




v. Michango
Tangu mwanzo wa kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi vya siasa, kumekuwepo na kuteremka kwa kiwango cha utoaji michango ya hiari na ya wajibu. Ni vema tuendelee kuelimisha, kushawishi na kuhimiza wanachama. Ili wawe wote wakilipa ada zao na kutoa michango inayowahusu. Ni muhimu zaidi kukusanya, kuzitunza na kuzitumia fedha zinazopatikana kwa kufuata kanuni za fedha kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CCM.

vi. Elimu
a) Elimu kwa Wanachama Ni bayana kwamba CCM irejeshe Idara au kitengo maalum kinachoshughulikia suala la Elimu na mafunzo kwa viongozi na wanachama wote wa CCM, ili kuwajenga na kuwaimarisha, kwa maana pasipo hilo tutaendelea kujenga Chama chenye wanachama wenye ufahamu finyu kichama, kisiasa na hata kiitikadi, kwa sasa inatolewa kwa kiwango cha chini.


b) Elimu kwa wote. Katika kipindi cha 1992 - 1997, tumeweza kusimama kidete, kuimarisha elimu wilayani. Ogezeko la idadi ni ushahidi kamili:
Pamoja na juhudi hizo, bado Wilaya inahitaji kuongeza au kukamilisha baadhi ya Madarasa na madawati. Na kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusu kuwaandikisha watoto wao wenye umri wa kwenda shule. Tunayashukuru mashirika binafsi mfano madhehebu mbalimbali ya dini kwa kuanzisha shule za chekechea (Kindergarten Schools). Shule hizi ndizo msingi madhubuti kwa elimu ya juu.

vii. Ulinzi na Usalama
Kwa wastani, kumekuwa na hali ya utulivu na amani katika Wilaya yetu. Jukumu zima la ulinzi na usalama limeelekezwa kwa wananchi wenyewe zaidi kuliko kuiachia dola na vyombo vya usalama pekee.

Mashauri mbalimbali yaliyoendeshwa chini ya mabaaraza ya jadi yamemalizika mapema na haki kuonekena kutendwa, kwa pande zote: yaani walalamikaji na walalamikiwa. Kinyume chake, kumekuwa na malalamiko kadhaa ya wananchi juu ya kucheleweshwa kwa mashauri katika Mahakama hususani Mahakama ya mwanzo.

Tunaipongeza pia idara ya uhamiaji, kwa kazi yake nzuri ya kusimamia na kulinda taratibu za watu waingiao na watokao nchini.

viii. Afya
Mada hii inaangaliwa katika uwanja mpana kutokana na maana halisi ya neno Afya kama lilivyoainishwa na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linalosisitiza; ‘Ukamilifu wa hali ya mtu na jamii kwa ujumla, kimwili, kiakili na hata kisaikolojia. Na kwamba haimaanishi kutokuwepo kwa maradhi au ulemavu pekee’.

a. Huduma za afya bado hazijitoshelezi katika Wilaya. Hii ni kutokana na ukosefu wa chakula, madawa na vitendea kazi hususani, katika Hospitali yetu ya Mkoa na hata kituo chetu cha huduma za kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano cha Nyasho (MCH – Clinic). Aidha zahanati za watu binafsi na maduka ya dawa mengi yametakiwa kufungwa kutokana na kutokuwa na sifa za watumishi, vifaa na majengo yanayopaswa kwa mujibu wa taratibu za sasa za Wizara ya Afya.

b. Tunawapongeza wafadhili wote ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya afya au shughuli zinazoinua kiwango cha afya ya mwananchi hapa Wilayani nazo ni:- Uzazi wa mpango, (Family planning), Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mama na mtoto (SCPD), Mpango wa Chanjo (EPI), Mradi wa HESAWA, Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma (TB and Leprosy Control Programme), Udhibiti wa Ueneaji wa UKIMWI (NACP), Udhibiti wa ueneaji wa magonjwa ya Kuhara (CDD), n.k Wananchi walio wengi wamefaidika na wataendelea kufaidika na huduma zilizotolewa na miradi hiyo ya kitaifa au kanda ya ziwa, pasipo kuzisahau siku za chanjo za Kitaifa (NIDs) dhidi ya ugonjwa wa “Kupooza” ambapo wilaya yetu kwa awamu mbili (1996) tulivuka lengo la kitaifa (95%).


c. Ni jambo la kujivunia pia kuwa: Wilaya ya Musoma Mjini ndiyo imeongoza kitaifa kwa tathimini ya kwanza katika utekelezaji wa mfumo wa taarifa za uendeshaji huduma za afya (MTUHA).

