Wednesday, January 2, 2008

HOTUBA YA A.M. CHIRANGI - MWENYEKITI WA CCM WILAYA YA MUSOMA MJINI KWENYE MKUTANO MKUU WA CCM WILAYA YA MUSOMA MJINI - AGOSTI 1997.

Baada ya kutoa huduma kwa miaka 15 mfululizo, ebu msome kiongozi huyu anavyohutubu.


I. UTANGULIZI

A) SALAAM NA SHABAHA YA HOTUBA

Ndugu wasimamizi wa uchaguzi, ndugu wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM (W), ndugu wageni waalikwa, mabibi na mabwana. Awali ya yote ninapenda wasalimuni nyote na kuwakaribisheni kushiriki vema na kikamilifu katika kikao hiki cha Chama Wilayani Musoma Mjini.

Hotuba hii inakusudia kuwapeni picha halisi ya maendeleo ya Wilaya yetu kwa mtazamo wa Chama cha Mapinduzi na nasaha zangu binafsi kwa Chama na Serikali baada ya kuwatumikieni katika dhamana mliyonienzi kwa muda wa takribani, miaka kumi na mitano (1982 - 1997).

B) PONGEZI NA MAELEKEZO YA KAZI KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU WA CCM (W)
Ninachukua wasaa huu kwa moyo wa dhati pasipo husuda, wala uzandiki kuwapongezeni wale wote mliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano huu wa viongozi wa Chama katika ngazi za matawi na kata kwa kipindi cha 1997 – 2002 na pia kwa wale wote ambao majina yenu yamepitisha kugombea nafasi mbalimbali za Chama Wilayani, Mkoani hadi Taifa, dhamira na makusudio yenu katika kukitumia Chama ziendelee kwa kadri ya majukumu na nafasi zetu pasipo uvunjaji wowote wa miiko na maadili ya uongozi. Sote tunapaswa kuyaeneza matunda ya uhuru kwa wananchi wote kwa manufaa yao na maendeleo ya Taifa zima kwa ujumla.

Wajumbe wa kikao hiki pamoja na kazi nyingne zote mtakazokuwa nazo, mtapaswa kutoa maelekezo ya utekelezaji wa sera ya CCM kwa kipindi kijacho kutokana na taarifa ya kazi iliyotolewa na Halmashuri Kuu ya CCM Wilaya.

Aidha mtahakikisha kuwa maazimio na maagizo ya vikao vya ngazi za juu yanatekelezwa kwa maendeleo ya wilaya yetu na Taifa letu kwa ujumla.
Mtayazungumzia mambo yote yahusuyo: “Ulinzi, Usalama na Maendeleo ya Wilaya Musoma Mjini, mtaunda Kamati za Mkutano Mkuu wa CCM (W) kwa kadri itakavyofaa na zaidi ya yote mtashiriki katika Uchaguzi huru na wa haki kuwachagua:-
Mwenyekiti wa CCM (W), Wajumbe kumi kuingia Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, Wajumbe watano kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM-Taifa.
Ni mategemeo yangu kuwa mtatumia vizuri haki hiyo mliyonayo kuwasimika watu wenye stahili na moyo wa kuitumikia CCM, pasipo upendeleo.



C) SERA YA CCM
Ni bayana kuwa maendeleo ya Serikali ya chama cha Mapinduzi yanaendelea kupimwa na Watanzania wote kwa mizani iliyojiwekea yenyewe. Hii ndiyo sera ya CCM kama ilivyofafanuliwa katika ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Taifa ya CCM ya Oktoba 1995.

Ndugu viongozi, sote tunapaswa kuelekeza nia, nguvu, raslimali, ujuzi na uzoefu wetu wote katika mwelekeo wa ilani hiyo kwa kipindi chote cha 1995 - 2002.

