Wednesday, January 2, 2008

UONGOZI NA UTAWALA KATIKA CHAMA NA SERIKALI


Moja ya makala nyingi zilizoandikwa na Mutaragara



I. UTANGULIZI- TAIFA LENYEWE LILIVYO
Taifa ni watu au raia wa nchi hiyo kutokana na asili ya kuzaliwa au kuandikishwa uraia na uzalendo wa kuishi kwao. Taifa lina vyombo viwili ambavyo kwavyo majukumu mbalimbali hutekelezwa yaani Chama na Serikali (Utawala, Bunge na Vyombo vya mahakama na polisi).

CHAMA:
Kinazaa uongozi na kazi yake kuu ni kushika hatamu za uongozi wa kuweka sera, kuzisimamia na kuweka umbile la Serikali kwa kudhibiti utekelezaji wake.

SERIKALI:
Inazaa utawala, inatekeleza majukumu ya Taifa kwa kusimamia sheria zinazoundwa na Bunge lake na kulinda nchi kufuatia Katiba na taratibu zilizowekwa.

MAANA YA CHAMA:
Chama ni umoja wa watu waliojiunga pamoja ili kutimiza lengo, kusudi shabaha fulani. Kuna aina nyingi za vyama ambavyo vimegawanyika katika mafungu matano:-
i. Kidini - Uzima wa milele
ii. Kisiasa - Uhuru na kuweka sera
iii. Kiuchumi - Uzalishaji na faida
iv. Kiutamaduni - Michezo na burudani
v. Kijamii - Huduma mbalimbali

KAZI YA CHAMA:
- Kusimamia, kulinda, kutetea –Imani au shabaha yake.
- Kueneza, kukuza malengo, shabaha yake.
- Kulinda haki na hadhi ya wafuasi wake.
- Kuweka malengo, mipango, umbile la chama
- Kuweka ushirikiano, umoja kati yao.

CHAMA CHA KISIASA:
Ni cha watu wote Wakulima, Wavuvi, Wafugaji, Wafanya biashara, Wafanyakazi n.k. Ni mtetezi wa Umma dhidi ya uonevu, dhuluma na vitendo vyovyote vinavyonyima wananchi haki zao za kuwa raia huru katika nchi yao wenyewe. Chama ndicho kinajenga Ujamaa ili kutimiza demokrasi ambayo inaonekana katika vikao kutokana na maamuzi yake.

KAZI ZAKE:
Chama kinashika hatamu za uongozi wa kuweka umbile la Serikali na malengo yake. [Kuongoza ni kuonyesha njia]. Serikali inatekeleza malengo yaliyowekwa na Chama kwa njia ya utendaji. Vyombo hutegemeana na kushirikiana.
MIUNDO YAKE: CHAMA SERIKALI
- Jumuiya ya Wananchi - Wizara za Serikali
- Viongozi - Idara za Wizara
- Wanachama - Mashirika
- Wananchi - Raia

VIKAO VYA CHAMA:
Vikao ambavyo ndivyo msingi au chemichemi ya demokrasi ni vya muhimu sana kutokana na maamuzi yake. Maamuzi ya ngazi ya juu yanatekelezwa na vikao vyote vya ngazi ya chini kwa muda unaotakiwa.
Katika shughuli za chama maoni ya walio wengi yanatiliwa mkazo mradi yanasimamia maslahi ya Chama na kwamba maoni ya wachache hayapuuzwi.
Katika Chama si uamuzi peke yake ni lazima uamuzi wa vikao uwe ni sahihi kiitikadi na uwe na maslahi na msimamo wa Chama kisiasa kuzingatia maazimio ya vikao vya juu na chini.
Uongozi/Menejimenti, Utendaji wa Kamati, Halmashauri kuu na Mkutano Mkuu, toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa, licha ya shina au usimamizi wa kikundi.

KUIMARISHA CHAMA KWA KUIMARISHA UONGOZI:
i. Msimamo wa kijamaa, mzalendo, mwenye maadili ya itikadi.
ii. Vitendo na tabia yake idhihirishwe kwa anaowaongoza wanachama na wananchi kuwa ni kijamaa.
iii. Imani ya kiongozi inaambukiza na kuimarisha imani ya kuwaongoza.
iv. Msimamo thabiti wa ujamaa wa kiongozi ni budi uambatane na uwezo wa kuongoza kwa kuelewa, kueleza, kushauri, kushawishi na shirikisha.
v. Si mnafiki wala wa kuyumbayumba na mkweli.
vi. Umoja na uongozi wa pamoja ni silaha kuu ya ufanisi wa maendeleo ya binadamu.