d. Sambamba na vituo vya afya, ndani ya Wilaya hii tunavienzi vyama vya hiari kwa ajili ya kuboresha maisha ya welemavu Tanzania (CHAWATA), Chama cha Maalbino, Chama cha wasioona, na vyama vinginevyo kama vile The Lions Club, Msalaba Mwekundu (Red Cross) n.k.

iv. Ushirika
Ni masikitiko makubwa kuwa chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Mara (MCU- 1984 Ltd) kimefilisiwa na kufutwa katika kipindi hiki, kutokana na kushindwa kujiendesha kifedha, ikiwa ni athari zitokanazo na uongozi mbaya, ubadhirifu, ulafi (Institutionalized greedy), na malimbikizo ya riba kubwa ya NBC.

x. Maji
Ukosefu wa maji kwa maeneo mengi ya wilaya bado ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa kudumu. Aidha kuna baadhi ya sehemu zenye mabomba ambazo bado hazipati maji kwa mashine kushindwa kusukuma maji.

Tunaushukuru mpango wa Hesawa kwa kutuchimbia kisima kimoja cha maji huko Bweri. Ni vema kama Hesawa itaendelea na msaada wa jinsi hiyo kwa maeneo mengine ya mji wetu.

Ikumbukwe kwamba, watu wengi wanaopata maji kutoka ziwani au mtoni wanayatumia hivyo hivyo tu, bila kuyachemsha wala kuchujwa. Ni vema elimu hiyo isambazwe na kuenea kwa watu wote ili tuweze kudhibiti magonjwa yasababishwayo na kunywa maji machafu na yasiyo salama.
Jumla ya vituo vya maji bomba 5 vimejengwa katika kipidi hiki.

xi. Barabara
Barabara kuu ya Nyerere inahitaji kufanyiwa ukarabati na pia kupanuliwa. Barabara zingine za ndani zina hali mbaya. Ni vema zikarabatiwe na kuwekewa mitaro kwa kutumia njia ya kuwashirikisha wananchi.
Aidha, Halmashauri ya Mji inapaswa kufikiri namna ya kurejesha Taa za barabarani ili kuongeza mwanga na kwa ajili ya usalama nyakati za usiku.

Jumla ya barabara 20 mpya zilitengenezwa katika Kata ya Kigera eneo la Kwangwa ‘A’ zinapaswa kutunzwa. Barabara zilitengenezwa kwa juhudi zangu nikishirikiana na Halmashauri ya Mji na wakazi wa maeneo hayo,

xii. Burudani na Michezo
Wilaya inatoa pongezi za dhati kwa kanisa Katoliki kwa kukiendesha kituo cha Michezo kwa vijana (Hope Centre) kinachopakana na Kituo cha Utamaduni cha Musoma (MCC). FAT Wilaya na Baraza la Michezo (W) wanapaswa kuwa na mikakati madhubuti kwa kuwashirikisha wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo Timu yetu ya Maji F.C. iliyoko daraja la I Taifa.
Idara zihusike kuwashirikisha wananchi na wafadhili mbalimbali kushughulikia kasoro za wazi zinazoonekana kwa mfano kutokamilika kwa uwanja wa kumbukumbu ya Karume, kutokuwa na kituo cha michezo ya watoto wadogo, ukosefu wa bustani nzuri ya kupumzikia na upungufu wa vikundi vya kudumu vya usanii katika fani zake (k.v. maonyesho, lugha na ufundi).

xiii. Umeme
Nishati hii inaendelea kusambazwa na kusimamiwa na shirika la Umma TANESCO. Kwa sasa umeme unaotolewa ni wa uhakika. Tatizo bado ni wanachama wengi kushindwa kumudu gharama za kuingiza (Installation charges) umeme katika nyumba zao.

xiv. Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi
Katika kipindi hiki kumekuepo na mabadiliko ya mitambo ya njia za simu katika mji wa Musoma na via yake. Kitu ambacho kimeongeza uthamani wa huduma za simu. Zipo ofisi chache Musoma zenye huduma za Fax, Telex na E-Mail. Shirika la Posta limeendeleea kutoa huduma ya kusafirisha na kupokea barua, vifurushi na vipeto.

Njia zote za usafiri na uchukuzi hutumika kuingia au kutoka nje ya Wilaya hii. Kwa mfano:-
a. Nchi Kavu:
Kuna magari mengi madogo na makubwa ya abiria, kwenda sehemu zote.
b. Majini Kuna mitumbwi, na boti za watu binafsi, Meli mara nyingi hutumika kwa ajili ya kusafirisha mizigo (shehena) badala ya abiria.
c. Angani: Shirika la Ndege Tanzania (ATC), JWTZ na wakati fulani mashirika binafsi yanayomiliki ndege ndogo kama vile MAF na AIM n.k. yanaendelea kuutumia uwanja wa ndege wa Musoma kubeba au kuteremsha mizigo, hali Kadhalika, kusafirisha abiria.