Yafuatayo ndiyo maeneo muhimu ya kuzingatia ili CCM iendelee kupata ridhaa ya wananchi wengi zaidi wa Tanzania na hivyo kuiwezesha kuongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi kijacho cha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000, na hatimaye katika kuwafikisha Watanzania kwenye Mapinduzi ya kweli na kuendeleza mapambano dhidi ya aina zote za unyonyaji, udhalilishaji, udhoofishaji na uzoroteshaji wa maisha na uchumi wa Taifa letu.

i) Kutumia sayansi na teknolojia katika uchumi.
ii) Kuimarisha kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa.
iii) Kuimarisha na kuendeleza viwanda vyetu, mashirika ya Umma machache yenye faida na kukuza biashara.
iv) Kuhimiza matumizi bora ya maliasili, kukuza utalii na kuhifadhi mazingira.
v) Kuendeleza uchimbaji madini na kupanua sekta ya nishati.
vi) Kuimarisha sekta ya mawasiliano na uchukuzi.
vii) Kuboresha na kupanua huduma za jamii hususani elimu, afya, maji na nyumba.
viii) Kuimarisha na kuzienzi fani za michezo na sanaa.
ix) Kuongoza kwa kufuata kanuni za Menejiment, biashara na kujitegemea katika kuliinua pato la Taifa.
x) Kuzingatia nafasi, haki na wajibu wa wafanyakazi, vijana, wanawake na walemevu katika jamii yetu.
xi) Kuimarisha ulinzi na usalama.
xii) Kuboresha uhusiano wetu na nchi za nje.
xiii) Kudumisha ushirikiano na umoja. Kudumisha Muungano kati ya Tanzania Bara na visiwani.
xiv) Kuimarisha Chama.

II. MIZANIA YA KAZI ZA CCM (W) KWA KIPINDI CHA 1992 – 1997
Ndugu Wajumbe, siyo kazi rahisi kuandaa mizania ya mahesabu ya taasisi au kampuni fulani. Kwa kuwa kabla ya kufanya hivyo wataalam hukamilisha kwanza kazi ya Kuorodhesha mali, wadai na wadeni katika kipindi husika.

Ili kuweza kuonyesha uwiano wa hasi na chanya. Sawia na mfano huo; tunawajibika kuorodhesha mafanikio na matatizo yote yaliyojitokeza kwa kipindi husika. Sikusudii kutoa taarifa ya kazi ya CCM, bali ninadodosa machache yake niliyoyaona muhimu katika kipindi changu cha uongozi. Jinsi yalivyoathiri maendeleo yetu na ikiwezekana mapendekezo yangu:-

i. Uanachama
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka huu 1997 tunao wanachama wa CCM 6262 ikilinganishwa na wanachama 7061 waliokuwepo mwaka 1992 kabla ya kuyafunga matawi ya sehemu za kazi na majeshi.

Hata hivyo, uchunguzi wa kina unaonyesha kuwa uhai wa wanachama waliopo hauridhishi sana hususan baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

ii. Vikao vya Chama 1997
Suala la vikao kwa mujibu wa Katiba limetekelezwa kwa kiwango kikubwa. Hasa katika ngazi ya Wilaya na chini ya wastani katika ngazi nyingine kama ifuatavyo kwa mwaka 1997:-

NGAZI YA VIKAO
ASILIMIA YA LENGO
Vikao vya Kamati ya siasa
Vimefanyika mara saba =>100%
Vikao vya Halmashauri
mara tatu =>100%
Vikao vya Mkutano Mkuu
Mara mbili =>100%

iii. Mashina na matawi ya CCM
1987, kulikuwa na jumla ya mashina 550 ya CCM mwaka huu 1997, idadi ya mashina imeogezeka na kufikia 808. Mwaka 1987, kulikuwa na jumla ya matawi arobaini na tatu (43). 30 yalikuwa ya sehemu za kazi na 13 ya mitaani. Mwaka jana (1996) tulikuwa na jumla ya matawi 56, katika kata 3.

iv. Jumuiya za Chama 1997
Wilaya inazo Jumuiya tatu (3), yaani; vijana, wazazi na Wanawake zinazoongozwa na Chama. Kwa ujumla Jumuiya hizi zina maendeleo ya wastani tu.
Kazi kubwa ambazo zimeweza kufanywa na Jumuiya hizo ni kama vile:-
1. Kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM na kuunda matawi mapya.
2. Kutoa hamasa kwa Umma juu ya umuhimu wa Elimu na ujenzi wa mashule.
3. Kuunga mkono kwa dhati CCM katika chaguzi mbalimbali za Serikali.