KUIMARISHA UONGOZI WA CHAMA KATIKA SEHEMU ZA KAZI:
Wakuu wa kazi waweke msimamo wa kazi za kizalendo utakaoimarisha uwezo wao wa kitaalamu. Suala la kwanza ni kuleta mafanikio ya utekelezaji wa kazi. Wanachama na viongozi wawe mstari wa mbele kwa kutimiza wajibu wao wa kazi na kuona malengo yaliyowekwa yanafanikiwa.

Kuandaa Makada wa Chama kwa mafunzo na semina zenye malengo ya kupiga vita upotoshaji na uzushi juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea katika Taasisi maalumu za wananchi, wanafunzi, majeshi, wafanyakazi, vijana, wanawake na wana utamaduni. Waandishi wa habari, kuwahamasisha ili kuinua mwamko wao. Kuwapa mwelekeo na msimamo wa kisiasa na wa uchumi wa kijamaa.

Maandalizi ya waomba uanachama na uongozi yapimwe. Chama ni Vikao, wajumbe na watendaji wa kuchaguliwa kusimamia maazimio ya vikao kama Secretariet ilivyo. Kujikosoa na kukosoana ni silaha ya kimapinduzi kwa kusema kweli, kukubali kujirekebisha na vikao kuweka utaratibu wa kujikosoa.

Kuimarisha Chama ni pamoja na kudhibiti fedha, kutoa michango na kutafuta njia nyingine za kudumu katika kuimarisha chama na jumuiya zake.
Uharibifu na kutumia vibaya vyombo vya kazi na mali ya umma kama vile magari, mashine na zana nyinginezo muhimu si vizuri.

II. UONGOZI NA UTAWALA (MENEJIMENTI)
Maneno haya yanaenda kwa kima kimoja, maana kazi ya uongozi na utawala zinatimiza kusudi moja ambalo ni Taifa. Mgawanyiko unatokana na utendaji wa majukumu yake ndiyo kuhitirafiana kwa mbinu na nyenzo zake kama:-
Chama - Kauli au sura yake ni tufanyeje? mwaonaje? huwa uongozi wa pamoja kwa maamuzi ya umma ambayo ndiyo Demokrasia halisi ya kujadili, kuazimia na kusimamia.

Serikali - Kauli yake Njoo hapa, Nenda pale, Fanya hivi, Naona hivi. Uwezo wa vyombo vya madola nguvu na mabavu kama Mahakama na Majeshi yote.
- Uongozi: Huzaa viongozi na
- Utawala: Huzaa watawala.
Kama ndivyo napenda tuone sura ya upande mmoja wa shilingi yaani uongozi kwa undani zaidi.

III. VIONGOZI
Viongozi wanapatikana kwa njia kuu nne zifuatazo:-
- Kujifunza - Wataalamu
- Kuchaguliwa - Kupigiwa kura
- Kuteuliwa - Mwenye madaraka
- Kurithi - Ufalme – Utemi

IV. AINA AU MITINDO YA UONGOZI:
Kuna aina kama nne hivi za uongozi, nazo ni kama zifuatazo:-

i. Uongozi wa mabavu (Autocratic Leadership)
Uongozi wa aina hii kiongozi hujiona kwamba ni yeye tu ndiye ajuaye kila kitu. Hasikilizi wala haombi mawazo au mawaidha kutoka kwa walio chini yake. Maamuzi yote hufanywa naye. Yeye ni mtu wa kutoa amri na maelekezo tu. Hajali mawazo na fikira za mwenzake.

ii. Uongozi Huria (Laissez faire Leadership)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hutoa ruksa kubwa kwa watu wake wawe huru kufanya watakavyo. Huchukulia juu juu tu mambo ya uongozi wake. “Iwe hivyo”, huwa ndiyo hulka ya uongozi wake. Hatoi miongozo wala amri zenye uzito kwa walio chini yake.


iii. Uongozi wa Kidemokrasia (Democratic Leadership)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hujali sana na huamini watu wake, hutoa miongozo lakini wakati huo huo husikiliza na kutilia maanani mawazo na mapendekezo ya wengine. Huwahusisha wote wanaohusika katika kutoa uamuzi na kutafuta mbinu mbalimbali za kutatulia/kutekeleza shughuli za ofisi. Isitoshe, kiongozi wa aina hii hujali sana matatizo ya walio chini yake.

iv. Uongozi wa Urasimu (Bureaucratic)
Uongozi wa aina hii, kiongozi hujali na kufuata sana tena sana misingi, kanuni na milolongo ya taratatibu zinazotawala utendaji wa kazi za ofisini. Huhakikisha kwamba kila kitu hakina budi kufanywa kwa kufuatana na kanuni zilizowekwa . Urasimu haupendi mabadiliko ya mara kwa mara.