Aidha wananchi tunasikiliza redio na kupata magazeti mengi siku hizi. Wachache kati ya wakaazi wa mji wetu wamebahatika kuwa na vyombo vya Televisheni (T.V Sets) vinavyowawezesha kuona na kusikia habari za dunia hii kwa kupitia studio za nchi za nje. Hata hivyo wengine wengi wamekuwa wakifika kwenye kituo chetu cha Utamaduni (Musoma Cultural Centre), kwenye kumbi mbalimbali za burudani, kwa ajili ya kuona na kusikiliza matangazo ya televisheni.

xv. Kilimo, Ufugaji na Uvuvi
Hizi ndizo shughuli kubwa wanazojishirikisha wananchi wa Wilaya ya Musoma Mjini kwa ajili ya maisha yao.

Kwa ujumla kinachoonekana ni kwamba shughuli hizi zinaleta pato dogo sana kwa wananchi wa Wilaya kwa ujumla kwa vile bado hatujatumia sayansi na teknolojia kwa wingi katika shughuli hizo. Aidha, bado wengi wetu hatufuati kanuni na maelekezo ya kilimo, ufugaji au uvuvi wa kisasa.
Katika kipindi hiki, tatizo kubwa lililojitokeza ni ukame wa muda mrefu uliosababisha njaa katika wilaya yetu.
Tunaushukuru Serikali kwa kutuletea chakula cha msaada kuokoa maisha yetu. Kazi ya uvuvi imeathirika na matatizo mbalimbali kama vile kuenea kwa magugu maji yanayoua samaki na uvuvi haramu kwa kutumia sumu; kitu ambacho kimeathiri soko la minofu ya samaki wetu huko nje. Ni vema kuwa idara ya Mali Asili na vyombo vya dola visaidie kuwakamata wahalifu wote na kuwaadhibu ipasavyo. Hata hivyo ushirikiano wa wananchi wenyewe unahitajika kwa kiwango kikubwa. Uvuvi bora utaweza kuleta faida kubwa zaidi kwa kuliinua pato la Wana Musoma na Taifa letu kwa ujumla.

xvi. Viwanda
Pamoja na kuongezeka viwanda vipya hapa wilayani mfano: kiwanda cha magodoro, na viwanda vya kuandaa na kusafirisha minofu ya samaki, Chama kinasikitika juu ya kuanguka na kufungwa viwanda vyetu kama vile: kiwanda cha maziwa (Mara Milk),

Na kiwanda cha Nguo (MUTEX). Hii si tu imepunguza pato la mwananchi na Taifa, bali pia imepunguza ajira kwa vijana.
Utaratibu wa kuona kama upo uwezekano kwa kuvibinafsisha au kuingia ubia unaendelea kufanywa. Kiwanda cha soda za Vimto na SIDO bado vinaendelea kutoa huduma.

xvii. Mashirika / Makampuni ya Umma
Katika wilaya yetu yapo makampuni au mashirika yanayofanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii nayo ni:-