v. Michango
Tangu mwanzo wa kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi vya siasa, kumekuwepo na kuteremka kwa kiwango cha utoaji michango ya hiari na ya wajibu. Ni vema tuendelee kuelimisha, kushawishi na kuhimiza wanachama. Ili wawe wote wakilipa ada zao na kutoa michango inayowahusu. Ni muhimu zaidi kukusanya, kuzitunza na kuzitumia fedha zinazopatikana kwa kufuata kanuni za fedha kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CCM.

vi. Elimu
a) Elimu kwa Wanachama Ni bayana kwamba CCM irejeshe Idara au kitengo maalum kinachoshughulikia suala la Elimu na mafunzo kwa viongozi na wanachama wote wa CCM, ili kuwajenga na kuwaimarisha, kwa maana pasipo hilo tutaendelea kujenga Chama chenye wanachama wenye ufahamu finyu kichama, kisiasa na hata kiitikadi, kwa sasa inatolewa kwa kiwango cha chini.


b) Elimu kwa wote. Katika kipindi cha 1992 - 1997, tumeweza kusimama kidete, kuimarisha elimu wilayani. Ogezeko la idadi ni ushahidi kamili:
Pamoja na juhudi hizo, bado Wilaya inahitaji kuongeza au kukamilisha baadhi ya Madarasa na madawati. Na kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhusu kuwaandikisha watoto wao wenye umri wa kwenda shule. Tunayashukuru mashirika binafsi mfano madhehebu mbalimbali ya dini kwa kuanzisha shule za chekechea (Kindergarten Schools). Shule hizi ndizo msingi madhubuti kwa elimu ya juu.

vii. Ulinzi na Usalama
Kwa wastani, kumekuwa na hali ya utulivu na amani katika Wilaya yetu. Jukumu zima la ulinzi na usalama limeelekezwa kwa wananchi wenyewe zaidi kuliko kuiachia dola na vyombo vya usalama pekee.

Mashauri mbalimbali yaliyoendeshwa chini ya mabaaraza ya jadi yamemalizika mapema na haki kuonekena kutendwa, kwa pande zote: yaani walalamikaji na walalamikiwa. Kinyume chake, kumekuwa na malalamiko kadhaa ya wananchi juu ya kucheleweshwa kwa mashauri katika Mahakama hususani Mahakama ya mwanzo.

Tunaipongeza pia idara ya uhamiaji, kwa kazi yake nzuri ya kusimamia na kulinda taratibu za watu waingiao na watokao nchini.

viii. Afya
Mada hii inaangaliwa katika uwanja mpana kutokana na maana halisi ya neno Afya kama lilivyoainishwa na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linalosisitiza; ‘Ukamilifu wa hali ya mtu na jamii kwa ujumla, kimwili, kiakili na hata kisaikolojia. Na kwamba haimaanishi kutokuwepo kwa maradhi au ulemavu pekee’.

a. Huduma za afya bado hazijitoshelezi katika Wilaya. Hii ni kutokana na ukosefu wa chakula, madawa na vitendea kazi hususani, katika Hospitali yetu ya Mkoa na hata kituo chetu cha huduma za kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano cha Nyasho (MCH – Clinic). Aidha zahanati za watu binafsi na maduka ya dawa mengi yametakiwa kufungwa kutokana na kutokuwa na sifa za watumishi, vifaa na majengo yanayopaswa kwa mujibu wa taratibu za sasa za Wizara ya Afya.

b. Tunawapongeza wafadhili wote ambao wanafadhili miradi mbalimbali ya afya au shughuli zinazoinua kiwango cha afya ya mwananchi hapa Wilayani nazo ni:- Uzazi wa mpango, (Family planning), Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mama na mtoto (SCPD), Mpango wa Chanjo (EPI), Mradi wa HESAWA, Udhibiti wa Kifua Kikuu na Ukoma (TB and Leprosy Control Programme), Udhibiti wa Ueneaji wa UKIMWI (NACP), Udhibiti wa ueneaji wa magonjwa ya Kuhara (CDD), n.k Wananchi walio wengi wamefaidika na wataendelea kufaidika na huduma zilizotolewa na miradi hiyo ya kitaifa au kanda ya ziwa, pasipo kuzisahau siku za chanjo za Kitaifa (NIDs) dhidi ya ugonjwa wa “Kupooza” ambapo wilaya yetu kwa awamu mbili (1996) tulivuka lengo la kitaifa (95%).


