Thursday, January 3, 2008

KUMBUKUMBU ZA MWAKA MMOJA JUU YA MAISHA YA MZEE CHIRANGI
KIUMBE HADIMU AMBAYE JAPO AMEKUFA SAUTI YAKE NA MATENDO YAKE YANAENDELEA KUTOA CHANGAMOTO CHANYA KATIKA MAISHA YETU WANAMARA NA TAIFA ZIMA KWA UJUMLA.

Hakutoka katika familia maarufu wala hakuwa na mali nyingi na elimu yake ilikuwa tu ya wastani. Hata hivyo ukithubutu kunyambulisha mitizamo, misimamo na matendo yake waweza kubaini kuwa upatikanaji wa viumbe wenye matendo sanjari na kauli mbiu ya ‘HAKI HUINUA TAIFA’ ni adimu katika ulimwengu wa leo.

Siku kama ya leo, mwaka mmoja uliopita makucha ya kifo pasipo huruma wala taarifa yalituondolea pumzi ya uhai Mzee wetu


Amos Mutaragara Chirangi wa Muhongo wa Nyawayega wa Rihu- Omumbogo wa Kumusoma gwa Nyambita..

Marehemu mzee Chirangi aliyezaliwa mwaka 1932 huko Bushora Mwirengo Mugango, Mkoani Mara aliacha alama za kishujaa kama Kiongozi, Mzalendo na Muumini wa kuigwa katika kizazi hiki na vijavyo.

Familia ya Chirangi inawashukuru sana wananchi wote wa Mkoa wa Mara na kwingineko, Serikali yetu, Jumuiya zote za Kidini, CCM na Vyama vyote vya siasa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi na Asasi mbalimbali za kijamii kwa Faraja, Misaada mbalimbali, Umoja na Mshikamano wao waliotuonyesha wakati wa msiba hadi huduma za mazishi za marehemu baba yetu Mutaragara Chirangi. Ni bayana kuwa hakuna chombo chochote cha habari wala mtunzi wala hifadhi ya makumbusho inayoweza kwa ukamilifu kutuhabarisha juu ya wasifu wa marehemu mzee Chirangi. Hata hivyo kweli isiyofichika huchomoza popote ikitukumbusha machache tu ya utu na utumishi wake kwa wanadamu. Kila mwaka familia yake itakuwa inaainisha dhamira moja kuu ambayo inaakisi moja ya sifa zake kama changamoto kwetu. Mwaka huu tunaanza na sifa yake ya UWEKAJI MIPANGO (Planning):-

Kila kitu chake alitaka kiwe kimeandaliwa barabara kwa wakati muafaka na kwa kiwango kinachoridhisha hivyo akaitwa ‘mzee wa Standard’. Ni mzee aliyepinga kwa vitendo uongozi na maisha ya uzima moto, ndiposa tulishuhudia hata akiwa amejiandalia Wosia kwa familia na kaburi lake mwenyewe sio kwa udhoofu wa afya yake bali kwa msingi wa kujiandaa na kutotaka kusababisha usumbufu wowote kwa jamii wakati anajua kuwa kauli ya Mungu pale Edeni kuwa ‘hakika mtakufa’ ni ya kweli na kwamba ilimuhusu pia hata na yeye.
Ni mzee aliyekuwa rafiki wa karibu wa nyenzo KALENDA si kwa sababu ya kujua jinsi siku zinavyokwenda bali zaidi kujipanga katika siku zinavyokuja.
Tunapoanza mwaka mpya 2008 sauti ya mzee Chirangi inatuasa sote kuwa tuwe watu wa mipango na utekelezaji. Tuweke mipango yetu ya muda mfupi na mrefu popote tulipo iwe ni katika familia, au katika Chama au Taasisi au Kampuni au Usharika, au Jumuiya yeyote kwa ajili ya maendeleo yetu. Maana ni kweli kuwa usipojua unapoelekea kamwe huwezi kupotea maana popote utakapokuwa utafikiri kuwa umefika.

“ Busara zako, utu wako na hekima zako ni hazina kubwa sana sio kwa familia yako tu bali kwetu sisi sote” Mgeni namba. 228 wa Mzee Chirangi. Mh. H. N. Ole – Mkuu wa Wilaya Musoma, Aug. 2001.

KWA HESHIMA NA SHUKRANI, FAMILIA YA CHIRANGI INAWASILISHA.
Prof. Dr. Sospeter Muhongo
Mdogowe Mzee Mutaragara

3 comments:

Anonymous said...

Mzee wa kazi, mzee wa haki, mzee aliyefit kila alipopewa uongozi.
Mungu ailaze pema peponi roho yake.

Alhaji Hussein

Anonymous said...

ndio maana huyu mzee alipendwa sana na nyerere

Anonymous said...

mimi namkumbuka sana kwa kupenda michezo. kipindi chake kama Mwenyekiti wa FAT(M). Mara Stars ilikuwa tishio uliza wachezaji wa enzi hizo wa mzizima watakwambia. Aliwahi kuwa mdhamini wa FAT Taifa kwa muda mrefu sana.