a. Benki ya Taifa ya Biashara (NMB) kwa sasa inaelekea kufanyiwa marekebisho makubwa na kuundwa upya, baada ya kuwa imefunga baadhi ya matawi yake. Kwa mfano Mukendo hapa Wilayani. Ni vema tuwaeleweshe wananchi mababadiliko haya ili wasipoteze uteja wao ambao ni ufalme na unahitajika sana kwa Taasisi mpya ya NMB 1997.
b. CRDB (1996) Ltd. Tawi limezinduliwa rasmi hivi karibuni, na Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere.
c. Kampuni ya simu (Telecom Company), kama ilivyokwisha kufafanuliwa mapema. Imeshauriwa vibanda vya simu viwekwe angalau kimoja kwa kila Kata.
d. Shirika la Posta na Benki ya Akiba limefunga pia baadhi ya matawi yake madogo. Vituo vilivyobaki vinaendelea kutoa huduma ya kusafirisha barua na vifurushi na kutunza fedha za watu katika akaunti kwenye benki ya posta. Hata hivyo tumeweza kupata huduma za utumiaji barua / vifurushi kwa haraka zaidi; kwa njia ya EMS na pia Money Fax inayowezasha kutuma fedha kwa haraka zaidi na usalama.
e. Kampuni ya Biashara ya Mkoa (RTC). Hii imefunga huduma zake kutokana na kushindwa kujiendesha, katika mfumo huu wa uchumi wa soko huria.
f. Shirika la Bima la Taifa (NIC), lienaendelea kutoa huduma ya kuwawekea bima watu, na mali zao kupitia ofisi yake kuu na mawakala wake.
g. Shirika la Taifa la Akiba ya Uzeeni (NPF); hili lina wateja wengi hususani, wafanyakazi wote wanaopaswa kujiunga na NPF kwa mujibu wa sheria. Tunashauri shirika liwe linatuma taarifa (statement) za jumla ya mafao ya wateja wao angalau mara moja kwa mwaka ili kuwafundisha kuhusu amana zao.
h. Shirika la nyumba la Taifa (NHC). Shirika hili linazo nyumba chache sana kulingana na mahitaji ya nyumba kwa wakazi, hasa watumishi wageni Wilayani, watumishi wa Serikali na mashirika ya umma na binafsi. Hata hivyo zile ziliaopo ni chakavu; ni vema kama zitakuwa zikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kabla uharibifu haujawa mkubwa. Kwani “Usipoziba ufa utajenga ukuta”.
i. Shirika la Maendeleo ya Wilaya (MUDECO); tofauti na jina lake, shirika hili lilikosa maendeleo kabisa hatimaye likafunga shughuli zake. Hii ilitoka ilitokana na kujiendesha kwa hasara na zaidi watu binafsi kujiondoa na kuondoa hisa zao. Hata hivyo mali (mtaji wa shirika) zilikuwa zinaibiwa mara kwa mara, kitu ambacho kilidhoofisha shirika.

xviii. Biashara na masoko
Dhamana ya masoko inagusa mambo makuu manne. Bidhaa/huduma itolewayo, bei yake, kutangazwa kwake na mahali pa kutokea/ kuuzia bidhaa / huduma. Hivyo kabla ya kuongelea biashara au masoko, Chama kinatuasa kuhakikisha kuwa tunazalisha bidhaa bora, za kutosha au tunatoa huduma za kuridhisha.

Ni vema Halmashauri ya Mji ifanye utafiti wa kina kuhusu kodi na ushuru unaofaa kutozwa kwa wafanyabiashara katika masoko yetu na penginepo katika vibanda au nyumba zao.

Inashauriwa kuwa: wafanyabiashara wadogo wadogo kama vile wanaong’arisha viatu, vinyozi n.k. wapewe nafasi za kustawi kwa kupunguziwa kodi, na utaratibu uwepo wa kuwapatia wote wenye leseni vitambulisho ili wasisumbuliwe kama wazururaji. Hata hivyo, itakuwa busara kama Halmashauri ya Mji wetu itaangalia uwezekano au itaandaa mkakati mpya utakaoiwezesha kukusanya ushuru wa vituo vya taxi na magari madogo ya abiria, kwa kuwa sasa, magari haya yanafanya kazi zao vichochoroni kwa kujificha, hivyo kuikosesha Halmashauri mapato yake.

xix. Hifadhi ya Mazingira
CCM inaendelea kutetea mazingira tunamoishi. Serikali Kuu na Serikali ya Mji waendelee kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira. Aidha, hatua kali zichukuliwe dhidi ya wachafuzi wa mazingira kwa mfano: wanaokata miti ovyo, kuchoma nyasi, wachafuzi wa hali ya hewa kutoka viwandani, magari na kadhalika. kuwepo na kampeni kamambe ya kudumu ya kila mwananchi kupanda na kutunza miti.

Elimu kuhusu hifadhi ya Mazingira itolewe mashuleni na zaidi kwenye Mpango wa Elimu ya Watu Wazima.



xx. Nafasi, haki na wajibu wa Jumuiya za Wafanyakazi, Vijana na wanawake.
a. Wafanyakazi: Serikali ivitambue vyama huru vya Wafanyakazi vilivyoshirikishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Tanzania (TFTU). Serikali isisitize juu ya haki na stahili za watumishi, mazingira ya kazi na vitendea kazi sambamba na nidhamu na uwajibikaji kazini. Tatizo la mishahara kuchelewa limeendelea kuwepo. Serikali ilitafutie ufumbuzi wa kudumu.
b. Vijana: Umoja wao ndani ya CCM uimarishwe na wahamasishwe ili washiriki katika kuzalisha mali kwa moyo.
c. Wanawake: Serikali iendeleze vita dhidi ya desturi na mila mbovu zinazowadhalilisha wanawake kijinsia. Wanawake wapewe nafasi sawa na Wanaume kwa kadri ya uwezo wao.

xxi. Huduma zaDini katika jamii
Wananchi wa mji wa Musoma wameendelea kupata huduma za kiroho kulingana na imani zao kwa kupitia kwenye madhehebu yao ya Kikristo Kiislamu, Kihindu n.k. Serikali ihakikishe kuwa waumini wanatatua na kusuluhisha migogoro yao wenyewe kama ipo ili kudumisha amani, usalama na utulivu.