c. Ni jambo la kujivunia pia kuwa: Wilaya ya Musoma Mjini ndiyo imeongoza kitaifa kwa tathimini ya kwanza katika utekelezaji wa mfumo wa taarifa za uendeshaji huduma za afya (MTUHA).

d. Sambamba na vituo vya afya, ndani ya Wilaya hii tunavienzi vyama vya hiari kwa ajili ya kuboresha maisha ya welemavu Tanzania (CHAWATA), Chama cha Maalbino, Chama cha wasioona, na vyama vinginevyo kama vile The Lions Club, Msalaba Mwekundu (Red Cross) n.k.

iv. Ushirika
Ni masikitiko makubwa kuwa chama Kikuu cha Ushirika Mkoani Mara (MCU- 1984 Ltd) kimefilisiwa na kufutwa katika kipindi hiki, kutokana na kushindwa kujiendesha kifedha, ikiwa ni athari zitokanazo na uongozi mbaya, ubadhirifu, ulafi (Institutionalized greedy), na malimbikizo ya riba kubwa ya NBC.

x. Maji
Ukosefu wa maji kwa maeneo mengi ya wilaya bado ni tatizo linalohitaji ufumbuzi wa kudumu. Aidha kuna baadhi ya sehemu zenye mabomba ambazo bado hazipati maji kwa mashine kushindwa kusukuma maji.

Tunaushukuru mpango wa Hesawa kwa kutuchimbia kisima kimoja cha maji huko Bweri. Ni vema kama Hesawa itaendelea na msaada wa jinsi hiyo kwa maeneo mengine ya mji wetu.

Ikumbukwe kwamba, watu wengi wanaopata maji kutoka ziwani au mtoni wanayatumia hivyo hivyo tu, bila kuyachemsha wala kuchujwa. Ni vema elimu hiyo isambazwe na kuenea kwa watu wote ili tuweze kudhibiti magonjwa yasababishwayo na kunywa maji machafu na yasiyo salama.
Jumla ya vituo vya maji bomba 5 vimejengwa katika kipidi hiki.

xi. Barabara
Barabara kuu ya Nyerere inahitaji kufanyiwa ukarabati na pia kupanuliwa. Barabara zingine za ndani zina hali mbaya. Ni vema zikarabatiwe na kuwekewa mitaro kwa kutumia njia ya kuwashirikisha wananchi.
Aidha, Halmashauri ya Mji inapaswa kufikiri namna ya kurejesha Taa za barabarani ili kuongeza mwanga na kwa ajili ya usalama nyakati za usiku.

Jumla ya barabara 20 mpya zilitengenezwa katika Kata ya Kigera eneo la Kwangwa ‘A’ zinapaswa kutunzwa. Barabara zilitengenezwa kwa juhudi zangu nikishirikiana na Halmashauri ya Mji na wakazi wa maeneo hayo,

xii. Burudani na Michezo
Wilaya inatoa pongezi za dhati kwa kanisa Katoliki kwa kukiendesha kituo cha Michezo kwa vijana (Hope Centre) kinachopakana na Kituo cha Utamaduni cha Musoma (MCC). FAT Wilaya na Baraza la Michezo (W) wanapaswa kuwa na mikakati madhubuti kwa kuwashirikisha wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo Timu yetu ya Maji F.C. iliyoko daraja la I Taifa.
Idara zihusike kuwashirikisha wananchi na wafadhili mbalimbali kushughulikia kasoro za wazi zinazoonekana kwa mfano kutokamilika kwa uwanja wa kumbukumbu ya Karume, kutokuwa na kituo cha michezo ya watoto wadogo, ukosefu wa bustani nzuri ya kupumzikia na upungufu wa vikundi vya kudumu vya usanii katika fani zake (k.v. maonyesho, lugha na ufundi).

xiii. Umeme
Nishati hii inaendelea kusambazwa na kusimamiwa na shirika la Umma TANESCO. Kwa sasa umeme unaotolewa ni wa uhakika. Tatizo bado ni wanachama wengi kushindwa kumudu gharama za kuingiza (Installation charges) umeme katika nyumba zao.

xiv. Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi
Katika kipindi hiki kumekuepo na mabadiliko ya mitambo ya njia za simu katika mji wa Musoma na via yake. Kitu ambacho kimeongeza uthamani wa huduma za simu. Zipo ofisi chache Musoma zenye huduma za Fax, Telex na E-Mail. Shirika la Posta limeendeleea kutoa huduma ya kusafirisha na kupokea barua, vifurushi na vipeto.