V. WAJIBU MKUBWA WA KIONGOZI
- Kubuni mipango ya maendeleo
- Kusimamia mipango na shughuli zilizopangwa
- Kushawishi waongozwa katika shughuli za maendeleo
- Kuongoza vikao kwa mujibu wa katiba au miongozo
- Kuwakilisha wenzake katika vikao mbalimbali
- Kuwa mzungumzaji kwa niaba ya chama au anaowaongoza



VI. MIIKO YA KIONGOZI:
- Kutumia madaraka cheo kwa faida yake.
- Kupokea na kutoa hongo.
- kuwa na Majivuno - sifa.
- Kudhulumu au kutotoa haki
- Kuiba mali ya umma (ubadhilifu)
- Kutokuwa na msimamo (kigeugeu)

VII. HAKI ZA KIONGOZI
- Kuongoza - kauli - sauti.
- Heshima - hadhi.
- Maslahi - marupurupu.
- Motisha na vivutio.
- Kutambuliwa -kukubalika

VIII. SIFA ZA KIONGOZI BORA
- Mwenye utu na heshima
- Muelewa
- Mwenye kushirikiana
- Mweye vitendo (mbunifu na mchapakazi)
- Mwenye tabia nzuri
- Mwaminifu
- Aliye mstari wa mbele
- Mwenye ushawishi
IX. KANUNI ZA MENEJIMENT
Mtaalamu wa Menejiment Mfaransa aitwaye Henri Fayol (1841-1925) alipendekeza kanuni za Management 14 kama ifuatavyo:-

1. Mgawanyo wa kazi.
Kila mfanyakazi afanye kazi katika eneo la ujuzi au utaalamu wake.

2. Madaraka na wajibu.
Kila mfanyakazi apewe madaraka yanayolingana na wajibu wake na yaelezwe waziwazi.

3. Nidnamu
Kila mtumishi anapaswa kutii yale yaliyokubalika. Uvunjaji wowote usivumiliwe.

4. Amri moja.
Mfanyakazi awajibike mahala pamoja ambapo anapewa maagizo ya kufanya.

5. Uelekeo mmoja
Ili kufikia lengo kila mtumishi na idara zote zinapaswa kufikiria katika uelekeo mmoja kufikia kusudi moja kuu. Hii ina msisitizo katika maono au dhima ya shirika, umoja au chama au taasisi.

6. Matakwa ya pamoja
Makusudi ya mtumishi binafsi na idara au wizara binafsi kamwe yasipewe nafasi kupinga matakwa na makusudi ya pamoja. Matakwa ya pamoja yapewe kipaumbele.

7. Malipo ya haki.
Malipo - pawe na misingi inayoeleweka katika malipo. Malipo kama mshahara na marupurupu mengine yalipwe bila upendeleo.

8. Msongamano wa madaraka.
Madaraka na mamlaka yawekwe sehemu moja. Na wengine wapokee maagizo ya kutililika toka hapo ili kuondoa mikanganyiko na kuleta mfanano katka maendeleo.

9. Mtiririko wa mamlaka
Kazini pawepo na ngazi za kiutawala ambazo huelekeza mtiririko wa mamlaka na amri zitolewazo.

10. Uwepo wa utaratibu.
Sehemu ya kazi lazima pawepo utaratibu au mipango maalum na watu pamoja na vitu vya kufanyia kazi. Kila kitu au mtu awe sehemu inayotakiwa kwa wakati kuafaka.

11. Pawepo na ubinadamu kazini (usawa)
Pawepo hali ya ubinadamu kazini kama vile huruma, kutopendelea, kutokuwa na chuki, uonevu, dharau na dhuluma.

12. Muda wa ajira
Watumishi wazuri waruhusiwe kutumika muda wao wote

13. Kila mtu apewe nafasi.
Kila mtu yaani mfanyakazi apewe nafasi ya kuendeleza kipaji chake katka kazi aliyonayo au ujuzi au utaalamu wake

14. Umoja na ushirikiano.
Pawepo na uhusiano na amani katika kazi maana yake kila mfanyakazi au kazi hutegemea umoja ni nguvu.

1 comment:

Anonymous said...

Laiti kama wanasiasa wetu leo wangefuata misingi na uelewa huu basi tungekuwa na maendeleo makubwa sana!