III. NASAHA ZANGU BAADA YA MIAKA KUMI NA MITANO (15) KATIKA UONGOZI

Kipengele hiki kinabeba nguvu na udhaifu wangu kwa pamoja. Kwa muhtasari, ninakusudia kuwashirikisha katika mawazo au ndoto zangu juu ya mambo muhimu niliyoyaona katika kipindi hiki cha miaka kumi na mitano yanahitaji marekebisho, kuondolewa au kusisitizwa kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi mkazi wa Musoma Mjini.

Ndugu Wajumbe, kuweni huru kukubali au kutokubaliana nami maana huenda sikunukuu kutoka kwenye Katiba ya CCM, Mwongozo wa CCM, Programu ya Chama, Ilani ya Uchaguzi wala popote:-

a. Ukabila:Matumizi ya ukabila kwa gharama ya kumbagua mtu kutoka katika stahili au haki fulani,ni ugonjwa sugu ambao umesitisha maendeleo ya Musoma na Mkoa wetu wa Mara kwa ujumla. Tubadilike, tumkemee yeyote mwenye nia ya kutugawa kwa makabila ya lugha na sehemu tulizozaliwa.
b. Utamaduni wa uoga na kulindana:Maadili na miiko ya kiongozi kwa mujibu wa Katiba yanaendelea kusimama kidete, kama mti wenye mizizi mirefu bila kijali kimbunga kizungukacho. Kiongozi yeyote anayepotosha au kukubali kupotashwa kwa mahesabu ya kulinda maslahi ya wachache anyang’anywe dhamana aliyopewa mara moja; hata kama iko katikati ya meno yake …… Haki huliinua Taifa ……

c. Kazi ya Kujitolea:Ninashauri vikao vya CCM Taifa viangalie kwa upya muundo wa Chama na ikiwezekana virejeshe maslahi ya Watendaji wote kutoka ngazi za matawini hadi Taifa.

d. Kutowajibika Mkosefu:Mwanadamu anapaswa kutunukiwa kulingana na kazi aliyofanya, “nzuri au mbaya”. Kama wanafahamika kwa nini Chama kisiwajibishe wale wote wasionia mamoja nasi? Kwa mfano:- Waliokusanya michango ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wakaitumia. Waliofilisi M.C.U. (1984) Ltd pasipo kupewa kibali cha kuwa “Mfilisi”.

e) Kutokutii kanuni za menajimenti (Esprit de Corp and Unity of Direction)
Ni gharama kubwa sana kwa Chama, mtu au watu kuvunja kipande cha mnyororo Kinachounganisha Shina, Tawi, Mkoa au Taifa. Wakati mwingine tukubali kutokubaliana, lakini tubakie na umoja ushirikisha wetu, kama Chama.

f) Haki ya Kikatiba:
Wananchi sehemu moja au nyingine wameshuhudia kwa uchungu maumivu ya miaka Mitano ya kutawaliwa na sio kuongozwa na viongozi waisofaa kutokana na wananchi fulani kuamua kuuza haki zao za kupiga kura kwa thamani ya kitenge, chupa ya kinywaji, T-shirt n.k.


Kama ambavyo nimekuwa nikisema na kutenda, ieleweke wazi kuwa kiongozi achaguliwaye kwa kutoa fedha, ataongoza kwa kuchukua fedha, vilevile achaguliwaye kwa kufuata ukabila, atasimamia kabila, naye yule achaguliwaye kwa kampeni moto toka juu huenda akaondolewa kwa kampeni baridi kutoka chini. Aidha, ni kitendo cha kutokukomaa kisiasa, kujenga chuki na hasira kwa mtu yeyote eti kwa sababu ya kutokupigia kura, kukushinda kwenye uchaguzi au kuazimia kugombea nafasi uliyodhani umetengewa wewe pekeke.

IV. HITIMISHO:
Mungu, Muumbaji na Mpaji awabariki na kuwalinda nyote.
Ninawashukuruni wale wote tuliowahi kufanya kazi nao Wilayani, makatibu na Wajumbe wote.

Ninawapongezeni wale wote tulioshirikiana kwa dhati katika kampeni za uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge. Na katika Mji wetu wote waliochaguliwa ni wagombea kupitia Chama cha Mapinduzi.

Aidha Mgombea Urais na Mwenza wake kupitia CCM, ndio waliopata kura nyingi zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine katika Wilaya yetu, katika uchaguzi Mkuu wa Taifa wa kwanza uliovishirikisha vyama vingi.