Njia zote za usafiri na uchukuzi hutumika kuingia au kutoka nje ya Wilaya hii. Kwa mfano:-
a. Nchi Kavu:
Kuna magari mengi madogo na makubwa ya abiria, kwenda sehemu zote.
b. Majini Kuna mitumbwi, na boti za watu binafsi, Meli mara nyingi hutumika kwa ajili ya kusafirisha mizigo (shehena) badala ya abiria.
c. Angani: Shirika la Ndege Tanzania (ATC), JWTZ na wakati fulani mashirika binafsi yanayomiliki ndege ndogo kama vile MAF na AIM n.k. yanaendelea kuutumia uwanja wa ndege wa Musoma kubeba au kuteremsha mizigo, hali Kadhalika, kusafirisha abiria.

Aidha wananchi tunasikiliza redio na kupata magazeti mengi siku hizi. Wachache kati ya wakaazi wa mji wetu wamebahatika kuwa na vyombo vya Televisheni (T.V Sets) vinavyowawezesha kuona na kusikia habari za dunia hii kwa kupitia studio za nchi za nje. Hata hivyo wengine wengi wamekuwa wakifika kwenye kituo chetu cha Utamaduni (Musoma Cultural Centre), kwenye kumbi mbalimbali za burudani, kwa ajili ya kuona na kusikiliza matangazo ya televisheni.

xv. Kilimo, Ufugaji na Uvuvi
Hizi ndizo shughuli kubwa wanazojishirikisha wananchi wa Wilaya ya Musoma Mjini kwa ajili ya maisha yao.

Kwa ujumla kinachoonekana ni kwamba shughuli hizi zinaleta pato dogo sana kwa wananchi wa Wilaya kwa ujumla kwa vile bado hatujatumia sayansi na teknolojia kwa wingi katika shughuli hizo. Aidha, bado wengi wetu hatufuati kanuni na maelekezo ya kilimo, ufugaji au uvuvi wa kisasa.
Katika kipindi hiki, tatizo kubwa lililojitokeza ni ukame wa muda mrefu uliosababisha njaa katika wilaya yetu.
Tunaushukuru Serikali kwa kutuletea chakula cha msaada kuokoa maisha yetu. Kazi ya uvuvi imeathirika na matatizo mbalimbali kama vile kuenea kwa magugu maji yanayoua samaki na uvuvi haramu kwa kutumia sumu; kitu ambacho kimeathiri soko la minofu ya samaki wetu huko nje. Ni vema kuwa idara ya Mali Asili na vyombo vya dola visaidie kuwakamata wahalifu wote na kuwaadhibu ipasavyo. Hata hivyo ushirikiano wa wananchi wenyewe unahitajika kwa kiwango kikubwa. Uvuvi bora utaweza kuleta faida kubwa zaidi kwa kuliinua pato la Wana Musoma na Taifa letu kwa ujumla.

xvi. Viwanda
Pamoja na kuongezeka viwanda vipya hapa wilayani mfano: kiwanda cha magodoro, na viwanda vya kuandaa na kusafirisha minofu ya samaki, Chama kinasikitika juu ya kuanguka na kufungwa viwanda vyetu kama vile: kiwanda cha maziwa (Mara Milk),

Na kiwanda cha Nguo (MUTEX). Hii si tu imepunguza pato la mwananchi na Taifa, bali pia imepunguza ajira kwa vijana.
Utaratibu wa kuona kama upo uwezekano kwa kuvibinafsisha au kuingia ubia unaendelea kufanywa. Kiwanda cha soda za Vimto na SIDO bado vinaendelea kutoa huduma.

xvii. Mashirika / Makampuni ya Umma
Katika wilaya yetu yapo makampuni au mashirika yanayofanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii nayo ni:-

a. Benki ya Taifa ya Biashara (NMB) kwa sasa inaelekea kufanyiwa marekebisho makubwa na kuundwa upya, baada ya kuwa imefunga baadhi ya matawi yake. Kwa mfano Mukendo hapa Wilayani. Ni vema tuwaeleweshe wananchi mababadiliko haya ili wasipoteze uteja wao ambao ni ufalme na unahitajika sana kwa Taasisi mpya ya NMB 1997.
b. CRDB (1996) Ltd. Tawi limezinduliwa rasmi hivi karibuni, na Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere.
c. Kampuni ya simu (Telecom Company), kama ilivyokwisha kufafanuliwa mapema. Imeshauriwa vibanda vya simu viwekwe angalau kimoja kwa kila Kata.
d. Shirika la Posta na Benki ya Akiba limefunga pia baadhi ya matawi yake madogo. Vituo vilivyobaki vinaendelea kutoa huduma ya kusafirisha barua na vifurushi na kutunza fedha za watu katika akaunti kwenye benki ya posta. Hata hivyo tumeweza kupata huduma za utumiaji barua / vifurushi kwa haraka zaidi; kwa njia ya EMS na pia Money Fax inayowezasha kutuma fedha kwa haraka zaidi na usalama.
e. Kampuni ya Biashara ya Mkoa (RTC). Hii imefunga huduma zake kutokana na kushindwa kujiendesha, katika mfumo huu wa uchumi wa soko huria.
f. Shirika la Bima la Taifa (NIC), lienaendelea kutoa huduma ya kuwawekea bima watu, na mali zao kupitia ofisi yake kuu na mawakala wake.
g. Shirika la Taifa la Akiba ya Uzeeni (NPF); hili lina wateja wengi hususani, wafanyakazi wote wanaopaswa kujiunga na NPF kwa mujibu wa sheria. Tunashauri shirika liwe linatuma taarifa (statement) za jumla ya mafao ya wateja wao angalau mara moja kwa mwaka ili kuwafundisha kuhusu amana zao.
h. Shirika la nyumba la Taifa (NHC). Shirika hili linazo nyumba chache sana kulingana na mahitaji ya nyumba kwa wakazi, hasa watumishi wageni Wilayani, watumishi wa Serikali na mashirika ya umma na binafsi. Hata hivyo zile ziliaopo ni chakavu; ni vema kama zitakuwa zikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara kabla uharibifu haujawa mkubwa. Kwani “Usipoziba ufa utajenga ukuta”.
i. Shirika la Maendeleo ya Wilaya (MUDECO); tofauti na jina lake, shirika hili lilikosa maendeleo kabisa hatimaye likafunga shughuli zake. Hii ilitoka ilitokana na kujiendesha kwa hasara na zaidi watu binafsi kujiondoa na kuondoa hisa zao. Hata hivyo mali (mtaji wa shirika) zilikuwa zinaibiwa mara kwa mara, kitu ambacho kilidhoofisha shirika.

xviii. Biashara na masoko
Dhamana ya masoko inagusa mambo makuu manne. Bidhaa/huduma itolewayo, bei yake, kutangazwa kwake na mahali pa kutokea/ kuuzia bidhaa / huduma. Hivyo kabla ya kuongelea biashara au masoko, Chama kinatuasa kuhakikisha kuwa tunazalisha bidhaa bora, za kutosha au tunatoa huduma za kuridhisha.

Ni vema Halmashauri ya Mji ifanye utafiti wa kina kuhusu kodi na ushuru unaofaa kutozwa kwa wafanyabiashara katika masoko yetu na penginepo katika vibanda au nyumba zao.