Ninawiwa deni kubwa na Idara, Taasisi zote za Serikali, Jumuiya za Chama na wananchi wote wa Musoma Mjini kwa: Kunisahihisha, kunitathmini, kuniongoza, kunifundisha na zaidi ya yote; kunipa dhamana hii, maana sasa nimekuwa kama dhahabu iliyopitishwa kwenye moto.

“TUJISAHIHISHE, TUSAHIHISHANE NA TUSAMEHEANE”

Mungu Ibariki CCM! Mungu Ibariki Musoma Mjini!





KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

UONGOZI NA UTAWALA KATIKA CHAMA NA SERIKALI


Moja ya makala nyingi zilizoandikwa na Mutaragara



I. UTANGULIZI- TAIFA LENYEWE LILIVYO
Taifa ni watu au raia wa nchi hiyo kutokana na asili ya kuzaliwa au kuandikishwa uraia na uzalendo wa kuishi kwao. Taifa lina vyombo viwili ambavyo kwavyo majukumu mbalimbali hutekelezwa yaani Chama na Serikali (Utawala, Bunge na Vyombo vya mahakama na polisi).

CHAMA:
Kinazaa uongozi na kazi yake kuu ni kushika hatamu za uongozi wa kuweka sera, kuzisimamia na kuweka umbile la Serikali kwa kudhibiti utekelezaji wake.

SERIKALI:
Inazaa utawala, inatekeleza majukumu ya Taifa kwa kusimamia sheria zinazoundwa na Bunge lake na kulinda nchi kufuatia Katiba na taratibu zilizowekwa.

MAANA YA CHAMA:
Chama ni umoja wa watu waliojiunga pamoja ili kutimiza lengo, kusudi shabaha fulani. Kuna aina nyingi za vyama ambavyo vimegawanyika katika mafungu matano:-
i. Kidini - Uzima wa milele
ii. Kisiasa - Uhuru na kuweka sera
iii. Kiuchumi - Uzalishaji na faida
iv. Kiutamaduni - Michezo na burudani
v. Kijamii - Huduma mbalimbali

KAZI YA CHAMA:
- Kusimamia, kulinda, kutetea –Imani au shabaha yake.
- Kueneza, kukuza malengo, shabaha yake.
- Kulinda haki na hadhi ya wafuasi wake.
- Kuweka malengo, mipango, umbile la chama
- Kuweka ushirikiano, umoja kati yao.

CHAMA CHA KISIASA:
Ni cha watu wote Wakulima, Wavuvi, Wafugaji, Wafanya biashara, Wafanyakazi n.k. Ni mtetezi wa Umma dhidi ya uonevu, dhuluma na vitendo vyovyote vinavyonyima wananchi haki zao za kuwa raia huru katika nchi yao wenyewe. Chama ndicho kinajenga Ujamaa ili kutimiza demokrasi ambayo inaonekana katika vikao kutokana na maamuzi yake.

KAZI ZAKE:
Chama kinashika hatamu za uongozi wa kuweka umbile la Serikali na malengo yake. [Kuongoza ni kuonyesha njia]. Serikali inatekeleza malengo yaliyowekwa na Chama kwa njia ya utendaji. Vyombo hutegemeana na kushirikiana.
MIUNDO YAKE: CHAMA SERIKALI
- Jumuiya ya Wananchi - Wizara za Serikali
- Viongozi - Idara za Wizara
- Wanachama - Mashirika
- Wananchi - Raia

VIKAO VYA CHAMA:
Vikao ambavyo ndivyo msingi au chemichemi ya demokrasi ni vya muhimu sana kutokana na maamuzi yake. Maamuzi ya ngazi ya juu yanatekelezwa na vikao vyote vya ngazi ya chini kwa muda unaotakiwa.
Katika shughuli za chama maoni ya walio wengi yanatiliwa mkazo mradi yanasimamia maslahi ya Chama na kwamba maoni ya wachache hayapuuzwi.
Katika Chama si uamuzi peke yake ni lazima uamuzi wa vikao uwe ni sahihi kiitikadi na uwe na maslahi na msimamo wa Chama kisiasa kuzingatia maazimio ya vikao vya juu na chini.
Uongozi/Menejimenti, Utendaji wa Kamati, Halmashauri kuu na Mkutano Mkuu, toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa, licha ya shina au usimamizi wa kikundi.

KUIMARISHA CHAMA KWA KUIMARISHA UONGOZI:
i. Msimamo wa kijamaa, mzalendo, mwenye maadili ya itikadi.
ii. Vitendo na tabia yake idhihirishwe kwa anaowaongoza wanachama na wananchi kuwa ni kijamaa.
iii. Imani ya kiongozi inaambukiza na kuimarisha imani ya kuwaongoza.
iv. Msimamo thabiti wa ujamaa wa kiongozi ni budi uambatane na uwezo wa kuongoza kwa kuelewa, kueleza, kushauri, kushawishi na shirikisha.
v. Si mnafiki wala wa kuyumbayumba na mkweli.
vi. Umoja na uongozi wa pamoja ni silaha kuu ya ufanisi wa maendeleo ya binadamu.

KUIMARISHA UONGOZI WA CHAMA KATIKA SEHEMU ZA KAZI:
Wakuu wa kazi waweke msimamo wa kazi za kizalendo utakaoimarisha uwezo wao wa kitaalamu. Suala la kwanza ni kuleta mafanikio ya utekelezaji wa kazi. Wanachama na viongozi wawe mstari wa mbele kwa kutimiza wajibu wao wa kazi na kuona malengo yaliyowekwa yanafanikiwa.

Kuandaa Makada wa Chama kwa mafunzo na semina zenye malengo ya kupiga vita upotoshaji na uzushi juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea katika Taasisi maalumu za wananchi, wanafunzi, majeshi, wafanyakazi, vijana, wanawake na wana utamaduni. Waandishi wa habari, kuwahamasisha ili kuinua mwamko wao. Kuwapa mwelekeo na msimamo wa kisiasa na wa uchumi wa kijamaa.

Maandalizi ya waomba uanachama na uongozi yapimwe. Chama ni Vikao, wajumbe na watendaji wa kuchaguliwa kusimamia maazimio ya vikao kama Secretariet ilivyo. Kujikosoa na kukosoana ni silaha ya kimapinduzi kwa kusema kweli, kukubali kujirekebisha na vikao kuweka utaratibu wa kujikosoa.

Kuimarisha Chama ni pamoja na kudhibiti fedha, kutoa michango na kutafuta njia nyingine za kudumu katika kuimarisha chama na jumuiya zake.
Uharibifu na kutumia vibaya vyombo vya kazi na mali ya umma kama vile magari, mashine na zana nyinginezo muhimu si vizuri.

II. UONGOZI NA UTAWALA (MENEJIMENTI)
Maneno haya yanaenda kwa kima kimoja, maana kazi ya uongozi na utawala zinatimiza kusudi moja ambalo ni Taifa. Mgawanyiko unatokana na utendaji wa majukumu yake ndiyo kuhitirafiana kwa mbinu na nyenzo zake kama:-
Chama - Kauli au sura yake ni tufanyeje? mwaonaje? huwa uongozi wa pamoja kwa maamuzi ya umma ambayo ndiyo Demokrasia halisi ya kujadili, kuazimia na kusimamia.

Serikali - Kauli yake Njoo hapa, Nenda pale, Fanya hivi, Naona hivi. Uwezo wa vyombo vya madola nguvu na mabavu kama Mahakama na Majeshi yote.
- Uongozi: Huzaa viongozi na
- Utawala: Huzaa watawala.
Kama ndivyo napenda tuone sura ya upande mmoja wa shilingi yaani uongozi kwa undani zaidi.

III. VIONGOZI
Viongozi wanapatikana kwa njia kuu nne zifuatazo:-
- Kujifunza - Wataalamu
- Kuchaguliwa - Kupigiwa kura
- Kuteuliwa - Mwenye madaraka
- Kurithi - Ufalme – Utemi

IV. AINA AU MITINDO YA UONGOZI:
Kuna aina kama nne hivi za uongozi, nazo ni kama zifuatazo:-

i. Uongozi wa mabavu (Autocratic Leadership)
Uongozi wa aina hii kiongozi hujiona kwamba ni yeye tu ndiye ajuaye kila kitu. Hasikilizi wala haombi mawazo au mawaidha kutoka kwa walio chini yake. Maamuzi yote hufanywa naye. Yeye ni mtu wa kutoa amri na maelekezo tu. Hajali mawazo na fikira za mwenzake.

ii. Uongozi Huria (Laissez faire Leadership)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hutoa ruksa kubwa kwa watu wake wawe huru kufanya watakavyo. Huchukulia juu juu tu mambo ya uongozi wake. “Iwe hivyo”, huwa ndiyo hulka ya uongozi wake. Hatoi miongozo wala amri zenye uzito kwa walio chini yake.


iii. Uongozi wa Kidemokrasia (Democratic Leadership)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hujali sana na huamini watu wake, hutoa miongozo lakini wakati huo huo husikiliza na kutilia maanani mawazo na mapendekezo ya wengine. Huwahusisha wote wanaohusika katika kutoa uamuzi na kutafuta mbinu mbalimbali za kutatulia/kutekeleza shughuli za ofisi. Isitoshe, kiongozi wa aina hii hujali sana matatizo ya walio chini yake.

iv. Uongozi wa Urasimu (Bureaucratic)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hujali na kufuata sana tena sana misingi, kanuni na milolongo ya taratatibu zinazotawala utendaji wa kazi za ofisini. Huhakikisha kwamba kila kitu hakina budi kufanywa kwa kufuatana na kanuni zilizowekwa . Urasimu haupendi mabadiliko ya mara kwa mara.