Inashauriwa kuwa: wafanyabiashara wadogo wadogo kama vile wanaong’arisha viatu, vinyozi n.k. wapewe nafasi za kustawi kwa kupunguziwa kodi, na utaratibu uwepo wa kuwapatia wote wenye leseni vitambulisho ili wasisumbuliwe kama wazururaji. Hata hivyo, itakuwa busara kama Halmashauri ya Mji wetu itaangalia uwezekano au itaandaa mkakati mpya utakaoiwezesha kukusanya ushuru wa vituo vya taxi na magari madogo ya abiria, kwa kuwa sasa, magari haya yanafanya kazi zao vichochoroni kwa kujificha, hivyo kuikosesha Halmashauri mapato yake.

xix. Hifadhi ya Mazingira
CCM inaendelea kutetea mazingira tunamoishi. Serikali Kuu na Serikali ya Mji waendelee kusimamia usafi na utunzaji wa mazingira. Aidha, hatua kali zichukuliwe dhidi ya wachafuzi wa mazingira kwa mfano: wanaokata miti ovyo, kuchoma nyasi, wachafuzi wa hali ya hewa kutoka viwandani, magari na kadhalika. kuwepo na kampeni kamambe ya kudumu ya kila mwananchi kupanda na kutunza miti.

Elimu kuhusu hifadhi ya Mazingira itolewe mashuleni na zaidi kwenye Mpango wa Elimu ya Watu Wazima.



xx. Nafasi, haki na wajibu wa Jumuiya za Wafanyakazi, Vijana na wanawake.
a. Wafanyakazi: Serikali ivitambue vyama huru vya Wafanyakazi vilivyoshirikishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Tanzania (TFTU). Serikali isisitize juu ya haki na stahili za watumishi, mazingira ya kazi na vitendea kazi sambamba na nidhamu na uwajibikaji kazini. Tatizo la mishahara kuchelewa limeendelea kuwepo. Serikali ilitafutie ufumbuzi wa kudumu.
b. Vijana: Umoja wao ndani ya CCM uimarishwe na wahamasishwe ili washiriki katika kuzalisha mali kwa moyo.
c. Wanawake: Serikali iendeleze vita dhidi ya desturi na mila mbovu zinazowadhalilisha wanawake kijinsia. Wanawake wapewe nafasi sawa na Wanaume kwa kadri ya uwezo wao.

xxi. Huduma zaDini katika jamii
Wananchi wa mji wa Musoma wameendelea kupata huduma za kiroho kulingana na imani zao kwa kupitia kwenye madhehebu yao ya Kikristo Kiislamu, Kihindu n.k. Serikali ihakikishe kuwa waumini wanatatua na kusuluhisha migogoro yao wenyewe kama ipo ili kudumisha amani, usalama na utulivu.

III. NASAHA ZANGU BAADA YA MIAKA KUMI NA MITANO (15) KATIKA UONGOZI

Kipengele hiki kinabeba nguvu na udhaifu wangu kwa pamoja. Kwa muhtasari, ninakusudia kuwashirikisha katika mawazo au ndoto zangu juu ya mambo muhimu niliyoyaona katika kipindi hiki cha miaka kumi na mitano yanahitaji marekebisho, kuondolewa au kusisitizwa kwa ajili ya maendeleo ya mwananchi mkazi wa Musoma Mjini.

Ndugu Wajumbe, kuweni huru kukubali au kutokubaliana nami maana huenda sikunukuu kutoka kwenye Katiba ya CCM, Mwongozo wa CCM, Programu ya Chama, Ilani ya Uchaguzi wala popote:-

a. Ukabila:Matumizi ya ukabila kwa gharama ya kumbagua mtu kutoka katika stahili au haki fulani,ni ugonjwa sugu ambao umesitisha maendeleo ya Musoma na Mkoa wetu wa Mara kwa ujumla. Tubadilike, tumkemee yeyote mwenye nia ya kutugawa kwa makabila ya lugha na sehemu tulizozaliwa.
b. Utamaduni wa uoga na kulindana:Maadili na miiko ya kiongozi kwa mujibu wa Katiba yanaendelea kusimama kidete, kama mti wenye mizizi mirefu bila kijali kimbunga kizungukacho. Kiongozi yeyote anayepotosha au kukubali kupotashwa kwa mahesabu ya kulinda maslahi ya wachache anyang’anywe dhamana aliyopewa mara moja; hata kama iko katikati ya meno yake …… Haki huliinua Taifa ……

c. Kazi ya Kujitolea:Ninashauri vikao vya CCM Taifa viangalie kwa upya muundo wa Chama na ikiwezekana virejeshe maslahi ya Watendaji wote kutoka ngazi za matawini hadi Taifa.