V. WAJIBU MKUBWA WA KIONGOZI
- Kubuni mipango ya maendeleo
- Kusimamia mipango na shughuli zilizopangwa
- Kushawishi waongozwa katika shughuli za maendeleo
- Kuongoza vikao kwa mujibu wa katiba au miongozo
- Kuwakilisha wenzake katika vikao mbalimbali
- Kuwa mzungumzaji kwa niaba ya chama au anaowaongoza



VI. MIIKO YA KIONGOZI:
- Kutumia madaraka cheo kwa faida yake.
- Kupokea na kutoa hongo.
- kuwa na Majivuno - sifa.
- Kudhulumu au kutotoa haki
- Kuiba mali ya umma (ubadhilifu)
- Kutokuwa na msimamo (kigeugeu)

VII. HAKI ZA KIONGOZI
- Kuongoza - kauli - sauti.
- Heshima - hadhi.
- Maslahi - marupurupu.
- Motisha na vivutio.
- Kutambuliwa -kukubalika

VIII. SIFA ZA KIONGOZI BORA
- Mwenye utu na heshima
- Muelewa
- Mwenye kushirikiana
- Mweye vitendo (mbunifu na mchapakazi)
- Mwenye tabia nzuri
- Mwaminifu
- Aliye mstari wa mbele
- Mwenye ushawishi
IX. KANUNI ZA MENEJIMENT
Mtaalamu wa Menejiment Mfaransa aitwaye Henri Fayol (1841-1925) alipendekeza kanuni za Management 14 kama ifuatavyo:-

1. Mgawanyo wa kazi.
Kila mfanyakazi afanye kazi katika eneo la ujuzi au utaalamu wake.

2. Madaraka na wajibu.
Kila mfanyakazi apewe madaraka yanayolingana na wajibu wake na yaelezwe waziwazi.

3. Nidnamu
Kila mtumishi anapaswa kutii yale yaliyokubalika. Uvunjaji wowote usivumiliwe.

4. Amri moja.
Mfanyakazi awajibike mahala pamoja ambapo anapewa maagizo ya kufanya.

5. Uelekeo mmoja
Ili kufikia lengo kila mtumishi na idara zote zinapaswa kufikiria katika uelekeo mmoja kufikia kusudi moja kuu. Hii ina msisitizo katika maono au dhima ya shirika, umoja au chama au taasisi.

6. Matakwa ya pamoja
Makusudi ya mtumishi binafsi na idara au wizara binafsi kamwe yasipewe nafasi kupinga matakwa na makusudi ya pamoja. Matakwa ya pamoja yapewe kipaumbele.

7. Malipo ya haki.
Malipo - pawe na misingi inayoeleweka katika malipo. Malipo kama mshahara na marupurupu mengine yalipwe bila upendeleo.

8. Msongamano wa madaraka.
Madaraka na mamlaka yawekwe sehemu moja. Na wengine wapokee maagizo ya kutililika toka hapo ili kuondoa mikanganyiko na kuleta mfanano katka maendeleo.

9. Mtiririko wa mamlaka
Kazini pawepo na ngazi za kiutawala ambazo huelekeza mtiririko wa mamlaka na amri zitolewazo.

10. Uwepo wa utaratibu.
Sehemu ya kazi lazima pawepo utaratibu au mipango maalum na watu pamoja na vitu vya kufanyia kazi. Kila kitu au mtu awe sehemu inayotakiwa kwa wakati kuafaka.

11. Pawepo na ubinadamu kazini (usawa)
Pawepo hali ya ubinadamu kazini kama vile huruma, kutopendelea, kutokuwa na chuki, uonevu, dharau na dhuluma.

12. Muda wa ajira
Watumishi wazuri waruhusiwe kutumika muda wao wote

13. Kila mtu apewe nafasi.
Kila mtu yaani mfanyakazi apewe nafasi ya kuendeleza kipaji chake katka kazi aliyonayo au ujuzi au utaalamu wake

14. Umoja na ushirikiano.
Pawepo na uhusiano na amani katika kazi maana yake kila mfanyakazi au kazi hutegemea umoja ni nguvu.