d. Kutowajibika Mkosefu:Mwanadamu anapaswa kutunukiwa kulingana na kazi aliyofanya, “nzuri au mbaya”. Kama wanafahamika kwa nini Chama kisiwajibishe wale wote wasionia mamoja nasi? Kwa mfano:- Waliokusanya michango ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wakaitumia. Waliofilisi M.C.U. (1984) Ltd pasipo kupewa kibali cha kuwa “Mfilisi”.

e) Kutokutii kanuni za menajimenti (Esprit de Corp and Unity of Direction)
Ni gharama kubwa sana kwa Chama, mtu au watu kuvunja kipande cha mnyororo Kinachounganisha Shina, Tawi, Mkoa au Taifa. Wakati mwingine tukubali kutokubaliana, lakini tubakie na umoja ushirikisha wetu, kama Chama.

f) Haki ya Kikatiba:
Wananchi sehemu moja au nyingine wameshuhudia kwa uchungu maumivu ya miaka Mitano ya kutawaliwa na sio kuongozwa na viongozi waisofaa kutokana na wananchi fulani kuamua kuuza haki zao za kupiga kura kwa thamani ya kitenge, chupa ya kinywaji, T-shirt n.k.


Kama ambavyo nimekuwa nikisema na kutenda, ieleweke wazi kuwa kiongozi achaguliwaye kwa kutoa fedha, ataongoza kwa kuchukua fedha, vilevile achaguliwaye kwa kufuata ukabila, atasimamia kabila, naye yule achaguliwaye kwa kampeni moto toka juu huenda akaondolewa kwa kampeni baridi kutoka chini. Aidha, ni kitendo cha kutokukomaa kisiasa, kujenga chuki na hasira kwa mtu yeyote eti kwa sababu ya kutokupigia kura, kukushinda kwenye uchaguzi au kuazimia kugombea nafasi uliyodhani umetengewa wewe pekeke.

IV. HITIMISHO:
Mungu, Muumbaji na Mpaji awabariki na kuwalinda nyote.
Ninawashukuruni wale wote tuliowahi kufanya kazi nao Wilayani, makatibu na Wajumbe wote.

Ninawapongezeni wale wote tulioshirikiana kwa dhati katika kampeni za uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge. Na katika Mji wetu wote waliochaguliwa ni wagombea kupitia Chama cha Mapinduzi.

Aidha Mgombea Urais na Mwenza wake kupitia CCM, ndio waliopata kura nyingi zaidi kuliko wagombea wa vyama vingine katika Wilaya yetu, katika uchaguzi Mkuu wa Taifa wa kwanza uliovishirikisha vyama vingi.

Ninawiwa deni kubwa na Idara, Taasisi zote za Serikali, Jumuiya za Chama na wananchi wote wa Musoma Mjini kwa: Kunisahihisha, kunitathmini, kuniongoza, kunifundisha na zaidi ya yote; kunipa dhamana hii, maana sasa nimekuwa kama dhahabu iliyopitishwa kwenye moto.

“TUJISAHIHISHE, TUSAHIHISHANE NA TUSAMEHEANE”

Mungu Ibariki CCM! Mungu Ibariki Musoma Mjini!





KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

2 comments:

Anonymous said...

HAYA MANENO YAKE NANUKUU NDYO YANAPASWA KUHUBIRIWA KOTE ULIMWENGUNI.

' Kama ambavyo nimekuwa nikisema na kutenda, ieleweke wazi kuwa kiongozi achaguliwaye kwa kutoa fedha, ataongoza kwa kuchukua fedha, vilevile achaguliwaye kwa kufuata ukabila, atasimamia kabila, naye yule achaguliwaye kwa kampeni moto toka juu huenda akaondolewa kwa kampeni baridi kutoka chini. Aidha, ni kitendo cha kutokukomaa kisiasa, kujenga chuki na hasira kwa mtu yeyote eti kwa sababu ya kutokupigia kura, kukushinda kwenye uchaguzi au kuazimia kugombea nafasi uliyodhani umetengewa wewe pekeke.'

Anonymous said...

Alikuwa Mzee wa shoka asiyeogopa kusema kweli.
Mungu amlaze pepa peponi